Na MUSSA YUSUPH,
Shinyanga
IDADI ya wananchi waliofurika katika mikutano ya kampeni za Mgombea Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Shinyanga, imeweka rekodi ya kipekee.
Katika mikutano hiyo iliyofanyika jana Uwanja wa Kambarage Shinyanga Mjini na Uwanja wa Magufuli uliopo wilayani Kahama, idadi kubwa zaidi ya wananchi ilishuhudiwa huku wengine wakishindwa kuingia ndani ya viwanja hivyo kwa sababu ya wingi wa watu.
Hali hiyo haikuwakatisha tamaa wananchi hao walionesha mapenzi yao ya dhati kwa mgombea urais kupitia CCM, hivyo walishuhudia mikutano hiyo katika migahawa, maduka na vibanda vya runinga.
Makundi ya wananchi yalianza kumiminika katika viwanja hivyo kuanzia saa 2 asubuhi wakiwa na matamanio ya kumshuhudia kiongozi wao mpendwa.
Akizungumza na wananchi waliofurika katika mkutano wake wa kampeni uliofanyika Uwanja wa Kambarage, Dk. Samia alisema miaka mitano ijayo atafanya makubwa zaidi yenye kugusa maisha ya Watanzania.
Alisema lengo la dhamira hiyo ni kuimarisha na kuuhifadhi utu wa Mtanzania unawiri na kuheshimika.
Dk. Samia alisema serikali yake pindi itakapopewa ridhaa ya kuongoza taifa, itafanya mambo makubwa zaidi katika sekta za elimu, afya, kilimo, maji na miundombinu.
Katika mkutano huo, Dk. Samia aliwapa nafasi Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, Waziri wa Maji, Jumaa Aweso na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi na Ajira, Patrobas Katambi, kuelezea kwa kina mafanikio yaliyopatikana katika sekta hizo.
Akizungumzia mafanikio yaliyopatikana katika sekta ya kilimo, mgombea ubunge Jimbo la Nzega Mjini, Bashe alisema hali ya uchumi katika mkoa huo inabebwa kwa shughuli za madini na kilimo.
Alisema Dk. Samia alipoingia madarakani alizungumzia namna anavyokerwa na umaskini wa wakulima na wafugaji wanaoishi maeneo ya vijijini.
Alieleza mkoa huo ni wakulima wazuri wa pamba, mpunga, dengu, choroko na mbaazi, mazao ambayo yalikuwa hayana thamani.
Hata hivyo, alisema mwaka huu mauzo ya choroko ni zaidi ya sh. bilioni sita huku dengu ikifikia zaidi ya sh. bilioni 26 fedha ambazo zimeingia mifukoni mwa wakulima.
Akizungumzia pamba, alisema mwaka huu wakulima wa zao hilo mkoani humo wamepewa sh. bilioni 20 za ruzuku za pembejeo.
Alisema hatua hiyo imewezesha uzalishaji kuongezeka kutoka tani 10,000 hadi tani 34,000 zilizozalishwa mwaka huu.
Alisema Dk. Samia alipoingia madarakani alikuta mradi ujenzi wa soko la kimataifa la mazao haujatekelezwa, lakini sasa mradi huo mkandarasi ameanza kujenga wilayani Kahama.
Alieleza hatua hiyo itawezesha wanunuzi wa mpunga kutoka nje ya nchi kununua katika soko hilo badala ya kwenda shambani kulangua wakulima.
Bashe alisema wakati bei ya mahindi ilipoporomoka, Dk. Samia aliiagiza Wakala wa Hifadhi ya Taifa ya Chakula (NFRA) kununua mazao ya wakulima sh. 700 kwa kilo badala ya sh. 200.
Aliahidi serikali inakwenda kufufua Chama Kikuu cha Ushirika Mkoa wa Shinyanga (SHIRECU), ambapo tayari tathmini ya madeni imefanyika, hivyo zaidi ya sh. bilioni sita zitalipwa.
Pia, alisema Dk. Samia ametoa fedha kufufua kiwanda cha kuchakata pamba cha ushirika huo ambapo kuanzia mwakani kitaanza kununua pamba.
MAPINDUZI HUDUMA ZA MAJI
Awali, mgombea ubunge wa Jimbo la Pangani mkoani Tanga, Jumaa Aweso, alisema kabla ya Dk. Samia kuingia madarakani hali ya upatikanaji maji ilikuwa chini ya asilimia 60.
Alisema baada ya uwekezaji wa zaidi ya sh. bilioni 100, hali ya upatikanaji maji imekuwa zaidi ya asilimia 80 huku maeneo ya vijijini kufikia zaidi ya asilimia 70.
AJIRA MILIONI NANE
Kwa upande wake, mgombea ubunge Jimbo la Shinyanga Mjini, Patrobas Katambi, alisema Dk. Samia amefikia lengo la ilani kwa kutoa ajira zaidi ya milioni nane kupitia miradi mikubwa ya kimkakati.
Alieleza kupitia mfuko wa uwezeshaji wananchi kiuchumi Dk. Samia ametoa zaidi ya sh. trilioni nne zilizowawezesha wananchi zaidi ya milioni 24.
Kuhusu pensheni alisema Dk. Samia ameimarisha mifuko ya pensheni kwa watumishi wa umma na sekta binafsi.
