NA MUSSA YUSUPH
KIBAIGWA imefunika hiyo ndiyo hali halisi ilivyoonekana wakati maelfu ya wananchi wa wilaya hiyo walivyofurika kumshuhudia mgombea Urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Rais Dk. Samia Suluhu Hassan alivyofika kunadi ilani ya uchaguzi ya CCM kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.
Umati huo ulimfanya Dk. Samia kupiga nao picha ‘Selfie’ ambayo imekuwa gumzo katika mitandao mbalimbali ya kijamii ikionyesha namna ambavyo kiongozi huyo alivyo na mapenzi ya dhati kwa wananchi.
Akizungumza na wakazi wa mji huo mdogo, uliopo wilayani Kongwa maarufu kwa biashara ya mahindi na alizeti, Dk. Samia amewaahidi wananchi endapo CCM itapewa tena ridhaa ya kuwaongoza itahakikisha kinamaliza tatizo la uhaba wa maji katika Jimbo la Kongwa.
Pia, Dk. Samia ameahidi kutekeleza huduma mbalimbali za kijamii ikiwemo sekta za afya, elimu, ujenzi wa machinjio, minada ya mifugo, majosho ya mifugo na kuimarisha kilimo.
Wakizungumzia ujio wa mgombea huyo wa Urais kupitia CCM, baadhi ya wakazi wa Kibaigwa walisema Rais Dk. Samia amewaletea miradi mingi ya maendeleo hususan sekta ya maji.
Mkazi wa mji huo, Janeth Maziku alisema tayari mradi mkubwa wa usambazaji maji katika mji huo umeshakamilika ukitoa huduma chini ya usimamizi wa Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA).
“Mradi huu kwa kiasi kikubwa umetupunguzia kero ya uhaba wa maji, sasa kinamama hatutembei umbali mrefu kutafuta maji. Hii ndiyo maana tumekuja kwa wingi kumuunga mkono Rais wetu kwani ametufanyia jambo zuri, tunamuahidi kumpigia kura,” alieleza.
Naye, Songela Mollel ambaye ni mfanyabiashara wa mazao alimpongeza Rais Dk. Samia kwa kuimarisha kilimo nchini hali ambayo imechochea ukuaji wa biashara ya mazao.
“Zamani utakuta baada ya muda serikali inazuia usafirishaji mahindi nje ya nchi kwa sababu uzalishaji wetu haukuwa mkubwa sana kukidhi mahitaji ya ndani na nje, lakini sasa wakulima wanapata fedha zaidi kwa kuwa uzalishaji umeongezeka na masoko yapo yakutosha. Tunamuomba Mama aendelee kutoa ruzuku ya mbolea na pembejeo kwa wakulima ili uzalishaji uwe mkubwa zaidi.
“Leo tunauza mahindi Kenya, Sudan Kusini, Malawi hadi Zambia. Tunapata fedha za kigeni na nchi inaendelea kufaidika kiuchumi. Ikifika Oktoba 29 Watanzania wote kura kwa Mama Samia,” alieleza.