MAKAMU wa Rais, Dk. Philip Mpango, ametoa maagizo sita ya kuzingatia kwa wenyeviti wa bodi na watendaji wakuu wa mashirika ya umma, katika kuleta ufanisi wa shughuli za mashirika hayo.
Maagizo hayo ni kudhibiti upotevu na ubadhirifu wa rasilimali za umma, ushirikiano na taasisi za kimataifa, kuongeza weledi na utafiti, utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050, kukamilisha mchakato wa urekebishaji sheria ya uwekezaji wa umma na kupunguza utegemezi wa serikali.
Dk. Mpango, alitoa maagizo hayo jijini Arusha, jana, katika kikao kazi cha wenyeviti wa bodi na watendaji wakuu wa taasisi za umma.
“Jambo la kwanza ni kudhibiti upotevu na ubadhirifu wa rasilimali za umma, mashirika ya umma, yaweze kujenga mazingira ya ushindani ni lazima kulinda rasilimali zilizopo ambazo ni nyenzo muhimu katika kufikia azma hiyo.
“Pamoja na kuanzishwa mifumo ya kukusanyia mapato kama GPG, TAUSI na kadhalika na kusajili mashine za kukusanyia mapato, bado kuna upotevu mkubwa wa fedha za serikali kama ripoti za CAG za kila mwaka zinavyoonesha.
“Kwa hiyo, ninahimiza taasisi na mashirika yote ya umma, kuimarisha usimamizi wa matumizi ya fedha, kudhibiti manunuzi na kuimarisha usimamizi wa mikataba pamoja kusimamia vyema rasilimali watu,” alisema.
Dk. Mpango, aliwaagiza wenyeviti na watendaji wakuu wa mashirika ya umma, kuimarisha uhusiano wa kitaasisi kati ya mashirika hayo na taasisi za kimataifa katika kunufaika na teknolojia, masoko, utafiti na utamaduni wa kufanya kazi.
“Kwa mfano TANESCO na REA, wanaweza kabisa kushirikiana na kampuni za kimataifa katika uzalishaji na usambazaji wa nishati safi na nafuu, lakini kadhalika, shirika letu la Reli, lina fursa ya kushirikiana na kampuni kama yale ya kutoka Korea Kusini au China katika usafirishaji wa mizigo na abiria.
“Kuifanya Tanzania yetu kuwa lango na kitovu cha biashara Afrika Mashariki, Kati na Kusini, pia Mashariki ya Kati na hata mashariki ya mbali,”alisema.
Dk. Mpango, alisema kuwepo kwa ushirikiano wa kimkakati na endelevu, ni uwekezaji wa muda mrefu, unaohitaji uaminifu, uvumilivu na mshikamano.
Akizungumzia weledi na kukuza utafiti, Dk. Mpango, alisema mashirika ya umma, yanapaswa kuongeza bidii ya weledi katika kufanya kazi ikijumuisha ubunifu na ustadi wa katika uzalishaji na utoaji wa huduma.
Alisema utafiti ni muhimu na una mchango mkubwa katika kukuza uchumi, kuleta teknolojia mpya, ubora wa huduma na utendaji wa kazi.
Aliwasisitiza wenyeviti wa bodi na watendaji wakuu wa mashirika hayo, kuzingatia utafiti katika kuyaendesha mashirika hayo.
Aidha, katika utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050, Dk. Mpango, alisema jitihada zinapaswa kufanywa malengo yatimie kwa kuwa, mashirika hayo yamebeba dhima kubwa ya kufikia malengo hayo.
Dk. Mpango, alisema dira hiyo, imetoa mwelekeo wa uchumi wa nchi kwa miaka 25 ijayo, ikiwemo kuwa na uchumi wa kipato cha kati cha juu chenye thamani ya Dola za Marekani trilioni moja, hivyo kufikia azma hiyo, lazima uchumi wa nchi, unapaswa kukua kwa wastani wa asilimia 10 kwa mwaka.
Alisema katika kipindi cha miongo miwili iliyopita uchumi nchini, umekuwa ukikua kwa asilimia 6.2, hivyo ni muhimu mashirika ya umma na binafsi, kuweka mikakati ya kuchangia pato la taifa kufikia lengo la Dira ifikapo 2050.
Akizungumzia kukamilisha mchakato wa kutunga sheria ya uwekezaji wa umma, Dk. Mpango alirejea maelekezo ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, aliyoyatoa kwa Waziri wa Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, kipindi alipopokea gawio la mashirika hayo mwaka huu.
