Na IRENE MWASOMOLA
MWENYEKITI wa Taasisi ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere na waziri katika awamu tofauti, Paul Kimiti, amefunguka namna suala la kuhamishia Makao Makuu ya Serikali Dodoma, lilivyokuwa gumu kwa baadhi ya mawaziri enzi za Hayati Mwalimu Julius Nyerere, huku akipongeza kufanikiwa kwa mpango huo na ujenzi wa Mji wa Serikali Mtumba.
Pia, amemshukuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan na Hayati Dk. John Pombe Magufuli, kwa kukamilisha maono ya Mwalimu Nyerere ya kuhakikisha Serikali inahamia Dodoma.
SIMULIZI YA SAFARI
Akizungumza na gazeti hili, jana, Kimiti alisema, wakati Mwalimu Nyerere analeta mpango wa kuhamia Dodoma wakati huo alikuwa Waziri katika Ofisi ya Waziri Mkuu na kwamba, viongozi wa kwanza waliotekeleza maagizo hayo ni yeye, Anna Makinda na Getruda Mongella.
Kwa mujibu wa Kimiti, wakati huo Waziri Mkuu alikuwa Edward Sokoine, ambaye aliagiza mawaziri wa ofisi yake kuhamia Dodoma, huku mawaziri wengine wakibaki Dar es Salaam.
“Wakati huo nilikuwa Ofisi ya Waziri Mkuu, ilikuwa kazi kubwa kwa kuwa mawaziri wote walibaki Dar es Salaam, sisi Ofisi ya Waziri Mkuu, ambayo tuna ratibu, tukitaka taarifa ilitulazimu kwenda Dar es Salaam, kilikuwa kipindi kigumu kwetu, sisi tuli ‘enjoy’ (tulifurahia) kukaa Dodoma, lakini wenzetu wakaona mzigo,”alisimulia.
Aidha, Kimiti alisema wakati huo vikao vya Bunge vilianza kufanyika Dodoma, katika Ofisi Ndogo za Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Kimiti alisimulia zaidi, baada ya hapo aliona mwitikio wa kuhamia Dodoma, ukisuasua na baadhi ya mawaziri walianza kurejea Dar es Salaam.
Alisema aliamua kuuza maeneo yake, ambayo aliyanunua likiwamo moja lililokuwa Msalato na baadaye alirudi Dar es Salaam.
Hata hivyo, Kimiti alisema baada ya muda mrefu kupitia Rais Magufuli alipoingia madarakani aliendeleza mpango wa Serikali kuhamia Dodoma.
“Namshukuru Rais na mtangulizi wake Magufuli kwa uamuzi na misimamo yao, ndiyo maana namsifia Mama ninapotumia ile kaulimbiu yake ya ‘Kazi Iendelee’, maana yake waliyoanzisha wenzake kama ni mazuri atayaendeleza,” alisema.
Mwenyekiti huyo wa Taasisi ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, alisema anafurahi kushuhudia maono ya Mwalimu Nyerere yametimia na Serikali imehamia Dodoma.
MAKUMBUSHO YA NYERERE DODOMA
Aidha, Kimiti aliiomba Serikali kutenga eneo la kujenga kumbukumbu ya Makumbusho ya Hayati Mwalimu Nyerere jijini Dodoma.
Kwa mujibu wa Kimiti, Butiama ni eneo dogo, hivyo kwa kua Serikali imeshahamia Dodoma, ni vyema Makumbusho ya Mwalimu Nyerere nayo yawe katika jiji hilo.
Alisema mwaka juzi, Serikali ilitenga sh. bilioni moja kutekeleza ujenzi wa makumbusho hiyo, lakini anaona kasi ya utekelezaji ni ndogo.
“Tutafute eneo zuri sasa heshima na ‘legacy’ yake ihamie Dodoma, tuweke kumbukumbu tupate eneo kubwa tuweke na wananyama wadogogo, kuwe na ‘conference centre’ (kituo cha mikutano), ‘swimming pool’ (bwawa la kuogelea), tunapokuja Dodoma tusije kuangalia majengo tu, tuangalie na kumbukumbu ya Baba wa Taifa na mambo aliyoyapenda,” aliongeza.
RAIS
Juzi Rais Dk. Samia alizindua Mji wa Serikali Mtumba, uliojumuisha majengo ya ofisi za wizara, taasisi za serikali, barabara za lami na miundombinu mingine.
