Na NJUMAI NGOTA
MGOMBEA Mwenza wa Urais Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi, amesema hadi sasa wanachama nchi nzima wa CCM milioni 13.3 wamejiandikisha katika daftari la kudumu la wapigakura kushiriki Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, mwaka huu.
Amesema hakuna chama kingine chochote Afrika Mashariki na Kati kilichokuwa na nusu ya wanachama wa CCM na hiyo inatokana na rekodi ya Chama kwamba wananchi kukipenda Chama kinachojali maendeleo yao.
Balozi Dk. Emmanuel alisema hayo , alipohutubia katika mkutano wa hadhara uliofanyika uwanja wa Furahisha, uliopo wilayani Ilemela.
“WanaCCM waliojiandikisha ni milioni 13.3, hakuna chama kingine chochote Afrika Mashariki na Kati kinao japo nusu ya wanachama wa CCM na hiyo inatokana na rekodi ya Chama, wananchi wanapenda chama kinachojali maendeleo yao.
“Wananchi wanataka chama kinachotafakari kuhusu maisha yao ya baadaye, wanataka chama kinachohangaika na kero zao. Chama Cha Mapinduzi kwa kiwango kikubwa kimejithibitisha kuyatekeleza hayo,”alisema.
Balozi Dk. Nchimbi alisema katika viti vya madiwani mkoani humo, Chama kimepita bila kupigwa, hakijapata wagombea katika kata 91, ambapo wamepata wagombea katika kata 90.
Aidha, Dk. Nchimbi alitumia fursa hiyo kuwaomba wakazi wa Mwanza kumchagua Rais Dk. Samia, wabunge na madiwani na alitumia fursa hiyo kuwanadi wabunge wa mkoa huo.
Balozi Dk. Nchimbi alimwahakikishia ushindi wa kishindo kutoka kwa wakazi wa Mwanza, kutokana na maendeleo makubwa aliyoyafanya.
Alisema dalili za ushindi wa kishindo kwa CCM zimeanza kuonekana kupitia matokeo ya awali ya wagombea wa CCM kupata ushindi mkubwa wa nafasi za udiwani na ubunge jijini Mwanza.
Alisema kara 90 sawa na zaidi ya asilimia 50 ya kata zote za Mwanza wagombea wa CCM wamepita bila kupingwa.
Alisema hiyo ni heshima kubwa kutoka kwa wananchi na hiyo ishara kwamba lOktoba 29, mwaka huu wananchi wataipa CCM ushindi wa kihistoria.
Kwa mujibu wa Balozi Dk. Nchimbi, Mkoa jirani wa Geita una majimbo tisa, majimbo saba hayana wapinzani na CCM imepita bila kupingwa kata 91 kati ya kata 122.
Alisema wananchi wananchi wameonyesha kwa vitendo Imani waliyonayo kwa Chama na ni heshima kubwa kwa chama na wamethamini kazi kubwa ya maendeleo iliyofanywa.
Kwa mujibu wa Balozi Dk. Nchimbi, wananchi hawataki maneno, wanataka matokeo na CCM imeonesha kwa vitendo kwamba inajali, hivyo ushindi wa mapema katika kata na majimbo .
“Dalili hizi si za kawaida, ni dhihirisho la imani ya wananchi kwa chama chenye misingi ya kazi na utu,” alisema.
Alitoa wito kwa wananchi wote kujitokeza kwa wingi Oktoba 29 na kupiga kura kwa CCM kuhakikisha Tanzania inaendelea kusonga mbele kwa kasi ya maendeleo na uongozi wenye utu na kazi.
MAMBO YATAKAYOTEKELEZWA MWANZA
Alisema katika kipindi cha miaka mitano ijayo wamejipanga kutekeleza miradi ya kimkakati mkoani huo.
Balozi Dk. Nchimbi aliitaja baadhi ya miradi hiyo ambayo watatekeleza katika kipindi cha miaka mitano ni kukamilisha ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR kutoka Isaka hadi Mwanza, maji na upatikanaji wa meli mpya mbili.
