Na ATHNATH MKIRAMWENI
JUMLA ya wanafunzi 898,755 wanatarajiwa kufanya Upimaji wa Kitaifa wa Kidato cha Pili kuanzia Novemba 10 hadi 20, mwaka huu.
Upimaji huo utafanyika katika shule 6,238 za sekondari nchini.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA), Profesa Said Mohamed, amesema jumla ya wanafunzi 889,266 wamesajiliwa kufanya upimaji huo, ambapo 396,383 ni wavulana (asilimia 44.57) na 492,883 ni wasichana (asilimia 55.43).
Amesema jumla ya wanafunzi 9,489 wa kujitegemea wamesajiliwa, kati yao wavulana ni 4,454 na wasichana 5,035.
Wanafunzi wenye mahitaji maalum pia watahusika katika upimaji huo ambapo waliosajiliwa ni 4,390, wakiwemo wenye uoni hafifu 1,674, wasioona (144), uziwi (999), ulemavu wa viungo (1,374), na ulemavu wa akili (199).
Amesema maandalizi maalumu yamefanyika, ikiwa ni pamoja na matumizi ya mitihani yenye maandishi ya nukta nundu na maandishi yaliyokuzwa kwa wanafunzi wenye uoni hafifu
Upimaji wa Kitaifa wa Kidato cha Pili ni muhimu kwa wanafunzi kwa sababu, unatoa fursa ya kutathmini uwezo wao baada ya miaka miwili ya masomo. Matokeo ya upimaji huu yatatumika kutathmini ubora wa ufundishaji na kujifunza katika shule za sekondari, na pia kuwasilisha ripoti kwa wadau wa elimu ili kuboresha mtaala na mbinu za ufundishaji.
Amesema Baaraza la Mitihani la Tanzania (NECTA) limekamilisha maandalizi ya upimaji, ikiwa ni pamoja na usambazaji wa karatasi za mitihani na nyaraka muhimu kwa shule zote.
Kamati za Mitihani za mikoa na halmashauri pia zimeandaa semina kwa wasimamizi wa mitihani na kuweka mikakati ya kuhakikisha usalama wa vituo vyote vya mitihani.
Pia Baraza limetoa wito kwa Kamati za Mitihani kuhakikisha kuwa usalama wa vituo vyote vya mitihani unazingatiwa na kwamba mazingira ya mitihani ni salama.
“Wasimamizi wote walioteuliwa wanatakiwa kusimamia mitihani kwa weledi na uadilifu wa hali ya juu, na kuhakikisha kuwa wanafunzi wanapata haki zao, hususan wanafunzi wenye mahitaji maalum,”amesema
Vilevile Baraza la Mitihani linawaamini wanafunzi wote wameshaandaliwa vyema kwa kipindi chote cha miaka miwili ya elimu ya sekondari hivyo wanatakiwa kufanya mitihani kwa kuzingatia kanuni za mitihani na kuepuka vitendo vya udanganyifu.
Pia mwanafunzi yeyote atakayebainika kujihusisha na udanganyifu atakumbana na hatua za kisheria.
Profesa Mohamed amewataka wamiliki wa shule kutambua kuwa shule zao ni vituo maalum vya mitihani, na hawatakiwi kuingilia majukumu ya wasimamizi wa mitihani. Wakuu wa shule pia wanatakiwa kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia mwongozo wa usimamizi wa mitihani.
Hata hivyo Baraza la Mitihani la Tanzania linawaomba wadau wote wa elimu na wananchi kwa ujumla kutoa ushirikiano wakati wa uendeshaji wa upimaji.




