Na MUSSA YUSUPH,
Geita
MGOMBEA Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Samia Suluhu Hassan, amewahakikishia wananchi kuleta maendeleo na kujenga uchumi jumuishi.
Akizungumza katika mkutano wake wa kampeni uliofanyika viwanja vya Shule ya Msingi Bukombe, Dk. Samia, aliwahakikishia wananchi kwamba, atawatumikia kuleta maendeleo na kujenga taifa jumuishi.
Alisema wachimbaji wa wilaya hiyo, walikuwa wakivamia Pori la Akiba Kigosi Moyowosi, kuchimba madini ya dhahabu kwa njia isiyo rasmi.
Alieleza kuwa, rasilimali hiyo ambayo Mungu ameishusha nchini, iwanufaishe vijana na serikali, imeamua kuwamilikisha baadhi ya maeneo kuliko vijana kuendelea kuiba.
“Kuliko wapigwe na askari wa uhifadhi, wapelekwe mahakamani, nikasema hapana. Nikamtaka Dk. Doto Biteko (Naibu Waziri Mkuu) na wenzake serikalini, waangalie namna watakavyoweza kufanya rasilimali hiyo iwafae vijana wa Bukombe.
Aliongeza: “Leo wanachimba, wanauza, tumewajengea masoko na maisha yanakwenda vizuri sana.
“Huku ndiko kujenga utu wa Mtanzania, ndiko kujenga utu wa vijana wetu. Ndiko kuwawezesha waendelee na maisha yao yawe mazuri, wapate heshima ya kutosha.”
Kwa upande wa kilimo, Dk. Samia, alisema wapo wakulima ambao kwa muda mrefu, walikuwa wakitaka kuvuna kwa kiasi kikubwa, wapate fedha za kutosha kuendesha maisha yao
Alibainisha hatua zilizochukuliwa na serikali kuwapatia ruzuku ya mbolea, dawa za kilimo kisha kuwajengea skimu za umwagiliaji walime na kuzalisha mazao kwa wingi.