VICTOR MKUMBO Na
AMINA KASHEBA
MGOMBEA Urais kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk. Samia Suluhu Hassan ameahidi kwamba hadi kufikia mwaka 2027 ujenzi wa Uwanja wa soka wa kisasa wa Dodoma utakuwa umekamilika.
Aliyasema hayo jana katika kampeni yake iliyofanyika v iwanja vya Tambukareli jijini Dodoma alipokuwa akizungumza na wananchi.
“Tunakwenda kumaliza uwanja wa soka wa kimataifa, ni matumaini yetu ifikapo mwaka 2027 utakuwa umeshakamilika ili utumike katika michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2027),” alisema Dk. Samia.
Alisitiza tayari mkandarasi alishapatikana ambapo anatarajia kuanza kazi ya ujenzi hivi karibuni.
“Tumejipanga kukamilisha ujenzi wa uwanja mkubwa wa soka wa Dodoma na mkandarasi tayari alishapatikana na ataanza kufanya kazi ya ujenzi hivi karibuni,” alisema.
Dk. Samia alisema Uwanja wa Dodoma ukikamilika utakuwa na uwezo wa kuchukua mashabiki 32,500 ambapo utajengwa na Kampuni ya Limonte Group ya Italia.
Katika kampeni hizo zilipambwa na burudani za wasanii mbalimbali wakiwemo Rajabu Kahali ‘Haromize’, Kontawa, Barobaro, Abdallah Sultan ‘Dullah Makabila’ na kikundi cha ngoma ya asili.
Mbali ya wasanii hao kutoa burudani katika kampeni hizo, nyota wa muziki wa bongo fleva, Harmonize alikuwa mwimbaji wa kwanza kuwanyenyua vitini viongozi baada ya kutoa burudani ya wimbo wake wa ‘Mama Anashindwaje’.
Wakati Harmonize anaimba viongozi wakiongozwa na Dk. Samia walionekana wamesimama na wengine kucheza kwa dakika 10 huku msanii huyo akitoa burudani ya aina yake na kuibua shangwe kwa wananchi waliojitokeza.