Na MWANDISHI WETU
WATANZANIA wametakiwa kuwa na utaratibu wa kupima saratani ya matiti, kuhakikisha wanagundua mapema kama wana dalili ili kuanza kupatiwa matibabu.
Mwaka huu uhamasishaji kuhusu saratani ya matiti umekuja na kauli mbiu ‘Kila Simulizi ni ya Kipekee, Kila Hatua ina Thamani’, inayosisitiza umuhimu wa taarifa sahihi, huduma zinazofaa na msaada kwa watu walioathiriwa na ugonjwa huo.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Meneja Mkuu wa Masoko na Mawasiliano wa Benki ya Exim, Kauthar D’souza, amesema kuna umuhimu wa utambuzi wa mapema na upatikanaji wa huduma za uchunguzi na matibabu kwa wakati ili kuboresha matokeo ya matibabu na kupunguza vifo kwa kushirikiana na Taasisi ya Saratani Ocean Road.
Alisema afya ya Watanzania kwa ujumla ni muhimu, hivyo kujitokeza na kupata vipimo mapema, kunasaidia kupata utambuzi ikiwemo kuanza matibabu ya haraka.
“Afya ya jamii inahitaji ushirikiano na hatua za pamoja, tumekuwa tukishirikiana na wataalamu kutoka Taasisi ya Saratani Ocean Road kuhakikisha Watanzania wanapata taarifa sahihi kuhusu afya na kuelewa umuhimu wa kuchukua hatua kwa wakati.
Kwa upande wake, Daktari wa Ocean Road, Maguha Stephano alisema kuwa kuelimisha jamii na kuhamasisha watu kutafuta huduma za afya mapema ni sehemu muhimu ya juhudi za kukabiliana na saratani ya matiti.




