Na AMINA KASHEBA
KOCHA timu ya taifa ‘Taifa Stars’, Hemedi Sulemain ‘Morocco’, amesema sababu ya kushindwa kupata ushindi katika mchezo wa kufuzu Kombe la Dunia 2026 dhidi ya Zambia ni wachezaji wake kukosa umakini wa kutumia nafasi.
Juzi, Stars ilifungwa bao 1-0 dhidi ya Zambia katika mchezo wa mwisho wa kuwania kufuzu Kombe la Dunia, uliofanyika dimba la New Amaan Complex, Zanzibar.
Akizungumza baada ya kumalizika kwa mchezo huo, kocha huyo alisema wachezaji wake kutokuwa makini katika umaliziaji ndiyo sababu ya kushindwa kupata ushindi.
” Bado umakini wa eneo la umalizaji kupata mabao limekuwa tatizo katika kikosi.
“Tunalijua suala la kutokufunga ila baada ya muda mfupi litakaa vizuri, tutalifanyia utatuzi, kwa sababu kupata mchezaji wa kufunga kama Mbwana Samatta ni ngumu lakini tuna imani tutapata,” alisema.
Kocha huyo alisema hivi sasa wachezaji waliopo katika kikosi wanapaswa kupata mechi mbalimbali kwa lengo la kupata uzoefu hadi ikifika michuano ya AFCON 2025, ana imani kikosi kitakuwa vizuri katika eneo la kufunga.
“Ni suala la muda, kwa wachezaji waliopo katika kikosi wakipata mechi mbalimbali za kucheza nina imani watakaa sawa hadi ikifika AFCON tutakuwa vizuri katika kupata mchezaji ambaye atakuwa mzuri katika eneo la umaliziaji,” alisema.
Katika kundi E, kuwania kufuzu Kombe la Dunia, Taifa Stars imemaliza nafasi ya tatu kwa alama 10, kinara Morocco ina pointi 21, Niger inafuatia kwa alama 12, Zambia ina pointi tisa wakati Congo Brazaville ikiwa na pointi moja.