Na MUSSA YUSUPH
MGOMBEA Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Samia Suluhu Hassan, ametoa wito kwa vijana nchini, wasikubali kudanganyika ili kuchafua amani ya nchi.
Dk. Samia, amesisitiza kuwa, Tanzania ni eneo sahihi kwa vijana kuishi tofauti na maeneo mengine Afrika.
Aliyasema hayo katika mkutano wa kampeni za Uchaguzi Mkuu, uliofanyika eneo la Buza, wilayani Temeke jijini Dar es Salaam.
“Nataka kuwahakikishia vijana wa Tanzania, hawa wazee wenzangu wanaelewa.
“Vijana wa Kitanzania msidanganywe, ukichukua Afrika Mashariki, Kusini na Kati, Tanzania ni pepo.
“Hapa mpo katika nchi yenye jina, yenye sifa zake, yenye kuendeleza watu wake.
“Msidanganywe wale ambao wapo nje wasiwadanganye. Hapa mpo pazuri kweli kweli,” alisisitiza.
Alisema: “Mkipata fursa kuingia kwa majirani zetu, mtaona vijana wenzenu wanavyokula ngumu. Mtasema mnataka kurudi kwenu.”
Alibainisha vijana wanategemewa kukabidhiwa nchi kuiendesha kama inavyoendeshwa bila kudanganywa.
Pia, alisema katika kuongoza nchi, taifa limeweka mifumo mizuri ya kidemokrasia kwa kuchaguana kila baada ya miaka mitano.
“Tulizeni munkali, nchi hii ni mali yenu, hakuna mwenye cheti anayesema nchi hii ni mali yangu. Sisi tunawakilisha wananchi, wananchi ndiyo nyinyi.
“Hakuna mwenye miliki ya wananchi, wananchi ndiyo ninyi. Tumepeana tu majukumu, niwaombe sana vijana msiharibu nchi yenu. Fuateni serikali yenu inavyowaambia, fuateni katiba yenu inavyowaelekeza,” alibainisha.
Dk. Samia alitoa wito kwa vijana kujitokeza kwa wingi kupigakura kwani ndiyo haki ya msingi kidemokrasia.
Alieleza kuwa, hakuna mfumo uliowekwa kuhusu siasa safi kwani siasa safi ni kuhakikisha nchi na wananchi wapo salama ikiwemo kujumuishwa katika maamuzi.
Alibainisha kuwa, serikali imekuwa ikiunda kamati kukusanya maoni kuhusu masuala mbalimbali yenye kuhusu maendeleo ya nchi.
“Hata panapotokea mazonge katika nchi tunaunda tume kuja kuwauliza, mnatoa maoni yenu. Hiyo ndiyo siasa safi. Mnapokerana mnaitana kuzungumza, tuyazungumze, tuelewane, twende pamoja hiyo ndiyo siasa safi,”alisema.
Alieleza kuwa, hayo ndiyo mambo ambayo Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere aliyoyasimamia ambapo serikali zote za CCM zimekuwa zikitekeleza.
Dk. Samia alisema kwa sasa watu wenye ulemavu wanapata haki zao za msingi kama mtu yeyote nchini kwani serikali inatekeleza ipasavyo maazimio ya kimataifa na sheria zilizopo nchini.
Alieleza kuwa, katika eneo la kujenga utu wa mwananchi serikali imefanyakazi kubwa.
Kuhusu ardhi, alisema Tanzania ina eneo kubwa la ardhi ambayo imegawanyika katika makundi mbalimbali.
Alisema karibu asilimia 40 ya ardhi ni maeneo ya hifadhi na mbuga za wanyamapori.
“Kwa nini ni hifadhi kwa sababu watu tunaongezeka basi wale watakaokuja wakute ardhi ipo inawasubiri. Wazee wetu wangetumia yote tusingekuta maeneo.
“Tuna ardhi kubwa lakini tulikuwa na tatizo katika kupanga, kiwanja kimoja kilikuwa kinagawiwa kwa watu wawili hadi watatu hasa hapa Dar es Salaam,” alieleza.
Alisema kwa sasa vitendo hivyo, vimedhibitiwa na serikali ipo katika mkakati wa kupima ardhi nyingine ikiwemo eneo la madini.
MIGIRO
Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Dk. Asharose Migiro, alisema baada ya Dk. Samia kushika uongozi alizitembea nchi zenye vyama rafiki na CCM kwa lengo la kuimarisha uhusiano.
