• ePaper
Wednesday, October 15, 2025
Subscribe
No Result
View All Result
Uhuru Publication
  • Habari
  • Michezo
  • Uchaguzi
  • Burudani
  • Toleo Maalumu
  • Kolamu
  • Makala
  • Hadithi
  • Habari
  • Michezo
  • Uchaguzi
  • Burudani
  • Toleo Maalumu
  • Kolamu
  • Makala
  • Hadithi
No Result
View All Result
ePaper
Uhuru Publication
No Result
View All Result
Home Habari

DK. SAMIA AWAPA FARAJA WENYE MAHITAJI MAALUMU

Abdurahman Jumanne by Abdurahman Jumanne
October 13, 2025
in Habari, Kitaifa, Siasa, Uchaguzi
0
DK. SAMIA AWAPA FARAJA WENYE MAHITAJI MAALUMU

MGOMBEA Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Samia Suluhu Hassan

0
SHARES
1
VIEWS
Share on FacebookShare on Twitter

Na MUSSA YUSUPH,

Geita

MGOMBEA Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Samia Suluhu Hassan, amesema serikali yake, itahakikisha inaimarisha zaidi ustawi wa makundi na watu wenye mahitaji maalumu.

Amesema makundi hayo wakiwemo wenye ulemavu, serikali yake baada ya kupewa ridhaa ya kuliongoza taifa, itahakikisha wananufaika kupitia ajira, afya, elimu na uwezeshaji kiuchumi kupitia mikopo.

Dk. Samia, alitoa hakikisho hilo, alipohutubia umati wa wananchi katika mkutano wake wa kampeni uliofanyika uwanja wa EPZA uliopo wilayani Geita mkoani hapa.

“Ndugu zetu wenye changamoto za ulemavu wa viungo, ulemavu wa ngozi, ulemavu wa kusikia, kwenye ilani hii (2025- 2030), tunakwenda kuendelea kuwapatia huduma zao kwenye maeneo ya elimu, afya zao, mikopo, ajira na michezo.

Alisisitiza: “Lakini, hata uwezo wao kuingia katika majengo mbalimbali ya serikali. Majengo yote tunayajenga kiasi ambacho, wenye ulemavu waweze kufika kuhudumiwa.”

Dk. Samia, alisema katika kipindi cha miaka mitano, jitihada za serikali zilielekezwa katika huduma za jamii, ujenzi wa miundombinu na mipango ya uwezeshaji wananchi kiuchumi.

Alibainisha kuwa, hatua hiyo, ina lengo la kuwafanya wananchi washiriki kikamilifu shughuli za uzalishaji katika sekta mbalimbali.

Dk. Samia alisema matokeo ya jitihada hizo za pamoja baina ya serikali na wananchi, zinaonekana wazi kwani Mkoa wa Geita kuna ustawi mkubwa wa kiuchumi.

“Geita ninayoijua mimi ya miaka 10 nyuma, siyo ile ninayoiona leo. Kwa kweli maendeleo ni makubwa,” alisema huku akishangiliwa na umati wa wananchi.

Dk. Samia, alisema ilani ya Uchaguzi (2025 – 2030), imeelekeza masuala mbalimbali, ikiwemo sekta za uzalishaji zenye kuleta mageuzi ya kiuchumi.

Alisema katika kilimo, lengo la serikali ifikapo 2030, ukuaji wake ufikie asilimia 10.

Pia, alieleza ilani imeelekeza katika ufugaji, serikali itaendelea kutoa chanjo kwa mifugo, ujenzi wa majosho na machinjio  maeneo mbalimbali.

Suala lingine ambalo alilitaja kwamba ilani imeelekeza ni ujenzi wa uchumi wa viwanda, kuimarisha biashara na fursa za ajira kwa vijana.

Alisisitiza kuwa, serikali itajenga viwanda vya kuchakata alizeti maeneo ya Nyaluanzaga, Bukoli na Busanda huku viwanda vya kusindika matunda vitajengwa eneo la Igate mkoani Geita.

“Kitaifa tunataka kuikuza sekta ya viwanda kutoka ukuaji wa asilimia nne ya sasa mpaka asilimia tisa mwaka 2030,” alisisitiza.

