NA MUSSA YUSUPH
MGOMBEA Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, ametaja vipaumbele muhimu vitakavyotekelezwa ndani ya siku 100 baada ya kuchaguliwa kuunda serikali.
Amesema serikali yake itajikita kuleta mabadiliko yatakayogusa moja kwa moja maisha ya wananchi katika kipindi cha miaka mitano ijayo.
Miongoni mwa vipaumbele hivyo ni ajira 12,000 kwa walimu na wataalamu wa afya, bima ya afya kwa wote, na matibabu bure kwa wajawazito, wazee na watoto.
Akihutubia maelfu ya wananchi waliohudhuria uzinduzi wa kampeni za CCM, Dk. Samia alisema hospitali zitapigwa marufuku kuzuia miili ya marehemu kwa sababu ya deni la matibabu.
Aidha, aliahidi serikali kugharamia vipimo vya afya vya gharama kubwa kwa wananchi wasiokuwa na uwezo na kuajiri watumishi 5,000 wa sekta ya afya ndani ya siku 100.
Katika sekta ya elimu, alisema mkakati mpya utahakikisha kila mtoto wa darasa la tatu anajua kusoma na kuandika sambamba na kuajiri walimu 7,000 wa hisabati na sayansi.
Serikali pia itazindua mpango wa ushirikiano kati ya vyuo, viwanda na sekta binafsi kuhakikisha wanafunzi wa ufundi wanapata mafunzo kwa vitendo.
Aliahidi kutenga shilingi bilioni 200 kwa ajili ya mitaji ya wajasiriamali wadogo, kuanzisha programu za mitaa ya viwanda wilayani na kuimarisha kilimo, uvuvi na mifugo.
Vipaumbele vingine ni kuanza ujenzi wa gridi ya taifa ya maji kutoka katika vyanzo vikuu na kuendeleza matumizi ya nishati safi kwa kupikia.
Dk. Samia alisema pia ataweka mifumo ya uwajibikaji wa viongozi, kuimarisha mashauriano na wadau, na kuunda tume maalum ya maandalizi ya katiba mpya.
MAFANIKIO MIAKA MINNE
Katika hotuba yake iliyoanza saa 10:48 jioni, Rais Dk. Samia Suluhu Hassan alitaja mafanikio makubwa yaliyopatikana katika kipindi cha uongozi wake, akisisitiza kuwa kupitia falsafa ya 4R, Tanzania imeendelea kuongoza kwa amani na utulivu kwa mujibu wa ripoti za kimataifa Afrika Mashariki.
Alisema alipoingia madarakani alikuta changamoto ya uhuru wa vyombo vya habari, ambapo alionesha utashi wa kisiasa kwa kuondoa kifungoni magazeti yaliyofungiwa, kuboresha sheria ya habari na kutoa leseni zaidi ya 1,000 kwa magazeti, redio 200, mitandao ya kijamii 300 na blogu 70.
Kuhusu mapambano dhidi ya rushwa, Dk. Samia alieleza kuwa serikali imeimarisha taasisi za CAG na TAKUKURU hali iliyosaidia Tanzania kupanda kutoka nafasi ya 87 hadi nafasi ya 82 kati ya nchi 170 duniani.
Aidha, aliongeza kuwa hali ya usimamizi wa fedha imeimarika, ambapo hati chafu zimepungua kutoka 10 mwaka 2021 hadi moja pekee mwaka jana, huku zenye mashaka zikishuka kutoka 81 hadi tano.
Akigusia uchumi, alisema bajeti ya serikali imeongezeka kutoka sh. trilioni 34.9 hadi 59.49 mwaka huu, huku deni la taifa likibaki salama kwa kuwa ni asilimia 46 ya pato la taifa ikilinganishwa na wastani wa asilimia 67 katika nchi za Afrika Mashariki.
Katika sekta ya madini, Dk. Samia alibainisha kuwa mchango wa wachimbaji wadogo umeongezeka kutoka asilimia 20 hadi 40, uzalishaji wa almasi umeongezeka kutoka karati 213,948 hadi 373,252, na viwanda vya uchakataji madini kuongezeka kutoka viwili hadi tisa.
Sekta ya utalii nayo imeimarika ambapo idadi ya watalii wa ndani na nje imeongezeka kutoka milioni 1.4 mwaka 2020 hadi milioni 5.3, huku mapato yakipanda kutoka dola milioni 700 hadi dola bilioni 3.9 mwaka jana.
Kwa upande wa kilimo, upatikanaji wa mbolea umeongezeka kutoka tani 600,000 hadi milioni 1.4, serikali imetoa ruzuku ya sh. bilioni 708, na mauzo ya mazao kupitia minada ya kimataifa yameongezeka kutoka sh. trilioni 1.1 hadi trilioni 4.2 mwaka huu, huku mauzo nje ya nchi yakifikia trilioni 9.2.
Akizungumzia miradi ya miundombinu, alisema reli ya kisasa ya SGR kipande cha Dar es Salaam – Morogoro kimekamilika, Morogoro – Makutupora kikiwa asilimia 97.9, huku vipande vingine vikikamilika kwa viwango tofauti. Aidha, ujenzi huo umetengeneza ajira zaidi ya 9,000 na unatarajiwa kuongeza kasi ya biashara na usafirishaji mizigo.
Vilevile, alisema serikali imeingia makubaliano na Zambia kuboresha reli ya TAZARA kwa mkataba wa dola bilioni 1.4, na Bandari ya Dar es Salaam imeongeza uwezo wa kushughulikia mizigo kutoka tani milioni 17 hadi milioni 27 huku muda wa kutia nanga ukipungua.