Na ATHNATH MKIRAMWENI
TANZANIA na Angola zimefungua fursa mpya za kiuchumi, baada ya kuchukua hatua mbalimbali za kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia, wenye lengo la kuchochea ukuaji wa uchumi.
Miongoni mwa hatua hizo ni kuandaa kongamano la biashara na uwekezaji, kuunganisha Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA) na Benguela nchini Angola, kuanzisha safari za moja kwa moja za anga na kupanua uwekezaji katika sekta za mafuta, gesi na madini.
Hatua hizo zimechukuliwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Angola, João Lourenço, baada ya mazungumzo rasmi yaliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari, Rais Dk. Samia, alisema mbali na Tanzania, Angola kuwa na uhusiano mzuri wa kihistoria, ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara ni mdogo.
Kwa sababu hiyo, viongozi hao wamekubaliana kuchukua hatua za kuimarisha uhusiano kwa manufaa ya mataifa yao.
Alisema miongoni mwa hatua hizo ni kuandaa kongamano la biashara na uwekezaji, litakalowakutanisha wafanyabiashara na sekta binafsi kutambua fursa zilizopo na kuongeza shughuli za kibiashara na uwekezaji.
“Licha ya uhusiano wetu mzuri, bado uhusiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya Tanzania na Angola ni mdogo sana, hivyo tumekubaliana kuandaa kongamano la biashara na uwekezaji ambapo wafanyabiashara wetu na sekta binafsi waweze kuangalia maeneo ya kushirikiana na kufanya biashara, “alisema.
Katika sekta ya usafirishaji, alisema nchi hizo zimekubaliana kuimarisha uunganishaji wa Reli ya TAZARA na Reli ya Benguela kuunganisha Bandari ya Dar es Salaam katika Bahari ya Hindi na Bandari ya Lobito nchini Angola katika Bahari ya Atlantiki.
Alisema kukamilika mipango hiyo na ukarabati wa reli hizo, kutarahisisha usafirishaji bidhaa na kuongeza fursa za biashara kati ya nchi hizo na maeneo mengine yatakayounganishwa na miundombinu hiyo.
Rais Dk. Samia alisema Tanzania na Angola zimetia saini mkataba wa huduma za usafiri wa anga, utakaowezesha kuanzishwa safari za moja kwa moja kati ya nchi hizo, hatua inayolenga kurahisisha safari za wafanyabiashara, watalii na kuchochea shughuli za kiuchumi.
Katika sekta ya mafuta na gesi, alisema Angola imeikaribisha Tanzania kushirikiana katika miradi ya usafishaji mafuta, huku Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), likiwa limeanza mchakato wa kuchunguza uwezekano wa kushiriki katika miradi hiyo ikiwemo unaohusishwa na Lobito.
“TPDC iharakishe mchakato wa kutathmini uwezekano wa kuingia ubia katika miradi ya mafuta ya Lobito nchini Angola, Tanzania iweze kunufaika na fursa za uwekezaji, kuongeza thamani ya rasilimali za mafuta na gesi na kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kati ya nchi hizi mbili,” alisema.
Alisema nchi hizo pia zimekubaliana kubadilishana uzoefu katika sekta ya madini, kuwajengea uwezo wachimbaji wadogo, wataalamu na kuongeza thamani ya madini ili rasilimali hizo zileta manufaa zaidi ya kiuchumi.
TANZANIA KUFUNGUA UBALOZI
Katika kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia, Rais Dk. Samia alisema Tanzania imefungua tena ubalozi wake nchini Angola na hivi karibuni atateua balozi atakayesaidia kuratibu shughuli za ushirikiano kati ya mataifa hayo.
“Tumekubaliana kufungua tena ubalozi wa Tanzania nchini Angola na hivi karibuni nitateua Balozi tuweze kufanya kazi kwa karibu zaidi, kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na kupanua ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya nchi zetu mbili,” alisema Rais Dk. Samia.
