NA SELINA MATHEW, Dodoma
WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda amesisitiza kutovumilia wakandarasasi na watendaji wazembe watakaokwamisha kukamilika kwa utekelezaji mradi wa ujenzi wa Uwanja wa Soka wa Arusha na uboreshaji miundombinu ya michezo nchini ambayo itatumika katika fainali za michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2027).
Michuano hiyo msimu ujao inatarajia kufanyika katika nchi tatu za Tanzania, Kenya na Uganda.
Amewataka wakandarasi wanaotekeleza miradi hiyo kuhakikisha inakamilika kwa mujibu wa mkataba na siyo vinginevyo.
Makonda aliyasema hayo bungeni jioni, wakati akichangia hotuba ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan aliyoitoa katika Bunge, Novemba, mwaka jana ambayo ilihitimishwa juzi.
Alisema Dk. Samia amewekeza katika miundombinu ya michezo ambapo kiasi cha sh. trilioni 1.27 zimetolewa kubadilisha mazingira na kuwatenegenezea vijana mazingira mazuri kupitia sekta hiyo.
“Mfano uwanja wa mpira wa Arusha ambao unajengwa umeshazidi asilimia 70 ya ujenzi ambapo sh. bilioni 338 zinatumika, mkandarasi ameshalipwa sh.bilioni 55 katika mkataba.
“Kadhalika, viwanja vya mazoezi vya AFCON 2027 sh. bilioni 51, ukarabati Uwanja wa Benjamin Mkapa sh. bilioni 31, Uwanja wa Uhuru sh.bilioni 19, Rais Dk. Samia amedhamiria kubadilisha na kujenga miundombinu ya michezo kwa ajili ya kizazi cha sasa na baadae,” alisema Makonda.
Makonda alitoa rai kwa wasimamizi na wajenzi wa miradi hiyo ambao ni wizara na wakandarasi kuhakikisha wanafanya kazi kwa mujibu wa mkataba.
“Tunataka viwanja vikamilike kabla ya mashindano ya AFCON 2027, vitabeba sura ya taifa na kuliweka katika ramani ya dunia kwa namna ya jinsi ndoto ya Rais Dk. Samia alivyotaka.
“Sitamvumilia mtu yeyote atakayekuwa mzembe, atakayeshindwa kukamilisha miradi hii kama ambavyo mikataba inataka,” alisema.
Pia aliipongeza Taifa Stars ambayo iliingia katika hatua ya 16 bora ya michuano ya AFCON 2025, iliyomalizika hivi karibuni nchini Morocco.
Waziri Makonda alisema serikali inakuja na mipango mizuri kuhakikisha kila mkoa unakuwa na timu yake ili kuweka ushindani wa michezo nchini.
“Tunatamani kuwa na mifumo ya kuandaa vijana katika umri mdogo waliopo shule wapate fursa ya kutumia nafasi ambayo Mwenyezi Mungu amewapa kupitia vipaji vyao ambapo shule 56 za mfano zinajengwa kwa ajili ya kuwatenegeneza watakaofanya vizuri.
“Ninawaomba wakuu wa mikoa, kila mkoa iwepo timu ya mkoa ili kuwatengenezea mazingira mazuri vijana wenye vipaji.
“Pia, mashirika ya umma yamiliki timu za mpira wa soka ili kuongeza hamasa, tuhakikishe watu wanashiriki michezo kila mahali,” alisema Makonda.



