• ePaper
Thursday, October 22, 2026
  • Login
No Result
View All Result
Uhuru Publication
  • Habari
  • Michezo
  • Uchaguzi
  • Burudani
  • Toleo Maalumu
  • Kolamu
  • Makala
  • Hadithi
  • Habari
  • Michezo
  • Uchaguzi
  • Burudani
  • Toleo Maalumu
  • Kolamu
  • Makala
  • Hadithi
  • Login
No Result
View All Result
ePaper
Uhuru Publication
Home AFYA

UKURASA MPYA BIMA YA AFYA KWA WOTE

Abdurahman Jumanne by Abdurahman Jumanne
October 22, 2026
in AFYA, Habari, Kitaifa
0
UKURASA MPYA BIMA YA AFYA KWA WOTE
0
SHARES
3
VIEWS
Share on FacebookShare on Twitter

NA WAANDISHI WETU

TANZANIA imeingia ukurasa mpya katika sekta ya afya, baada ya kuzindua awamu ya pili ya mpango wa Bima ya Afya kwa Wote utakaosajili kaya 625,000.

Awamu hiyo itaongeza wigo wa usajili kwa kuhusisha wakulima, wafugaji, wavuvi, bodaboda, mama lishe, wafanyakazi wa kampuni binafsi na kila mwananchi mwenye uwezo wa kujilipia.

Awamu ya kwanza ya mpango huo, ilihusisha kupatiwa bima ya afya wananchi wasio na uwezo ambapo kaya 198,709 kati ya kaya 276,004 zisizo na uwezo zilihakikiwa na kupewa kadi sawa na asilimia 72 ya lengo.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mpango huo, mjini Mtwara, jana, kwa niaba ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, Waziri wa Afya, Mohammed Mchengerwa, alisema awamu ya kwanza Mkoa wa Mtwara uliongoza kitaifa kwa kufikia idadi kubwa ya walengwa.

“Katika awamu hii, mtapata bima kupitia Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) au kupitia kampuni binafsi za bima ya afya zilizoidhinishwa na serikali, chini ya usimamizi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA). Serikali imehakikisha kuna vifurushi vinavyozingatia mahitaji na uwezo wa wananchi,” alisema.

Alifafanua kwamba vifurushi si jambo geni kwani  hata kwenye simu kuna vifurushi vya siku, wiki hadi mwezi.

“Unachagua kifurushi kulingana na fedha uliyonayo. Katika bima ya afya utaratibu ni huo huo, unachagua kifurushi kulingana na uwezo wako wa kuchangia,” alisema.

Aliongeza kuwa, “Kwa wananchi wenye kipato cha kawaida, serikali imewafikia. Tumeweka kifurushi kinachoitwa Fahari ya Afya ambacho wananchi watapata huduma muhimu za afya kwa sh. 150,000 kwa mwaka kwa kaya ya watu wasiozidi sita. Ukijiunga na Fahari Afya unapata huduma kuanzia zahanati hadi hospitali ya taifa, kwa kufuata utaratibu wa rufaa.”

MAGEUZI MAKUBWA NHIF

Mchengerwa alisema katika kufanikisha mpango huo, NHIF imefanya mageuzi makubwa manne; kwanza ni kusogeza huduma kwa kuwafuata wananchi.

Alisema huduma hiyo itajumuisha usajili, uhakiki na malipo kwa njia ya kidijitali, kupitia mawakala na mtandao wa taasisi za fedha ili mwananchi asilazimike kusafiri hadi mjini kupata kadi.

Waziri Mchengerwa alieleza kuwa, mageuzi ya pili ni madai ya vituo vya afya yatalipwa kwa wakati, kwa sababu kituo kisicholipwa kwa wakati ni kituo kinachomrudisha mgonjwa nyumbani.

Mageuzi ya tatu ni mifumo ya kidijitali kuonyesha nani amesajiliwa, nani ametibiwa, nani amelipwa na kila senti itaonekana.

Alibainisha kuwa, mageuzi ya nne ni NHIF kuzingatia huduma bora yenye kulingana na mahitaji husika ya mgonjwa.

“Mageuzi ya NHIF yamejumuishwa kimkakati katika ajenda pana ya mabadiliko ya sekta ya afya chini ya uongozi na usimamizi wa wizara.

“Kwa sababu Watanzania wanastahili ukweli. Hii siyo fimbo ya mchawi. Mageuzi ni safari. Hatuanzi tukiwa wakamilifu. Tunaanza tukiwa wenye dhamira na dhamira ndiyo imejenga kila jambo kubwa katika historia ya taifa hili,” alisisitiza.

MABALOZI KILA WILAYA

Mchengerwa alisema katika kufanikisha mpango huo, wizara itateua mabalozi wa Bima ya Afya kwa Wote kutoka nyanja mbalimbali.

Alisema mabalozi hao watahusishwa watu wenye ushawishi chanya ambao ni viongozi wa dini, mila, walimu, wataalamu wa afya, wasanii, wanamichezo, wafanyabiashara, wakulima, wafugaji, wavuvi, viongozi wanawake, vijana, wazee na watu wenye ulemavu.

“Kila kundi lina watu wanaoliamini, tunataka imani hiyo iwe daraja la kuwafikishia wananchi elimu na kuwahamasisha kujiunga na bima ya afya. Mabalozi hawa watakuwa na wajibu unaopimika.

Watashirikiana na uongozi wa wilaya kuelimisha, kuhamasisha na kuhakikisha wilaya yao inafikia lengo la uandikishaji,” alisisitiza.