Akizungumza baada ya kuzindua mradi huo, Rais Dk. Samia aliwataka watendaji wa Serikali kuhakikisha huduma zinawafikia wananchi walipo kupitia mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).
Rais alisisitiza matumizi ya TEHAMA kutowalazimisha wananchi kusafiri hadi makao makuu ya nchi Dodoma, kufuatilia huduma zinazoweza kupatikana katika maeneo yao.
Pia, alisisitiza mifumo ya TEHAMA katika wizara na taasisi za serikali inapaswa kuunganishwa kurahisisha upatikanaji wa taarifa, kupunguza urasimu na kuondoa utaratibu wa mwananchi kuwasilisha taarifa zilezile katika taasisi mbalimbali za serikali.
Rais Dk. Samia alisema kukamilika kwa miradi hiyo, kunapaswa kwenda pamoja na uboreshaji wa utoaji huduma kwa wananchi.
Alitoa mfano wa mwananchi kutoka Rukwa, Kagera, Mtwara au Kigoma, hapaswi kutumia muda na fedha nyingi kufika Dodoma kufuatilia jambo ambalo linaweza kushughulikiwa katika eneo analoishi.
SAFARI YA DODOMA
Safari ya Serikali kuhamia Dodoma inatajwa kihistoria ilianza mwaka 1966, baada ya Joseph Nyerere, mdogo wa Mwalimu Julius Nyerere, kuwasilisha hoja binafsi bungeni ya kutaka Dodoma iwe Makao Makuu ya Serikali.
Hata hivyo, mwaka 1973 Mwalimu Nyerere aliwasilisha katika kikao cha Halmashauri Kuu ya TANU pendekezo la Mji wa Dodoma, kuwa Makao Makuu ya Serikali, na kusema sharti liungwe mkono na matawi ya Chama nchini pote.
Baadaye Mwalimu Nyerere aliutangazia umma uamuzi wa kuufanya Mji wa Dodoma, kuwa Makao Makuu ya Serikali. Kazi ya kuuendeleza mji huo ikaanza.
Mwaka 1974 hadi 1978, baadhi ya hatua zilichukuliwa, ikiwa ni pamoja na Waziri Mkuu Rashid Kawawa, kuhamia Dodoma.
Mwaka 1978, Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu(CDA), ilianzishwa kusimamia ujenzi wa jiji la Dodoma. Hata hivyo, mchakato ulisuasua kwa miaka kadhaa kutokana na changamoto mbalimbali.
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilianza rasmi shughuli zake mkoani Dodoma, Februari mwaka 1996.
Mwaka 2000, Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, alielekeza kujengwa kwa ukumbi mpya wa Bunge uliopo Dodoma hadi sasa, kufuatia ukumbi wa awali kutokuwa mahususi kwa shughuli za kibunge.
Kazi haikuwa rahisi kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo za kiuchumi, safari ikawa ndefu na tangu 1973 hadi mwaka 2026, Rais Dk. Samia alipozindua Mji huo wa Serikali Mtumba, ikiwa ni miaka 53.
Rais Dk. Samia aliwahi kusema, kazi ilikuwa ngumu na ilikuwa ni jukumu la kila awamu iliyoingia madarakani kuwezesha kuanza ujenzi wa vitu mbalimbali ili Dodoma, ichukue sura ya kuwa Makao Makuu ya Serikali.
Julai 23, 2016, Rais wa Awamu ya Tano, Dk. Magufuli, aliukumbusha Mkutano Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kuhusu uamuzi wa kuhamishia rasmi shughuli za Serikali kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma.
Baada ya hapo, utekelezaji wa miradi mbalimbali ndani ya jiji la Dodoma uliendelea kwa kasi zaidi ikiwemo ujenzi wa Ikulu ya Chamwino, ambayo eneo lake liliongezwa kutoka ekari 66 hadi 8, 473, ndipo unjenzi wa jengo jipya la Ikulu ukaanza, na kuzinduliwa na Rais Dk. Samia Mei 20, 2023.
Oktoba 30, 2026, Rais Dk. Samia majengo ya ofisi za wizara 26, taasisi za Serikali na kilometa za barabara za lami katika Mji huo wa Serikali Mtumba.




