NA MWANDISHI WETU,
RIYADH
KATIBU Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk. Hassan Abbasi, ameihakikishia jumuiya ya kimataifa kuwa hali ya amani na utalii nchini Tanzania iko imara, kufuatia machafuko yaliyotokea katika baadhi ya maeneo wakati na baada ya uchaguzi.
Dk. Abbasi ametoa kauli hiyo leo Novemba 9, 2025, jijini Riyadh, Saudi Arabia, alipokuwa akiongoza ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa 26 wa Baraza Kuu la Shirika la Utalii Duniani (UN Tourism).
Akizungumza wakati akichangia Taarifa ya Utekelezaji ya Mwaka ya Shirika hilo, Dk. Abbasi amesema Tanzania imeendelea kunufaika na programu mbalimbali za UN Tourism, ikiwemo uandaaji wa Mkutano wa Dunia wa Utalii wa Vyakula kwa Kanda ya Afrika uliofanyika Arusha Aprili mwaka huu, pamoja na ufadhili wa miradi ya utunzaji wa mazingira katika Safu za Milima ya Usambara.
“Baada ya changamoto za uchaguzi, Serikali imefanya jitihada kubwa kurejesha hali ya utulivu nchini. Tanzania ni salama, vivutio vyetu vyote viko salama, na tunawakaribisha wajumbe wa mkutano huu na wadau wa utalii kuendelea kutembelea nchi yetu — kivutio bora cha utalii barani Afrika,” amesema Dkt. Abbasi.
Aidha, Tanzania imeendelea kuimarisha nafasi yake ndani ya shirika hilo, ikiwa ni miongoni mwa nchi 32 pekee kati ya wanachama 160 waliochaguliwa kuwa wajumbe wa Kamati ya Utendaji (Executive Committee).
Pia, Baraza Kuu hilo limeipitisha Tanzania kuwa Mjumbe wa Kamati ya Kuhakiki Wanachama (UN Tourism Credentials Committee).
Mkutano huo unaendelea jijini Riyadh, ambapo pamoja na masuala mengine, utajadili matumizi ya akili bandia (AI) katika kutangaza utalii na uchaguzi wa Katibu Mtendaji mpya wa shirika hilo.