Kwa upande wa madini, alieleza kuwa serikali itajenga maabara ya kisasa mkoani hapo ambayo itarahisisha kazi za wachimbaji badala ya kufuata huduma hiyo maeneo ya mbali.

MITAJI KWA WACHIMBAJI WADOGO

Vilevile, alisema serikali inajiandaa kutoa mitaji kwa wachimbaji wadogo kuwakuza wawe wachimbaji wakubwa kisha kupima maeneo mapya ya uchimbaji.

“Tunakwenda kupima zaidi maeneo ya nchi yetu kujua madini yapo wapi ili uchimbaji ukue zaidi hasa kwa wachimbaji wadogo.

“Uwanja wa maonyesho wa madini tunakwenda kuujenga kuwa uwanja wa kimataifa, kuwa uwanja wa mikutano wa sekta ya madini na uwanja wa maonyesho,” alisisitiza.

Katika sekta ya usafiri na usafirishaji, alisema ilani imeagiza uendelezaji ujenzi wa barabara ambapo kifungu cha 41 A kifungu kidogo G katika ilani ya mkoa huo kimeeleza barabara zitakazojengwa.

Pia, alisema ilani imeagiza kujenga viwanja vya ndege ambapo katika mkoa huo kitajengwa kiwanja cha ndege Geita na kukiendeleza kiwanja cha ndege Chato.

Akizungumzia usafiri majini, alisema maeneo yote yenye kuhitaji vivuko serikali itajenga miundombinu ya vivuko kuwezesha usafirishaji wananchi.

Kuhusu nishati, alisema serikali itajenga kituo cha kupoza umeme ambacho kitahakikisha umeme ndani ya mkoa huo unapatikana muda wote.

Alisema nishati hiyo itawezesha wananchi kufanya shughuli zao viwandani na katika makazi yao.

“Tutamalizia ile nngwe yetu ya umeme kwenye vijiji vilivyobakia na vitongoji lakini pia umeme kwenye visiwa,” alibainisha.

Dk. Samia, alisema serikali itaendeleza mbuga ya Burigi Chato na visiwa vya Rubondo pamoja na kudhibiti wanyamapori waharibifu.

“Tutapima ardhi na kumilikisha wananchi. Kwenye ilani yetu mpya imesema tunakwenda kupima maeneo yetu ikiwemo ardhi ya wafugaji kutoka ekari milioni 3.4 za sasa hadi ekari milioni sita zitakazomilikishwa kwa wafugaji.

Aliongeza: “Tunakwenda kupima maeneo ya miji, makazi na maeneo ya uwekezaji.”

Alisema eneo lingine ambalo ilani ya CCM imeagiza ni kuboresha ustawi wa wananchi katika afya.

Alisema serikali itajenga tawi la Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), hivyo matibabu ya moyo yatafanyika katika mkoa huo.

Alieleza kuwa, nchi na mikoa jirani na Geita nayo wagonjwa watapatiwa matibabu katika tawi hilo la JKCI.

Dk. Samia, alibainisha kuwa, serikali itaendelea na ujenzi wa zahanati, vituo vya afya na hospitali za halmashauri.

“Kwa hapa mjini tutaendelea kuboresha hospitali yetu ya wilaya na tutajenga jengo la kuhifadhia maiti,” alisisitiza.

Katika sekta ya elimu, alieleza kuwa serikali yake imejenga shule za sekondari, msingi na vyuo vya ufundi ili vijana waweze kujiajiri au kuajiriwa.

Awali, Katibu Mkuu wa CCM, Dk. Asha- Rose Migiro, alisema wananchi wana matumaini makubwa na Dk. Samia, kwani Mkoa wa Geita, umepiga hatua kubwa za maendeleo.

Alisema Dk. Samia ni kiongozi hodari, jemedari na mwenye maono, kwani uongozi wake ni wenye kuleta matokeo.

NAIBU WAZIRI MKUU

Kwa upande wake, Mgombea Ubunge Jimbo la Bukombe, Dk. Doto Biteko, alieleza kuwa, Dk. Samia amewezesha mkoa huo kuimarika zaidi kiuchumi.

