ABDUL DUNIA Na NASRA KITANA
ILE sikukuu ya burudani iliyosubiriwa na mashabiki wa Yanga kwa takriban mwaka mmoja imewadia, klabu hiyo ikipania mambo manne makubwa.
Yanga leo inatarajiwa kuadhimisha kilele cha Tamasha la Siku ya Mwananchi (Mwananchi Day) katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam. Mara ya mwisho klabu hiyo kufanya tamasha hilo ilikuwa mwaka jana.
Katika kilele hicho leo, klabu hiyo yenye maskani yake makutano ya mitaa ya Twiga na Jangwani jijini Dar es Salaam, imepanga kufanya mambo mbalimbali kuhakikisha mashabiki wake wanahisi ladha halisi ya sikukuu ya burudani.
Mbali na burudani na matukio mengine, Yanga itacheza mchezo wa kujipima nguvu dhidi ya Bandari ya Kenya saa 11:00 jioni.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga, Ally Kamwe, aliweka wazi klabu hiyo imepania haswa kuhakikisha tamasha hilo linafana.
Kamwe alisema kwanza imepania kuhakikisha mashabiki wanakuwa na shangwe wakati wote wa tamasha, pili wasanii na wapiga vyombo vya muziki wakiwa katika daraja la juu zaidi la ubora wao.
Meneja huyo alisema tatu wamepania kuhakikisha kunakuwa na mpangilio bora zaidi wa matukio katika tamasha huku nne wakitarajiwa burudani ya aina yake kutoka katika kikosi chao kwa dakika zote 90 katika mchezo huo.
“Tunategemea kuwa na tamasha bora sana, tumepania kuweka historia kubwa. Lengo letu ni kujaza viwanja viwili, kwanza Uwanja wa Benjamin Mkapa na baadae Uwanja wa Uhuru. Kila kitu tumepanga kukifanya katika ubora wa juu, tunaimani uwanjani utajaa na mashabiki watakaokuja tunaamini watakuwa na shangwe la hali ya juu,” alisema.
Kamwe alisema katika tamasha hilo, wasanii mbalimbali watatoa burudani wakiongozwa na Zuhura Othmani ‘Zuchu’, Dullah Makabila, Mzee wa Bwax na Meja Kunta.
YANGA VS BANDARI
Akizungumzia mechi ya leo, Kocha wa Yanga, Romain Folz, alisema anaamini utakuwa mchezo mzuru kutokana na maandalizi bora aliyoyafanya.
Folz alisema huo utakuwa wakati mzuri kwake kwani atapata muda wa kukiangalia vyema kikosi chake kwa msimu mpya.
Alisema anajua wazi wana michezo mingine iliyopo mbele lakini hivi sasa wameweka mipango yao katika mchezo dhidi ya Bandari.
“Yanga ni timu kubwa, kuandaa tukio kubwa kama Mwananchi Day ni kuonesha ukubwa wa klabu hii hapa nchini, Yanga inaitangaza Tanzania katika medani za soka kimataifa kupitia tamasha hili, ni wajibu wetu kama timu kurejesha heshima hii uwanjani kwa kuhakikisha tunakwenda kushinda mchezo ujao na kuonesha burudani,” alisema.
Nahodha wa Yanga, Bakari Mwamnyeto aliwaomba mashabiki kujitokeza kwa wingi kushuhudia mbinu bora za kocha Romain Folz na ubora wa nyota wapya.
Alisema wapo tayari kutoa burudani kwa mashabiki ambao watajitokeza Uwanja wa Mkapa, huku akiweka wazi tayari wameingia katika mfumo wa kocha huyo.
“Licha ya kwamba kocha ni mpya ndani ya timu tayari tumeshaelewa mifumo yake lakini wachezaji wapya ambao wamesajiliwa dirisha lililofungwa hivi karibuni na tayari tumetengeneza muunganiko bora,” alisema.
Kocha Mkuu wa Bandari, Ken Odhiambo, alisema anafahamu wanacheza na timu bora iliyo na wachezaji bora lakini wapo tayari kwa mchezo huo.
Alisema wataingia katika mechi hiyo kwa kuwaheshimu Yanga na wamejiandaa kutoa burudani kwa mashabiki.
“Yanga ni timu bora Afrika na ina wachezaji wengi wazuri, huu mchezo tunauchukulia kwa ukubwa na tunatambua tunatazamwa na watu wengi ni wakati mzuri kuonyesha ubora,” alisema.
“Hautakuwa mchezo rahisi, lakini tumejiandaa vizuri na tupo tayari kwa mchezo mashabiki kutoka mataifa mbalimbali watarajie mchezo mzuri.” alisema.
Nahodha Denis Nganga, alisema wamejiandaa vizuri na wanatambua wanakwenda kukutana na wachezaji wazuri, huku akimtaja Clement Mzize na Andy Boyeli ambao amekiri kuwa ni wachezaji wazuri.
“Tumejiandaa vizuri na tupo tayari kwa mchezo tunatarajia kukutana na timu nzuri iliyo na wachezaji wengi bora,” alisema.