Na AMINA KASHEBA
WASANII wa muziki bongo, Nasib Abdul ‘Diamond’, Rajab Kahali ‘Harmonise’ na kundi la singeli la Miso Misondo, jana walifunika kwa kutoa burudani ya aina yake katika uzinduzi wa kampeni ya uchaguzi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), uliofanyika Uwanja wa Tanganyika Packers, Kawe, jijini Dar es Salaam.
Wasanii hao walitoa burudani ya aina yake na kukonga nyoyo za maelfu ya watu waliojitokeza katika uzinduzi huo ambapo walionekana kuimba nao nyimbo mbalimbali.
Mastaa hao wa muziki, waliporomosha burudani ya aina yake kwa kuimba nyimbo tofauti zikiwemo zitakazotumika katika kipindi cha kampeni na kuwafanya waliohudhuria kucheza nao sambamba muda wote.
Miso Misondo walionyesha umahiri mkubwa wa kulitawala jukwaa kutokana na staili yao ya kipekee ya kucheza na makoti kitu kilichoibua shangwe uwanja mzima.
Miso Misondo waliibua shangwe baada ya kupanda jukwaani kutoa burudani kwa kucheza staili mbalimbali za muziki wa aina ya singeli na kuwavutia mashabiki wao.
Kutokana na staili hiyo uwanjani hapo watu ambao walijitokeza katika ufunguzi huo walionekana kuwafurahia zaidi wasanii kwa burudani ya aina yake.
Baada ya kushuka jukwaani, kiongozi wa kundi hilo anayejulikana kwa jina la Miso, alisieitiza kwamba amefarijika kuona umati wa watu ukiwashangilia kwani wanaonekana wanakubalika na kwa kiasi kikubwa.
Alisema walipata nafasi ya kufanya onyesho hilo katika uzinduzi wa kampeni, hivyo wataendelea kumuunga mkono Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kusambaza ujumbe kwa jamii ili wamchague katika uchaguzi utakaofanyika Oktoba 29, mwaka huu.
“Kwetu ni furaha kuona watu wengi kiasi hichi wanafurahia burudani yetu tuliyoitoa, hivyo tutaendelea kueneza ujumbe kwa jamii kuhakikisha tunamchagua Rais Dk. Samia kwa kishindo,” alisema.
Mbali na wasanii hao, wengine waliotoa burudani ni Mbwana Kilungi ‘Mbosso’, Rashid Makwiro ‘Chid Benzi’, Barobaro, bendi ya T.O. T, Mrisho Mpoto, Zanzibar One, Kidene Fighter na Raymond Mwakyusa ‘Ravyann’.