Na NASRA KITANA
WAKATI kikosi cha timu ya Taifa Stars kikiwa nchini Misri kwa ajili ya maandalizi ya mwisho ya mchezo dhidi ya Kuwait, wachezaji wa timu hiyo wameweka wazi kuwa watahakikisha wanapambana kwa jasho na damu ili kupata ushindi.
Stars inatarajiwa kushuka dimbani kumenyana na Kuwait katika mchezo wa kimataifa wa kirafiki wa Kalenda ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) utakaochezwa Jumamosi ya wiki hii, Uwanja wa Al Salam jijini Cairo nchini Misri saa 1:00 usiku.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, beki wa timu hiyo, Shomari Kapombe alisema kuwa wamejipanga vizuri kuhakikisha wanapata ushindi katika mchezo huo.
Kapombe alisema kuwa kila mchezaji yupo tayari na mchezo huo kwani kila mmoja ana morari ya kutosha kuhakikisha wanatumia vyema nafasi watakazozipata kupachika mabao.
“Tumejipanga vizuri kuelekea katika mchezo huo, tunajua ni mchezo mgumu na wenye changamoto kubwa lakini tutahakikisha tunapambana mwanzo hadi mwisho ili kupata matokeo mazuri,” alisema Kapombe.
Akimzungumzia Kaimu Kocha Mkuu, Miguel Gamondi, Kapombe alisema mabadiliko hayo hayataathiri chochote katika timu yao kwani ni kocha ambaye wanamfahamu.
Nyota huyo aliwataka mashabiki na wapenzi wa soka nchini kuendelea kuipa sapoti ya kutosha timu yao ili iweze kufanya vizuri katika mechi itakazocheza.
Naye nyota wa timu hiyo, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, alisema kuwa kama wachezaji wamejipanga vizuri ili kuweza kupata ushindi katika mchezo huo muhimu.
Tshabalala alisema kuwa kila mchezaji anajua jukumu lake ndiyo maana hawatakubali kuona wanapoteza mchezo huo.
Alisema kuwa mchezo huo ni moja ya maandalizi mazuri kuelekea katika mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON), itakayofanyika kuanzia mwezi ujao nchini Morocco.
“Kila mchezaji anajua umuhimu wa mchezo huo dhidi ya Kuwait, tumejipanga vizuri kuhakikisha tunapata ushindi katika mchezo huo muhimu, wachezaji wote wana morari ya kutosha kwa ajili ya kupambania taifa lao,” alisema Tshabalala.
Dikson Job alisema kuwa kila mchezo una umuhimu kwao, hivyo hawaangalii kama ni wa kirafiki au mashindano, mipango yao ni kupambana na kupata matokeo chanya.
“Kila mchezaji yupo tayari na amejipanga vyema kuhakikisha wanapambana ili kupata matokeo mazuri, tunaenda kupambania ushindi ili kuendelea kuipa heshima timu yetu,” alisema Job.
Kuhusu kocha mpya, Job alisema Gamondi ni kocha ambaye anamfahamu hivyo haitakuwa ngumu kwao kufuata maelekezo ambayo atawapatia.