Vilevile, alisema Dk. Samia alitoa fedha ujenzi wa hospitali ya kisasa mkoani hapa hatua ambayo imewezesha wananchi kupata huduma zote badala ya kwenda Dar es Salaam.
Pia, alisema katika sekta ya afya maeneo ya vijijini vimejengwa vituo vya afya suala ambalo halikutegemewa.
Kwa upande wa miundombinu, alieleza kuwa Dk. Samia alitoa zaidi ya sh. bilioni 40 kujenga uwanja wa ndege wa kisasa mkoani Shinyanga.
“Barabara ya kwenda hospitali ya rufaa sasa inajengwa, umetuletea stendi ya kisasa zaidi ya sh. bilioni 20. Kwenye sekta ya elimu leo tuna vyuo vikubwa viwili vya serikali na kimoja binafsi.
“Umetujengea madarasa kwa zaidi ya sh. bilioni sita, umetuletea mradi wa sh. bilioni 195 kusaidia kuongeza mtandao wa upatikanaji maji,” alisisitiza.
Katika umeme, alisema nishati hiyo inapatikana jimboni humo katika vijiji 14 huku mitaa yote ikiwa imefikiwa na huduma.
Mwenyekiti wa Mamalishe na Babalishe Tanzania, Havijawa Omari, alieleza kundi hilo limenufaika kupitia upatikanaji mikopo.
Alisema wengi walikuwa wakikimbia nyumba zao kwa sababu ya mikopo umiza, lakini hivi sasa wananufaika kupitia mikopo ya halmashauri.
Vilevile, alisema kundi hilo limenufaika kwa kupata majiko ya gesi ambayo yamewawezesha kuondokana na changamoto za kiafya zilizokuwa zikiwakabili.
“Sisi mamalishe na babalishe kutoka kwetu ndiyo riziki yetu. Oktoba 29 tunakwenda kutiki kisha tunarudi katika biashara zetu, hakuna maandamano,” alisisitiza.
Mbunge mstaafu wa Shinyanga Mjini, Stephen Masele, alisema katika kipindi cha uongozi wa Dk. Samia amefungua milango kwa wanawake ambao wamekuwa na uwezo wa kushika nafasi yoyote ya uongozi nchini.
Masele ambaye aliwahi kuwa Spika wa Bunge la Afrika, alisema Dk. Samia ni kiongozi mchapakazi, mnyenyekevu, mtulivu na mwenye hofu ya Mwenyezi Mungu.
Alieleza kiongozi huyo ameyagusa makundi mengi kwa kuyapa kipaumbele katika serikali yake.
WAGOMBEA UBUNGE
Mgombea ubunge Jimbo la Solwa, Ahmed Salum, alieleza katika kipindi cha miaka mitano jimbo hilo limepata sh. bilioni 26.6 za miradi ya maendeleo.
Alisema fedha hizo zimetumika kugharimia miradi ya maji katika vijiji 56 kati ya vijiji 68.
Vilevile, alisema vijiji sita vinaendelea kufikishiwa huduma hiyo kutoka Ziwa Victoria.
Kuhusu elimu, alisema fedha hizo zimetumika kununua madawati 2,160, ujenzi wa shule mpya mbili za msingi, nyumba tano za walimu na matundu ya choo zaidi ya 100.
Alisema hospitali mpya ya wilaya imejengwa kwa gharama ya sh. bilioni nane na kujenga jengo la utawala la halmashauri kwa zaidi ya sh. bilioni tatu.
Akizungumzia nishati ya umeme, alisema hakuna kijiji ambacho hakijafikishiwa nishati hiyo huku vitongoji zaidi ya 200 vikipatiwa umeme.
Mgombea ubunge viti maalumu, Christina Mzava, alisema katika sekta ya afya mkoa huo ulikuwa na hospitali mbili za wilaya, lakini ndani ya miaka minne zimefikia hospitali nane.
Pia, alisema mkoa huo umefikisha idadi ya vituo vya afya 46 kutoka vituo 25 vilivyokuwa awali huku idadi ya madaktari bingwa wa kina mama na watoto ikiongezeka.
Alisema uwezeshaji wananchi kiuchumi vikundi 1,421 vimenufaika baada ya kupatiwa zaidi ya sh. bilioni nane kwa vijana, wanawake na wenyeulemavu.
WANANCHI WAFUNGUKA
Mkazi wa Kahama, Josephina Mashimba, alisema amefika katika mkutano huo kumshuhudia Dk. Samia kwani amewawezesha wanawake kupata fursa ya mikopo kupitia halmashauri.
“Mikopo ya halmashauri imetufanya tuimarike zaidi kibiashara, kwani tunaipata bila masharti magumu. Nina mgahawa ambao unaniingizia faida kati ya sh. 70,000 hadi 100,000 jambo ambalo awali ilikuwa ndoto kwangu.
“Nimeajiri wasichana wanne na wavulana watatu. Hao wote wanaendesha maisha yao kupitia mgahawa wangu. Sina cha kumlipa Rais wangu ndiyo maana nikaona cha pekee ni kuja hapa uwanjani kumsikiliza na Oktoba 29 nitampigia kura,” aliongeza Josephina.