Na NJUMAI NGOTA,
Mara
MGOMBEA Mwenza wa Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi, ameahidi iwapo watapata ridhaa ya kuongoza nchi katika kipindi cha miaka mitano ijayo, serikali itaendelea kuwawezesha vijana wanufaike na rasilimali za madini na kuwapa mitaji.
Pia, amewaomba wananchi kumchagua Mgombea Urais wa CCM, Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, wabunge na madiwani wa Chama, katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, mwaka huu.
Balozi Dk. Nchimbi ameyasema hayo, Nyamongo, wilayani Tarime, mkoani Mara, katika mkutano wa hadhara wa kampeni za Chama wa kuelezea mafanikio yaliyopatikana katika utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama ya mwaka 2020-2025 na kunadi Ilani mpya ya Uchaguzi ya CCM.
“Wana-Nyamongo kipekee ninawapongeza viongozi wa Chama na serikali, tulikuwa na changamoto kubwa ya vikundi vya vijana na leseni za madini, ninafurahi kwamba, taarifa niliyopewa kuna vikundi 55 vimeundwa ambavyo vina vijana 1800,” amesema.
Amesema vijana hao wapo katika mafunzo na vikundi hivyo vyote vimepewa leseni za uchimbaji madini.
Balozi Dk. Nchimbi amemshukuru Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evance Mtambi na serikali ya mkoa huo kwa kutekeleza kwa vitendo maelekezo Rais Dk. Samia.
Mgombea huyo wa Urais amesema kipindi cha miaka mitano ijayo iwapo watapata ridhaa ya kuongoza nchi wataboresha mfumo wa mawasiliano, kati ya viongozi wa serikali na wananchi, kuhakikisha shida zao zinafika serikalini kwa wakati, zifanyiwe kazi kwa haraka na zisimamiwe.
“Nipo hapa nikiwa ni msaidizi mkuu kwa wagombea wetu niwakikishie, nitakuwa naye bega kwa bega kuhakikisha yote yaliyoahidiwa katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama na ambayo yamepangwa kutekelezwa ndani ya siku 100 za kwanza wanayatekeleza,” amesema.
Akizungumzia baadhi ya kazi zilizofanyika kipindi cha miaka mitano wilayani Tarime Vijijini, Balozi Dk. Nchimbi alizitaja kuwa ni kukamilika kwa Hospitali ya Nyamwaga, ambayo ya kisasa, kuongezeka kwa vituo vya afya kutoka sita hadi 11.
Kazi nyingine zilizofanyika ni kuongeza zahanati kutoka 31 hadi kufikia 50 katika kuendeleza kusongeza huduma za afya kwa wananchi.
“Vilevile vituo vya mama na mtoto vimeongezeka kwani miaka mitano iliyopita vilikuwa 37, hivi sasa vipo 62 karibu mara mbili ya vilivyokuwepo awali na shule za msingi zimeongezeka kutoka 137 hadi 162,”alisema.
Mgombea Mwenza wa Urais alisema katika kipindi cha miaka mitano iliyopita shule za sekondari zilikuwa 38, lakini hivi sasa zipo 54 na madarasa yameongezeka kutoka 637 hadi 1,043.
“Maendeleo hayo hayahitaji miwani, kila mtu anaona, aliyefurahi anao na aliyekasirika anaona,” alisema
Ameongeza watu wanaopata maji safi na salama wameongezeka kutoka asilimia 51 hadi kufikia asilimia 73, vijiji 68 vilivyokuwa vinapata huduma hiyo ambapo hivi sasa vimefikia 88, barabara zaidi ya asilimia 56 zimeboreshwa.
Amesema katika kipindi cha miaka mitano ijayo wamedhamiria kuongeza idadi ya zahanati kutoka 50 hadi kufikia 70, vituo vya afya kutoka 11 hadi 20 vifanye huduma ya upasuaji na uzalishaji wa watoto.
Balozi Dk. Nchimbi amesema wamedhamiria huduma ya maji safi na salama kati ya watu 100, iwafikie asilimia 95 na ujenzi wa barabara maeneo mbalimbali wilayani humo.
Awali, Balozi Dk. Nchimbi akiwa anakwenda Nyamongo katika mkutano wa hadhara, alipita kuhani msiba wa kada wa CCM, John Mwita.
GAVU
Katibu wa NEC, Idara ya Oganaizesheni ya CCM, Issa Haji Gavu, alisema CCM ndicho Chama pekee chenye dhamira ya kweli ya kubadilisha maisha ya Watanzania,
Alisema CCM siyo chama cha msimu, bali kimeonesha nia ya dhati ya kubadilisha nchi kwa kuwaleta maendeleo, yakiwemo huduma nzuri za kijamii kwa wananchi wa wilaya hiyo.
Kwa mujibu wa Gavu, huduma za afya hivi sasa Tarime zimeboreshwa na kuwaahidi wananchi kuwapa maendeleo makubwa.
Aliwaomba wananchi wa wilaya hiyo kujitokeza kwa wingi Oktoba 29, mwaka huu, kupiga kura kwa kumchagua Mgombea wa Urais kupitia CCM, Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, Mgombea Mwenza Balozi Dk. Nchimbi, wabunge na madiwani.
PETER MSIGWA
Kada wa CCM, Peter Msigwa, alisema katika kipindi cha miaka minne ya Rais Dk. Samia amefanya mambo makubwa tangu alipoingia madarakani.
Alisema mageuzi makubwa yamefanyika katika sekta mbalimbali, ikiwemo miradi ya maendeleo na nidhamu ya kiuongozi.
Msigwa alibainisha hatua hiyo inaonesha taswira mpya ya Tanzania inayojengwa juu ya misingi ya huruma, maarifa na weledi.
Aliyataja mafanikio mengine yaliyopatikana katika kipindi hicho kuwa ni kuongezwa kwa ruzuku za mbolea kutoka hekta 580,000 hadi hekta 987,000, hivyo kufungua njia mpya ya wakulima wa Tarime na nchi nzima kushiriki katika utajiri wa dunia unaotokana na sekta hiyo.