Na NJUMAI NGOTA, Mwanza
MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Mwanza, Michael Lushinge ‘Smart’, amesema wamejiandaa kikamilifu kushiriki uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 29, mwaka huu, huku akimwakikishia Mgombea Mwenza wa Urais wa Chama, Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi kuwa Mgombea wa Urais wa CCM, Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, atapata kura za kishindo mkoani humo.
Lushinge amesema hayo Kata ya Mwankulwe, wilayani Kwimba, alipomkaribisha Mgombea Mwenza wa Urais, Balozi Dk. Nchimbi, kuzungumza na mamia ya wananchi waliohudhuria uzinduzi wa kampeni za CCM.
Amesema Rais Dk. Samia na Mgombea Mwenza wa Urais watapata kura za kutosha na za kishindo mkoani humo.
“Katika mkoa huu, nikuhakikishie kura za kishindo kwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan. kama unavyofahamu Kanda ya Mwanza na Kanda ya Ziwa, kura zitakuwa za kutosha na ni za kishindo, hivyo tumejipanga kikamilifu kushiriki uchaguzi mkuu.
“Sisi wana-Mwanza tunaingia katika uchaguzi tukiwa kifua mbele, hivi ninavyozungumza tuna mtaji rasilimali, wanachama zaidi ya 700,000 tayari wamejisajili katika mfumo wetu.
“Hao ni wanachama ambao tunawatambua, nikuhakikishie Mkoa wa Mwanza na wana-Kwimba kwa ujumla, tumejiandaa kikamilifu kwa uchaguzi,”amesema.
Amesema Chama kiliteua wagombea wazuri na walifuata utaratibu wa kidemokrasia, hivyo wana uhakika kitapata ushindi wa kishindo.
Ametoa wito kwa wananchi na wanaCCM kuendelea kuwa wamoja na kutunza amani ambayo ni tunu waliyoikuta na kuirithi kutoka kwa wazee wao.
Katika hatua nyingine, Mwenyekiti huyo amesema Balozi Dk. Nchimbi, alikitumikia Chama vizuri alipokuwa Katibu Mkuu na ameacha alama kubwa na mshikamano ndani ya CCM.
“Hakika Chama hivi sasa ni kipya, kipo katika muundo mzuri na thabiti, ninaomba nikushukuru kwa uongozi wako uliotukuka kwa kukiongoza ukiwa Katibu Mkuu,”amesema.
Mwenyekiti huyo alitumia fursa hiyo kumpongeza Katibu Mkuu wa Chama, Balozi Dk. Asha-Rose Migiro kwa kuteuliwa na kudhibitishwa na Mkutano Mkuu wa Halmashauri Kuu Taifa wa CCM.