Na Mwandishi Wetu,
Zanzibar
KATIBU wa Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu ya CCM, Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis, amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, na Rais wa Zanzibar ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, wamekula kiapo cha kuwalinda Watanzania kwa mujibu wa Katiba, hivyo wananchi hawapaswi kuyumbishwa na wachochezi wa uvunjifu wa amani kutoka ndani au nje ya nchi.
Akizungumza na waandishi wa habari leo (6 Novemba 2025) katika Ofisi Kuu ya CCM Kisiwandui, Mbeto amesema viongozi hao wanatekeleza wajibu wao wa kikatiba wa kuwalinda wananchi na kulinda utu wao dhidi ya watu wasiolitakia mema Taifa.
“Viongozi wetu wanatekeleza takwa la kikatiba. Wananchi wanapaswa kujiepusha na vitendo vya uvunjifu wa amani, hasa wakati huu ambapo hatua zaidi zinaendelea kuchukuliwa dhidi ya waliopanga na kuchochea vurugu za Oktoba 29, 2025,” amesema Mbeto.
Amesisitiza kuwa amani ni tunu ya Taifa, hivyo kila Mtanzania ana wajibu wa kuilinda, na kwamba nchi haitashurutishwa na mtu, kikundi, au taifa la kigeni katika utekelezaji wa mambo yake ya ndani.
Mbeto amewaasa hasa vijana kukataa kutumika kuvuruga amani na kusababisha uharibifu wa mali, akisema ikipotea, amani ni vigumu kuirudisha.
Aidha, ametumia nafasi hiyo kuwapongeza Rais Dkt. Samia na Rais Dkt. Mwinyi kwa ushindi wa kishindo walioupata katika Uchaguzi Mkuu uliopita, akisema matokeo hayo yanaonyesha imani kubwa ya Watanzania kwa viongozi hao.
Katika uchaguzi huo, mgombea wa CCM kwa nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano, Dk. Samia Suluhu Hassan, alipata zaidi ya asilimia 97 ya kura, huku mgombea wa CCM kwa nafasi ya Rais wa Zanzibar, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, akiibuka na ushindi wa asilimia 74.08.




