Na AMINA KASHEBA
WAKATI Kocha wa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, Hemed Suleiman ‘Morocco’, akitangaza kikosi cha wachezaji 23, wachezaji wa Simba, Kibu Denis, Abdulrazack Hamza na kipa wa Azam FC, Aishi Manula wameachwa.
Pia, katika kikosi hicho wamo wachezaji walioitwa kwa mara ya kwanza ambao ni Antony Remy (Azam FC) na Edmund John (Yanga) huku Abdul Hamis (Azam FC) akirejeshwa kwa mara nyingine.
Akizungumza alipokuwa akitangaza kikosi hicho, Kocha Morocco amesema ameita wachezaji wenye uwezo wa kuisaidia timu kufanya vizuri katika michuano ya kufuzu kucheza Kombe la Dunia mwaka 2026.
Amesema kikosi chake kinatarajia kuingia kambini kesho kujiandaa na michezo miwili ya kuwania kufuzu Kombe la Dunia dhidi ya Congo Brazzavile utakaochezwa Septemba 5, mwaka huu kabla ya kuikabili Niger, Septemba 9, mwaka huu mechi zote Stars itakuwa ugenini.
“Nina imani na wachezaji niliowaita katika kikosi hiki wana kiwango bora na wanaweza kutusaidia kufanya vyema katika michuano ya kufuzu Kombe la Dunia.
“Tunatarajia kuingia kambini kujiandaa na michezo miwili ambayo tutakuwa ugenini dhidi ya Congo Brazzavile na Niger, malengo yetu ni kufanya vyema na kufikia malengo tuliyojiwekea,” alisema Kocha Morocco.
Amewataja wachezaji waliotwa katika kikosi hicho ni Yakoub Suleiman na Wilson Nangu (JKT Tanzania), Shomari Kapombe, Yusuph Kagoma na Selemani Mwalimu (Simba), Mohamed Hussein, Mudathir Yahya, Clement Mzize, Edmund John, Ibrahim Abdullah na Dickson Job (Yanga), Lusajo Mwaikenda, Pascal Msindo, Yahya Zaid, Abdul Hamis, Feisal Salum na Iddy Selemani (Azam FC).
Wengine ni Saimon Msuva (Al-Talaba SC- Iraq), Novatus Dismas (Goztepe FC, Uturuki), Mbwana Samtta (Le Havre AC, Ufaransa), Charles M’mombwa(Florian FC, Malta) na Antony Remmy (Azam FC U-20).
Katika michuano ya kufuzu Kombe la Dunia 2026, Tanzania imepangwa kundi E na timu za Moroco, Zambia, Congo Brazaville, Niger na Eritrea.
Katika msimamo wa kundi hilo, Tanzania ipo nafasi ya tatu ikiwa na pointi sita sawa na Niger iliyopo nafasi ya pili, Morocco inaongoza kundi akiwa na pointi tisa, Zambia pointi tatu nafasi ya nne huku Congo Brazzaville na Eritrea zikiburuza mkia.