Na HAPPINESS MTWEVE,
Dodoma
JESHI la Kujenga Taifa (JKT), limewataka watu waliofungua mitandao ya kughushi, kwa kutumia jina, nembo, rangi, namba za vikosi, majina ya vikosi au kambi, kuzifunga mara moja akaunti hizo.
Onyo hilo lilitolewa jijini hapa kwa vyombo vya habari na Kurugenzi ya Mawasiliano JKT Makao Makuu.
Pia, lilisisitiza yeyote atakayebainika anaendelea kutumia akaunti hizo za mitandao ya kijamii atachukuliwa hatua kali za kisheria.
Taarifa hiyo ilifafanua katika utekelezaji wa majukumu yake, JKT imekuwa na utaratibu wa kutoa taarifa zinazohusu shughuli zake kupitia vyombo vya habari au mitandao ya kijamii nchini.
“Tuna tovuti ambayo ni www.jkt.tz na mitandao ya kijamii ya JKT kwa Instagram ni jkttanzania na YouTube JKTTanzania au Twitter (x) ni JKTonline tz,”ilifafanua taarifa hiyo.
Jeshi hilo limedai hivi karibuni kumejitokeza baadhi ya watu kufungua akaunti za kughushi katika mitandao ya kijamii kwa kutumia jina, nembo na rangi za JKT na kuaminisha umma akaunti hizo za jeshi hilo la kujenga taifa.
Ilisema akaunti hizo, zimekuwa zikipakia maudhui yenye kuleta taharuki kwa jamii kuhusiana na shughuli zinazofanywa na JKT.
“Tunakumbusha wananchi kuendelea kupata taarifa sahihi zenye uhakika zinazolihusu kutoka makao makuu ya JKT,” iliongeza taarifa hiyo.