ONYO  LATOLEWA

Waziri Mchengerwa alisema Bima ya Afya kwa Wote ni mali ya kila mwananchi, hivyo kila mmoja ana wajibu wa kuulinda mpango huo.

“Tusikubali kuuharibu mpango huu kwa udanganyifu. Tusitumie kadi ya bima ya mtu mwingine. Tusitoe taarifa za uongo kupata huduma tusizostahili. Mtoa huduma asidai malipo ya mgonjwa ambaye hakumtibu.

Mwananchi asijifanye maskini ili alipiwe na serikali wakati ana uwezo, kwa sababu kila shilingi anayoichukua kwa hila ni shilingi anayonyang’anywa yule asiye nacho kweli,” alitahadharisha.

Aliongeza: “Udanganyifu wa mtu mmoja unaweza kuathiri manufaa ya wengi. Kadi moja ya uongo ni tone la sumu kisimani na wote tunakunywa maji yale yale.”

KIPIMO KWA MA-RC, DC 

Katika uzinduzi huo, alisema kuanzia sasa uandikishaji wa bima ya afya ni kipimo cha uongozi wa wakuu wa mikoa na wilaya.

Alisema mkoa utakaokuwa kinara kwa uandikishaji na ule utakaoshika mkia, taarifa zitafikishwa kwa Rais Dk. Samia.

“Tutapimaje kama tumefanikiwa? Tutapima mageuzi haya ya afya kwa hofu inayoondolewa kwenye kaya na heshima inayorudishwa kwa mgonjwa. Siku mama wa Tandahimba atakapolala usiku bila hofu ya homa ya mtoto wake, siku hiyo ndiyo tutasema tumefanikiwa.

“Mtoto huyo hatajua kuwa mama yake aliwahi kutazama chini. Kwa sababu mama huyo hatakuwepo tena. Badala yake atakuwepo mama anayetazama juu, anayetabasamu, anayesema: Nina kadi. Nina haki. Nina taifa langu nyuma yangu,” alieleza.

Awali, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dk. Grace Magembe alisema wizara hiyo itaendelea kuimarisha mifumo ya Teknolojia ya Hbari na Mawasiliano (TEHAMA), usimamizi wa dawa na vifaa tiba ili kuhakikisha utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote unaenda sambamba na utoaji wa huduma bora kwa wananchi.

Alisema wizara yake itaendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali, ikiwemo Ofisi ya Waziri Mkuu-TAMISEMI na wadau wengine, kuimarisha mifumo ya utoaji huduma na kuhakikisha mapato yatakayopatikana kupitia bima hiyo yanaelekezwa katika kuboresha huduma za afya.

Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Donald Msengi, alisema mkoa huo utaendelea kuunga mkono juhudi za serikali kuhamasisha wananchi kujiunga na Bima ya Afya kwa Wote kupata huduma bora za afya. Alisema viongozi na watendaji wa mkoa huo wana wajibu kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi kuhusu mpango huo.

Previous Post

KIKOMO BEI ZA MAFUTA ZINAVYO MLINDA MWANANCHI

Next Post

SERIKALI YAENDELEA KUBORESHA URATIBU WA MAFUNZO TARAJALI

Next Post
SERIKALI YAENDELEA KUBORESHA URATIBU WA MAFUNZO TARAJALI

SERIKALI YAENDELEA KUBORESHA URATIBU WA MAFUNZO TARAJALI

Leave a Reply Cancel reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Recommended

IGP MSTAAFU MANGU AWAASA WATANZANIA KUEPUKA VISHAWISHI VYA KUVUNJA AMANI

IGP MSTAAFU MANGU AWAASA WATANZANIA KUEPUKA VISHAWISHI VYA KUVUNJA AMANI

6 months ago
DK. NCHIMBI AAHIDI HUDUMA ZA AFYA KWA WATANZANIA

DK. NCHIMBI AAHIDI HUDUMA ZA AFYA KWA WATANZANIA

1 year ago

Popular News

  • SERIKALI YAENDELEA KUBORESHA URATIBU WA MAFUNZO TARAJALI

    SERIKALI YAENDELEA KUBORESHA URATIBU WA MAFUNZO TARAJALI

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • UKURASA MPYA BIMA YA AFYA KWA WOTE

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • KIKOMO BEI ZA MAFUTA ZINAVYO MLINDA MWANANCHI

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • DOUMBIA AFUNGUA AKAUNTI YA MABAO

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • WAZIRI MKUU ATETA NA MAKAMU WA RAIS WA IFAD

    0 shares
    Share 0 Tweet 0

Stay Update, Subscribe Now!

Check your inbox or spam folder to confirm your subscription.

Ukurasa Rasmi wa Televisheni ya Gazeti la Uhuru.

Facebook-f Instagram X-twitter Youtube tiktok
Quick Links
  • Habari
  • Michezo
  • Uchaguzi
  • Burudani
  • Toleo Maalum
  • Kolamu
  • Makala
Services
  • ePaper
Contact Information
  • Dar es Salaam,Tanzania
  • info@upl.co.tz
  • +255 783 925 742
Uhuru Publications , 2025 © All Rights Reserved
  • Terms & Conditions
  • Privacy Policy
  • FAQ
No Result
View All Result
  • Home
  • Habari
  • Michezo
  • Uchaguzi
  • Burudani
  • Toleo Maalumu
  • Kolamu
  • Makala
  • Contact
  • Hadithi

© 2026 JNews - Premium WordPress news & magazine theme by Jegtheme.

Not enough quota to unlock this post
Unlock left : 0
Are you sure want to cancel subscription?