NA FRED ALFRED,
DODOMA
VYAMA vya siasa nchini, vimempongeza Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, kukamilisha ujenzi wa miundombinu ya kisasa katika Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma.
Pongezi hizo zilitolewa katika ziara ya viongozi wa vyama hivyo katika Mji wa Serikali Mtumba jana, kuelekea uzinduzi rasmi wa majengo ya ofisi za wizara na taasisi za Serikali na barabara za lami unaofanyika leo.
Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa, Aggrey Mwanri, alisema maendeleo yaliyofikiwa yanaonesha dhamira ya Serikali ya kuifanya Dodoma iendane na hadhi yake kama makao makuu ya nchi.
Mwanri ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara, alisema wamefurahishwa na majengo ya kisasa na mazingira ya kazi waliyoona, akibainisha baadhi ya maeneo yanafanana na hoteli za hadhi ya nyota tano.
“Tumefurahi sana kuona jitihada za serikali kuifanya Dodoma kweli pafanane na makao makuu ya Serikali na nchi kwa ujumla. Kwetu sisi kama vyama vya siasa, tunafurahi kuhusishwa na maendeleo ya sampuli hii,” alisema Mwanri.
Alisema kuhamia shughuli kuu za serikali kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma, hakumaanishi tu kuhamisha ofisi, bali pia kuhamisha heshima na majukumu yanayohusiana na uamuzi mkubwa wa nchi.
Alisema wananchi wa Dodoma wana wajibu wa kulinda hadhi hiyo kuhakikisha majengo, barabara, miti na miundombinu mingine haviharibiwi.
“Uwekezaji huo unapaswa kwenda sambamba na utoaji wa huduma bora kwa wananchi, akiwataka watumishi wa serikali kuhakikisha wanaofika katika ofisi hizo kupata huduma wanatatuliwa changamoto zao kwa wakati.
Alisema serikali inayoongozwa na Rais Dk. Samia inatarajia kuona watumishi wakionesha uwajibikaji, uadilifu na weledi katika kutekeleza majukumu yao.
AAFP
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Chama cha Wakulima (AAFP), Rashid Ray, alisema kukamilika Mji wa Serikali Mtumba, ni hatua muhimu katika utekelezaji wa azma ya kuifanya Dodoma kuwa makao makuu yenye hadhi inayostahili.
Hata hivyo, alitaka watumishi wote wa serikali wanaopaswa kufanya kazi Dodoma kurejea katika makao makuu hayo ili wananchi wapate huduma bila usumbufu.
Alisema kumekuwa na vitendo kwa baadhi ya watumishi kurejea Dar es Salaam, jambo alilodai linaweza kupunguza ufanisi wa uwekezaji uliofanyika, ikiwa ofisi zitakuwa na majengo mazuri lakini watumishi wanaohitajika hawapo.
“Watu wote warudi Dodoma kama ilivyokuwa maelekezo yaliyotolewa, vinginevyo fedha zilizotumika hapa zitakosa maana kama majengo hayatakuwa na watumishi wanaotekeleza majukumu yao,” alisema.
Alisema ni muhimu kuhakikisha watumishi wa wizara na taasisi za Serikali, wanapatikana katika maeneo yao ya kazi ili wananchi wanapofika kupata huduma wasikute viongozi na watendaji muhimu hawapo.
CUF
Naye Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Hamad Rashid Hamad, aliipongeza serikali kwa kazi iliyofanyika, akisema kukamilika majengo hayo kunaonesha ndoto ya kuwa na makao makuu yenye miundombinu ya kisasa imeanza kuwa uhalisia.
Alisema viongozi wa vyama vya siasa wamepata fursa ya kutembelea baadhi ya majengo, yakiwemo ya Wizara ya Kilimo na Wizara ya Maji na kujionea maendeleo yaliyofikiwa.
Hamad alisema vyama vya siasa vinathamini kushirikishwa katika hatua hiyo muhimu ya maendeleo ya taifa, huku akisisitiza umuhimu wa watumishi wa Serikali kuhamia Dodoma na kutekeleza majukumu yao kwa kuwahudumia wananchi.
UDP
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa United Democratic Party (UDP), Swaumu Rashid, alisema kukamilika mradi huo ni matokeo ya amani na utulivu uliopo nchini.
Alisema miundombinu hiyo ni mali ya Watanzania wote na manufaa yake hayataishia kwa chama kimoja cha siasa, bali yatawanufaisha wananchi bila kujali itikadi zao.
“Tumeona matunda ya kodi zetu Watanzania. Hivyo, ni wajibu wetu sote kutunza miundombinu hii ili iweze kuendelea kutumika kwa manufaa ya taifa,” alisema.
Swaumu alitoa wito kwa Watanzania kuendelea kudumisha amani, utulivu na kushirikiana kulinda majengo na miundombinu iliyojengwa kwa fedha za umma.