AFYA YA MAMA NA MTOTO
Rais Dk. Samia aliitaka Angola kuimarisha ushirikiano na Tanzania katika sekta ya afya, hususan huduma za mama na mtoto, kwa kutumia uzoefu wa Tanzania katika kupunguza vifo vya wajawazito, watoto wachanga.
Rais Dk. Samia alisema amemweleza kuhusu nafasi yake kama kinara wa masuala ya afya ya mama na mtoto na umuhimu wa Angola kujiunga katika jitihada za kuhakikisha usalama wa mama na mtoto wakati wa kujifungua.
“Nimemweleza Rais Lourenço kuhusu nafasi yangu kama kinara wa masuala ya afya ya mama na mtoto na kumwomba Angola kuungana nasi katika jitihada za kuhakikisha hakuna mama anayefariki wakati wa kujifungua na hakuna mtoto anayefariki wakati wa kuzaliwa,”alisema.
RAIS WA ANGOLA
Kwa upande wake, Rais wa Angola, Lourenço alisema kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi, kutaziwezesha nchi hizo kunufaika fursa zilizopo katika mataifa hayo na kuongeza uwekezaji wa sekta binafsi katika nchi zote mbili.
Alisema mikataba iliyosainiwa itaweka mazingira ya kisheria yatakayowezesha ushirikiano wa taasisi za serikali na uwekezaji wa wafanyabiashara wa Tanzania nchini Angola na wa Angola nchini.
“Tunapozidisha uhusiano wa ushirikiano wa kiuchumi kati ya Angola na Tanzania, nchi zote mbili zitanufaika. Hatuwezi kufikia malengo yetu ya maendeleo ya kiuchumi na ustawi wa wananchi kwa kutegemea uwezo wetu wenyewe pekee, hivyo tunahitaji kuimarisha ushirikiano wetu,” alisisitiza.
Rais Lourenço alisema Angola iko tayari kushirikiana na Tanzania katika matumizi ya teknolojia ya satelaiti ya Angosat-2 kwa ajili ya mawasiliano, teknolojia, huduma za hali ya hewa na shughuli zingine za maendeleo ya kiuchumi.
Aidha, viongozi hao walijadili ushirikiano katika elimu na afya, hususan huduma za afya ya mama na mtoto, ambapo Angola ilileza nia ya kujifunza kutokana na uzoefu wa Tanzania katika kuboresha huduma hizo.
“Katika mazungumzo yetu, tulizungumzia ushirikiano katika sekta ya afya na Rais Samia alieleza uzoefu wa Tanzania katika afya ya uzazi na mtoto
Aliongeza: “Tunavutiwa kujifunza kutokana na uzoefu huo ili kuboresha hali katika nchi yetu na kuchangia maendeleo kwa ujumla.”
MIKATABA ILIYOSAINIWA
Katika hafla hiyo, nchi hizo zilitia saini mikataba na hati nne za makubaliano zinazolenga kuimarisha ushirikiano katika maeneo mbalimbali.
Mkataba wa kwanza ni wa kubadilishana wafungwa ambao unaohusu uhamisho wa wafungwa wanaotumikia vifungo kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Angola.
Mkataba wa pili ni wa huduma za usafiri wa anga, unaolenga kuweka msingi wa kuimarisha mawasiliano ya anga kati ya nchi hizo na kuwezesha safari za moja kwa moja, kurahisisha usafiri wa watu na kuchochea biashara, utalii.
Hati ya tatu ni ya ushirikiano katika sekta ya mawasiliano, iliyosainiwa na wawakilishi wa serikali za nchi hizo mbili kwa lengo la kuimarisha ushirikiano katika eneo hilo.
Hati ya nne ni ya ushirikiano kati ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) na Taasisi ya Taifa ya Hali ya Hewa ya Angola, inayolenga kuimarisha ushirikiano katika masuala ya hali ya hewa.