Alisema katika sekta ya nishati, Dk. Samia alitoa maagizo kutatua changamoto ya mgawo wa umeme, hatua ambayo imelifanya taifa kuondokana na changamoto hiyo.

Biteko ambaye pia ni Niabu Waziri Mkuu, alisema mkoa huo kwa sasa, unapata umeme kutoka Mwanza na Bulyankulu, huku mradi wa uzalishaji umeme kutoka Bwawa la Rusumo ukikaribia kukamilika.

Pia, alisema vijiji vyote vya mkoa huo, vimefikishiwa nishati hiyo, huku nguvu ikielekezwa vijiji vitatu vilivyopo maeneo ya kisiwani.

MIRADI MINNE YA UMWAGILIAJI

Mgombea Ubunge Jimbo la Nzega Mjini na Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, alisema baada ya Dk. Samia kuingia madarakani, serikali inatekeleza miradi minne ya umwagiliaji kwa gharama zaidi ya sh. bilioni 30.

Alisema matumizi ya mbolea yalikuwa chini, hata hivyo baada ya Dk. Samia kuingia madarakani ametoa sh. bilioni 2.8 za mbolea ya ruzuku kwa wakulima mkoani humo.

UPATIKANAJI MAJI WAONGEZEKA

Naye, Mgombea Ubunge Jimbo la Pangani, Jumaa Aweso, alisema hali ya upatikanaji maji katika mkoa huo miaka minne iliyopita, ilikuwa chini ya asilimia 40.

Aweso ambaye ni Waziri wa Maji, alisema baada ya Dk. Samia kutoa sh. bilioni 200 kuboresha hali ya upatiakanaji maji mkoani humo, asilimia 70 ya wananchi, wanapata huduma hiyo.

Vilevile, alisema mradi wa kutoa maji Ziwa Victoria kwenda katika mji huo, utaongeza upatikanaji maji kufikia asilimia 100, kwani mahitaji ya mji huo ni lita za ujazo milioni 22, wakati kiasi kitakachozalishwa kwa siku ni lita za ujazo milioni 40.

MGOGORO WANANCHI NA GGM WATATULIWA

Mgombea Ubunge Jimbo la Mtumba, Antony Mavunde, alisema Dk. Samia, alitoa maelekezo kuhusu utatuzi wa mgogoro baina ya wananchi na mgodi wa Geita Gold Mine katika eneo la leseni MSL namba 99/95.

Alisema katika mgogoro huo serikali imepunguza leseni ya mgodi kisha kurejesha kwa wananchi baadhi ya eneo ambapo Manispaa ya Geita imeanza mchakato kupima viwanja.

Mavunde, ambaye pia ni Waziri wa Madini, alisema mchakato wa tathmini kwa wananchi waliopisha maeneo ya mgodi huo imefikia asilimia 92 na baada ya kukamilika, watalipwa fidia.

Alisema kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BoT) sh. trilioni 3.2 zimetumika kununua dhahabu ya wachimbaji wa mkoa huo jambo ambalo limechechemua ukuaji uchumi kwa wananchi.

AHADI YA WACHIMBAJI WADOGO

Rais wa wachimbaji madini nchini, John Bina, alisema wachimbaji wadogo wa madini wametoa ahadi kwenda kumchagua Dk. Samia kwa kishindo ifikapo Oktoba 29 mwaka huu.

Alisema zamani wachimbaji madini, walionekana kama watu waliopotea, lakini kwa sasa, baada ya kufunguliwa fursa, wanaheshimika katika jamii.

Aliongeza kuwa, kwa sasa BoT, wananunua dhahabu moja kwa moja, hatua ambayo imeongeza soko la uhakika kwa wachimbaji wadogo.

Pia, alisema wachimbaji chumvi wametoa salamu za pongezi kwa Dk. Samia kufuatia hatua ya kuwaondolea kodi zaidi ya 20 ambazo zilikuwa kikwazo.

Hata hivyo, aliwasilisha maombi kutoka kwa wachimbaji hao kuanzishwa kwa soko kubwa la madini Afrika.