Miongoni mwa vyama hivyo ni FRELIMO (Msumbiji) ANC (Afrika Kusini) CNDD – FDD (Burundi) NRM (Uganda) SWAPO (Namibia) ZANUPF (Zimbambwe) na CPC (China).
CHATANDA
Mratibu wa uchaguzi Mkoa wa Dar es Salaam, Mary Chatanda, alisema wameshirikiana na viongozi wa chama mkoa huo katika kuhakikisha ushindi kwa CCM.
Alieleza kuwa serikali inayoongozwa na Dk. Samia, imetekeleza vyema ilani ya uchaguzi ya CCM (2020 – 2025) katika sekta mbalimbali nchini.
MTEMVU
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Abbas Mtemvu, aliwasilisha salamu kutoka kwa Wazee wa Dar es Salaam kwamba, kelele za mitandaoni ni za watu waliokosa staha.
WENJE
Aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Kanda ya Victoria, Ezekia Wenje, alisema huu ndiyo mwisho wa chama hicho kwa sababu kimewahadaa Watanzania.
Alisema CHADEMA kususia uchaguzi siyo suluhisho la utatuzi wa changamoto bali jambo sahihi ni kufanya mazungumzo.
Kwa upande wake, Mgombea Ubunge Jimbo la Kisarawe, Selemani Jafo, alisema uboreshaji wa upatikanaji umeme umewezesha viwanda kufanyakazi kwa ufanisi zaidi.
Alieleza kuwa, Tanzania kwa muda mrefu ilikuwa na changamoto ya sukari kwani mahitaji yalikuwa tani 800,000 hata hivyo baada ya jitihada za Dk. Samia uzalishaji sukari umeongezeka.
Mgombea Ubunge Jimbo la Iramba na Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba, alisema Dk. Samia amejenga shule za msingi zaidi ya 2,700 na shule za sekondari zaidi ya 1,000.
Alibainisha kuwa, kwa mara ya kwanza Tanzania imeingia katika historia ya kufanya uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji kwa kutumia fedha za ndani.
Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Mkoa wa Dar es Salaam, Nasra Mohammed, aliyataja mambo matatu ambayo vijana wameguswa kumpigia kura Dk. Samia.
Alisema sababu ya kwanza ni Dk. Samia kuongeza fedha za kujikimu kwa wanafunzi wa vyuo vikuu kutoka sh. 8,500 hadi sh. 10,000.
Pia, alisema Dk. Samia ameongeza bajeti ya mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu kutoka sh. bilioni 400 hadi sh. bilioni 900.
Naye, Mgombea Ubunge Jimbo la Temeke, Mariam Kisangi, alibainisha kuwa, katika miundombinu kupitia mradi wa DMDP sh. bilioni 43.7 zitatumika kujenga barabara kilometa 16 pamoja na vivuko sita.
Alisema katika eneo la Vituka watanufaika ujenzi wa barabara Voda – Vituka na Mashine ya Maji – Azimio ambayo itajengwa kwa fedha za ndani.
Mgombea Ubunge Jimbo la Mbagala, alisema wakazi wa jimbo hilo, wamenuifaka kupitia mradi wa mabasi ya mwendokasi ambapo wananchi wanatumia dakika 20 kufika katikati ya jiji.
Kwa upande wake, Mgombea Ubunge Jimbo la Chamazi, Abdallah Chaurembo, alimpongeza Dk. Samia kwa kuleta miradi mikubwa ya maendeleo katika jimbo hilo.
Alisema katika miaka mitano shule za maghorofa za msingi na sekondari zimejengwa katika Wilaya ya Temeke.
Mgombea Ubunge Jimbo la Kigamboni, Allan Sanga, alisema jimbo hilo limefanikiwa kupata sh. bilioni 38 zilizotumika katika miradi ya maendeleo na uwezeshaji wananchi kiuchumi.
Alieleza kuwa, Dk. Samia amejenga miundombinu ya barabara kwani ametengeneza historia kwa kufungua barabara za Mwasonga hadi Kimbiji kwa zaidi ya kilometa 40.
Pia, Mgombea Ubunge Viti Maalum, Stella Ikupa, alieleza kuwa, katika Mkoa wa Dar es Salaam wenye majimbo 12 wananchi wameeleza hawana mgombea mwingine mbadala zaidi ya Dk. Samia.