Pia, alirejea maagizo ya Rais Dk. Samia, kwa Msajili wa Hazina, Nehemia Mchechu ya kufuatilia utendaji wa mashirika ya umma huku akimpongeza msajili kwa kazi nzuri.
Makamu wa Rais aliielekeza kazi hiyo ikamilike kwa haraka, kufikia malengo ya serikali.
Kuhusu mashirika ya umma kupunguza utegemezi kwa serikali, aliyaelekeza mashirika ya umma, kuweka mikakati ya kupunguza utegemezi wa serikali na kuchangia katika mfuko mkuu wa serikali ifikapo mwishoni mwa mwaka huu wa fedha.
Aliyapongeza baadhi ya mashirika ya umma yaliyopunguza utegemezi wa serikali na hivi sasa yanajilipa mishahara.
“Hapa napenda kuyapongeza mashirika ambayo tumeambiwa ni TANESCO, STAMICO na TPDC, ambayo yalikuwa yanalipiwa mishahara na serikali shilingi bilioni 19.2 kwa mwaka, hivi sasa yanajitegemea na yamepunguza mzigo kwa serikali, ninayataka mashirika mengine yafuate mfano huu,” alisema.
Alilitaka Shirika la Reli Tanzania (TRC), kuzingatia ufanisi na mapato yake hayamezwi na gharama za reli ya kati, ambayo imekuwa haifanyi vizuri.
Akizungumzia uwekezaji wa serikali katika mashirika ya umma, alisema imewekeza sh. trilioni 86.29 katika mashirika hayo kutokana na umuhimu wake kwa uchumi wa nchi.
Alisema serikali imewekeza katika mashirika hayo kwa kuwa, yamekuwa yakinufaisha jamii moja kwa moja, kutoa ajira endelevu na kuchangia pato la taifa.
Kutokana na hilo, alisema Serikali ya Awamu ya Sita, imeweka usimamizi madhubuti wa mashikrika hayo chini ya Msajili wa Hazina kuhakikisha tija iliyokusudiwa inapatikana.
Kuhusu mafanikio ya mageuzi katika mashirika ya umma, alisema yameonesha matokeo chanya kutokana na kazi nzuri inayofanywa na Ofisi ya Msajili wa Hazina.
Dk. Mpango, alisema katika mashirika hayo, kumekuwa na ongezeko la mapato yasiyo ya kodi kutoka sh. bilioni 753.9 mwaka 2019 hadi 2020 na kufikia sh. trilioni 1.28 hadi kufikia kipindi cha mwaka jana, likiwa ni ongezeko la asilimia 37.
Alisema matarajio ya ongezeko la mapato hayo ni kufikia sh. trilioni mbili kwa mwaka wa fedha wa 2025/2026.
Katika hatua nyingine, aliwataka viongozi hao, kujitokeza kupiga kura katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, mwaka huu.
PROFESA KITILA MKUMBO
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, alisema serikali imezindua Dira ya Taifa ya mwaka 2025-2050, yenye malengo na shabaha ndefu ambayo itatekelezwa na mashirika ya umma pamoja sekta.
“Tunatarajia mashirika ya umma yatuongoze katika majukumu matano, Dira ya Taifa ya mwaka 2025-2050 itekelezeke kikamilifu kwa kuzingatia majukumu makuu matano,”alisema.
Profesa Kitila alitaja mambo hayo ni ujenzi wa miundombinu ya uchumi, kuwezesha sekta binafsi na siyo kuwa washindani,
NEHEMIA MCHECHU
Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu , alisema mkutano huo wa siku tatu, umehudhuriwa na washiriki zaidi ya 650 ambapo baadhi ya mashirika ya umma, yameimarika likiwemo Shirika la Umeme (TANESCO), Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC).
Alisema wameweka malengo ya kuhakikisha mashirika ya umma, yanachangia asilimia 10 ya bajeti kuu ya serikali ifikapo mwaka 2028, kutoka asilimia tatu hadi nne za hivi sasa ambazo zitahamasishwa kutoa tuzo kwa mashirika ya umma yatakayofanya vizuri mwaka hadi mwaka.
“Ongezeko la thamani ya uwekezaji wa serikali katika taasisi na mashirika Umma kwa sasa umefikia shilingi trilioni 86.29 sawa na ongezeko la asilimia 32 ikilinganishwa na mwaka 2019/20, limechagizwa na uwekezaji katika sekta za kimkakati.”alisema.