WAGOMBEA UBUNGE

Kwa upande wake, Mgombea Ubunge Jimbo la Geita Mjini, Mhandisi Chacha Mwita, alisema Dk. Samia amefanya makubwa katika jimbo hilo hususan changamoto ya maji ambapo kupitia mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria umefikia asilimia 73 hatua ambayo itamaliza shida hiyo.

Alieleza kuwa kwa kipindi cha miaka 26 kulikuwa na changamoto kwa baadhi ya wananchi waliopisha mgodi wa dhahabu Geita.

Hata hivyo, alisema baada ya maelekezo ya Dk. Samia mgogoro huo umeanza kutatulkwa kwa wananchi kufanyiwa tathimini kulipwa fidia zao.

Vilevile, alisema hatua ya Dk. Samia kupandisha hadhi mji huo kuwa manispaa, suala la miundombinu litakwenda kukamilika.

Mgombea Ubunge Jimbo la Nyang’wale, Hussein Nassor, aliyataja mafanikio yaliyopatikana katika jimbo hilo hususan sekta ya elimu.

Alisema jimbo hilo lilikuwa na shule za sekondari 12 ambapo sasa zimefikia shule 22 huku shule za msingi zikifikia 77 kutoka shule 20 kabla ya miaka minne.

Mgombea Ubunge Jimbo la Busanda, Dk. Jaffar Seif, alisema katika jimbo hilo kuna barabara yenye kilometa 133 kutoka Kahama kwenda Kakola ambayo ujenzi wake unaendelea kwa kiwango cha lami.

Alisema kipande kingine kilichosalia cha barabara hiyo kimeshatengewa zaidi ya sh. bilioni 100 kukamilisha mradi huo.

Pia, alisema wakulima wa alizeti wamepatiwa viwanda viwili ambavyo vitasaidia kuongeza thamani ya zao hilo.

Alieleza kuwa maeneo 11 yametengwa kwa ajili ya wachimbaji wadogo ambayo yatawawezesha wachimbaji.

Previous Post

WITO WA DK. NCHIMBI KWA VIONGOZI WA DINI

Next Post

DK. NCHIMBI ATAJA KIPAUMBELE CCM

Next Post
DK. NCHIMBI ATAJA KIPAUMBELE CCM

DK. NCHIMBI ATAJA KIPAUMBELE CCM

Leave a Reply Cancel reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Recommended

CCM YAAHIDI UJEZI WA VITUO VITANO VYA AFYA, ZAHANATI20 WILAYA YA KWIMBA

CCM YAAHIDI UJEZI WA VITUO VITANO VYA AFYA, ZAHANATI20 WILAYA YA KWIMBA

2 months ago
SIMBA NI MWENDO WA MABAO LIGI KUU

SIMBA NI MWENDO WA MABAO LIGI KUU

16 hours ago

Popular News

  • SIMBA NI MWENDO WA MABAO LIGI KUU

    SIMBA NI MWENDO WA MABAO LIGI KUU

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • JESCA: DK. SAMIA NI KIONGOZI JASIRI

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • MAFANIKIO YA WATANZANIA YAKO KATIKA MATENDO – DK. MIGIRO

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • DK. SAMIA AAHIDI UCHUMI JUMUISHI

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • DK. MWINYI AAHIDI KUJENGA HOSPITALI MAALUMU YA SARATANI

    0 shares
    Share 0 Tweet 0

Stay Update, Subscribe Now!

Check your inbox or spam folder to confirm your subscription.

Ukurasa Rasmi wa Televisheni ya Gazeti la Uhuru.

Facebook-f Instagram X-twitter Youtube tiktok
Quick Links
  • Habari
  • Michezo
  • Uchaguzi
  • Burudani
  • Toleo Maalum
  • Kolamu
  • Makala
Services
  • ePaper
Contact Information
  • Dar es Salaam,Tanzania
  • info@upl.co.tz
  • +255 783 925 742
Uhuru Publications , 2025 © All Rights Reserved
  • Terms & Conditions
  • Privacy Policy
  • FAQ
error: Content is protected !!
No Result
View All Result
  • Home
  • Habari
  • Michezo
  • Uchaguzi
  • Burudani
  • Toleo Maalumu
  • Kolamu
  • Makala
  • Contact
  • Hadithi

© 2025 JNews - Premium WordPress news & magazine theme by Jegtheme.