Na MWANDISHI WETIU
MKUU wa Mkoa wa Arusha, CPA Amos Makalla, amefanya kikao cha pamoja na wadau wa Utalii Arusha leo Alhamisi Septemba 25, 2025, lengo la kupokea changamoto zinazowakabili wadau na sekta ya utalii huku akisisitiza kuandaliwa kwa Mkakati wa miaka mitano wa ukuzaji utalii katika Mkoa wa Arusha.
Katika kikao hicho, CPA. Makalla amesema kuwa mkakati huo utaunganisha sekta mtambuka zinazohusiana na utalii, ikiwemo sekta ya michezo, mkakati ambao uhusika na maandalizi ya mapokezi ya wageni na watalii wakati wa michuano ya Mpira wa miguu kwa Mataifa ya Afrika AFCON 2027.
“Mpango kazi huo utahusisha kuwepo kituo cha utalii kitakachokuwa na nyaraka za utalii, tafiti za wanyamapori na na maonesho ya tamaduni za kitanzania hivyo timu nitakayoiunda itahusisha wataalamu kutoka Serikalini na wadau wa utalii ili sote tuzungumze lugha moja kwenye safari ya kukuza utalii Mkoa wa Arusha.” Amesema.
Aidha amesisitiza suala la uhifadhi endelevu Mkoani Arusha, usafi pamoja na utunzaji wa mazingira akieleza kuwa uhifadhi na utalii ni masuala yanayotegemeana na bila ya uhifadhi hakuna utalii utakaofanyika nchini.
Naye Katibu Mtendaji wa Baraza la Michezo Tanzania BMT, Neema Msitha, amebainisha kufurahishwa na mpango huo wa Mkoa akieleza utayari wa Wizara ya Michezo na Baraza kushirikiana katika maandalizi ya mpango huo utakaoeleza pia fursa za michuano ya AFCON na namna ya kuunganisha na sekta ya Utalii.
Baraza la michezo Taifa BMT na Bw. Eliufoo Nyambi, Mkurugenzi msaidizi wa maendeleo ya michezo kutoka Wizara ya habari, utamaduni, sanaa na michezo wameeleza kufurahishwa na mpango huo wa Mhe. Makalla na kueleza utayari wao katika kushirikiana na Mkoa kwenye uandaaji wa mpango huo pamoja na kuzieleza fursa zitakazotokana na michuano hiyo ya AFCON na namna ya kuiunganisha na sekta ya Utalii Mkoani Arusha.