Alisema Chama kimejipanga kutekeleza miradi mbalimbali katika mkoa huo ikiwemo elimu, afya, umeme na maji kwa kuhakikisha wananchi wanaendelea kunufaika na rasilimali za taifa.
Balozi Nchimbi alisema Mwanza ni kitovu cha maendeleo ya Kanda ya Ziwa kutokana na mchango wake katika kilimo, madini na ufugaji.
MAFANIKIO YALIYOPATIKANA MIAKA MINNE
Alisema kuna mafanikio makubwa yaliyopatikana katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Dk. Samia, ni ujenzi wa zaidi ya madarasa 4,000, vyuo vipya vya VETA vitatu na vituo vya vyuo vikuu vitatu vimeanzishwa mkoani humo.
Akizungumzia sekta ya maji, alisema asilimia 85 ya wakazi wa Mwanza wanapata maji safi na salama hiyo ni sawa na ongezeko la asilimia asilimia 10, ikilinganishwa na miaka iliyopita ambapo visima na mabwawa mapya yakichimbwa kuongeza upatikanaji.
SEKTA YA AFYA
Mgombea Mwenza wa Urais alisema zimejengwa hospitali mbili mpya, kuwekwa mashine za MRI na digital scan tatu na huduma za afya zikiboreka zaidi.
BARABARA
Balozi Dk. Nchimbi alisema zaidi ya kilometa 300 zimeboreshwa, soko kuu na stendi ya mabasi ya Nyegezi vimekamilika na majosho ya mifugo yameongezwa kutoka 53 hadi 77.
ELIMU
Alisema shule za msingi zimeongezeka kutoka 873 mwaka 2020 hadi 973, sekondari kutoka 219 hadi 308, huku kiwango cha ufaulu kikipanda kutoka asilimia 84 hadi 96.
KUHUSU KUZUIA MAITI
Mgombea Mwenza wa Urias, Balozi Dk. Nchimbi alisema kwa mila za Kiafrika haikubali kuzuia mwili wa marehemu kwenda kuzikwa.
Balozi Dk. Nchimbi alisema siku 100 za kwanza za Mgombea Urais wa Chama, Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, ataliondoa na iwapo kutakuwa na deni utatafutwa utaratibu.
DARAJA LA KIGOGO BUSISI
Alisema Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, alikuta ujenzi wa daraja hilo umefikia asilimia 33 ambapo alihakikisha linakamilika ikiwa ni njia ya kumuenzi mtangulizi wake Hayati Dk. John Magufuli.
NISHATI YA UMEME
Balozi Dk. Nchimbi alisema mitaa na vijiji vyote vya Mwanza vimeunganishwa na umeme, huku maeneo ya visiwa yakiendelea kupata huduma hiyo.
Pia, kukamilisha uboreshaji wa Uwanja wa Ndege wa Mwanza kwa kuwa na sifa kamilifu ya kuwa uwanja kimataifa.
“Jambo hili la kukamikisha uwanja limekuwa likiendelea, nataka niwaambie changamoto ndogo zinazotokana na uboreshaji huo tunazifahamu, tutachukua hatua kuhakikisha kwamba, zinaondolewa,”alisema.
Mgombea Mwenza wa Urais alisema mafanikio hayo ni yanatokana na kuwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, anayejali na anayejitahidi kutafuta , kugawanya na kusimamia rasilimali za taifa.
“Hakuna sehemu yoyote ya nchi iliyobaguliwa kwa sababu yoyote, kila sehemu imepata maendeleo kutegemea na mahitaji yaliyopo kutokana na kuwepo kwa wabunge na madiwani wanaotokana na CCM, viongozi wanaotimiza wajibu wao.
“Kipekee tunawapongeza Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, serikali yake na mabaraza la mawaziri, watendaji wa serikali, wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya, makatibu tarafa , watendaji wa kata wa vijiji, wote hao wamefanya kazi kubwa na viongozi wa CCM katika ngazi zote za usimamizizilishiriki kusimamia kuhakikisha maendeleo ya nchi yetu yanapatikana,”alisema.
Pia, Balozi Dk. Nchimbi aliwashukuru wanaCCM nchi nzima kwa kuhakikisha Chama kinasimamia maendeleo,”alisema.