Na NJUMAI NGOTA,
Tanga
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimevunja ukimya na kusema nidhamu ndani ya Chama ni nguzo muhimu ya kuimarisha demokrasia.
Amesisitiza kuwa, uteuzi wa wagombea ndani ya CCM, huzingatia vigezo vya uongozi, uaminifu na muda mwafaka, siyo matokeo ya kura za maoni.
Hayo yalielezwa Soni, Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto, mkoani Tanga, jana na Mgombea Mwenza wa Urais wa CCM, Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi.
Alikuwa akiwahutubia mamia ya wananchi waJimbo la Bumbuli katika mkutano wa kampeni kumwombea kura za urais Dk. Samia Suluhu Hassan.
Dk. Nchimbi alisema CCM inaendelea kuimarika kwa kufuata misingi imara ya uongozi na siasa.
“Uongozi ni kupeana kijiti. Unaweza usiteuliwe leo, ukapewa nafasi kubwa zaidi baadaye. Mimi mwenyewe niligombea uspika mwaka 2015, sikuteuliwa, leo hii ni miaka 10 baadaye, nimeteuliwa kuwa Mgombea Mwenza wa Urais kwa tiketi ya CCM.
“Hii ndiyo maana ya nidhamu ndani ya demokrasia,”alisema Dk. Nchimbi.
Alisema kila mwanachama wa CCM, anapaswa kuelewa kuwa, nafasi za uongozi siyo haki ya mtu,bali dhamana, hivyo ni muhimu kila mwanachama akajenga moyo wa kukubali uamuzi kwa heshima na unyenyekevu.
Akizungumzia Uchaguzi Mkuu utakaofanyikaOktoba 29, mwaka huu, Dk. Nchimbi, alisema mfumo wa vyama vingi na uchaguzi huru nchini,unatoa fursa kwa vyama kuwasimamisha wagombea,baadae kumteua mtu kwa kila nafasi.
“CCM ina wanachama zaidi ya milioni 13.4 waliosajiliwa kielektroniki, kila mmoja ana haki ya kugombea.
“Nafasi ni moja kila kata, jimbo au taifa. Tunapofanya uteuzi, siyo kwamba wengine hawafai, inakuwa safari hii ni zamu ya mwingine,” alisema.
“Katika nchi yetu, tuna utaratibu wa demokrasia ya vyama vingi na demokrasia ya uchaguzi, kila baada ya miaka mitano, tunafanya uchaguzi, mwaka huu ni miaka mitano inayokuja lazima tufanye uchaguzi.
“Kwa hiyo, katika ngazi ya umma, kila chama cha siasa, kinapeleka wagombea wakajinadi, wakajieleze na wakaeleze yaliyotokea nyuma wanayotaka kufanya baadaye,” alisema.
WAPONGEZWA KWA UZALISHAJI
Balozi Dk. Nchimbi aliwapongeza wananchi wa Lushoto kwa kuleta maendeleo kupitia kilimo huku zaidi ya asilimia 80 ya wakazi wa eneo hilo, akitegemea kulima.
“Viungo, matunda, mboga, misitu, uvuvi, biashara ndogondogo na madini vinapatikana hapa. Hongereni, mnatupa heshima kubwa,” alisema.
Alisema Lushoto ni sehemu muhimu kwa uzalishaji wa chakula na mazao ya biashara nchini.
Pia, alitumia fursa hiyo kuwapelekea salamu kutoka kwa Mwenyekiti wa Chama, Dk. Samia Suluhu Hassan, ambaye ni Mgombea Urais wa CCM.
“Dk. Samia amenituma niwape salamu za upendo na mshikamano na kuwashukuru kwa ushirikiano mkubwa waliompa katika kipindi chote cha uongozi wake,” alisema.
MAJIMBO YOTE TANGA CCM
Alisema viongozi wa CCM mkoani Tanga akiwemo Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa, Rajabu Abdulrahman na Katibu Mkuu mstaafu wa Chama, Yusuf Makamba kuwa, majimbo yote ya mkoa huo yatachukuliwa na CCM.
“Tumeungana kujenga Chama chetu na nchi yetu. Na matarajio yangu ni kwamba, hapa kwa wakwe zangu, tutapata kura zote za Dk. Samia, mbunge na diwani,” alisema.
MAKAMBA ANENA
Balozi Dk. Nchimbi alimpigia simu Katibu Mkuu mstaafu, Makamba akiwa jukwaani na kuwaombawananchi wa Jimbo la Bumbuli mkoani Tanga, kumchagua Dk. Samia, mgombea ubunge wa jimbo hilo, Mhandisi Ramadhani Singano na madiwani wote wa Chama.
Makamba alisema anaimani na wagombea wote wa CCM na alipenda kuhudhuria mkutano huo, kutokana na changamoto ya afya hakuhudhuria na kuwataka wakazi wa wa Mkoa wa Tanga, wasimwangushe katika uchaguzi huo.
MOMBO
Akiwa katika mkutano wa kampeni Mombo, Korogwe Vijijini, Dk. Nchimbi, aliwasisitiza wananchi wa maeneo hayo hawana deni kwa Dk. Samia bali anawadai kutokana na maendeleo makubwa aliyowafikishia.
“Rais wetu amegusa kila eneo elimu, afya, kilimo, uvuvi, umeme, biashara na miundombinu.
“Hili halihitaji mjadala, ni kazi kubwa inayozungumza yenyewe,” alisema.
Kwa mujibu wa Dk. Nchimbi, kasi ya utekelezaji wa Ilani ya CCM itaongezwa mara dufu endapo Chama kitaendelea kuaminiwa kuongoza dola.
Alisema katika kipindi kijacho iwapo watapewa ridhaa ya kuongoza nchini, watatekeleza miradi ya maendeleo kwa wananchi wa Korogwe Vijijini ikiwemo uboreshaji wa hospitali ya wilaya kufikia hadhi ya wilaya kwa majengo, vifaa, madaktari na wauguzi.
MNZAVA
Mgombea Ubunge wa Jimbo la Korogwe Vijijini kupitia CCM, Timotheo Mnzava, alisema serikali ya CCM imefanya kazi kubwa na hivi sasa ni muda wa kurudisha heshima kwa kupiga kura kwa wingi.
“Watu wa Korogwe Vijijini na Mombo tumejipanga. Hatuna deni, serikali ya CCM imefanya kazi katikaelimu, afya, umeme, barabara. Tumejiandaa kutoa kura za heshima kwa Rais Samia, mbunge na diwani,” alisema.
AWESO
Mgombea Ubunge wa Jimbo la Pangani na Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, aliwahakikishia wananchi kuwa, serikali imepeleka sh. bilioni 900 kwa mradi wa maji, ambao utekelezaji wake ulichelewa na hivi sasa utakamilika.
“Baada ya dhiki huja faraja. Faraja ni CCM, Samia, Nchimbi na serikali yetu. Nawahakikishia kazi hii itakamilika haraka,” alisema.