Na MUSSA YUSUPH,
Dodoma
MAELFU ya wananchi mkoani Dodoma, wamedhihirisha kuwa, Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimeendelea kukubalika kwa kishindo baada ya kujitokeza kwa wingi katika mikutano ya mgombea urais kupitia CCM, Dk. Samia Suluhu Hassan.
Katika mikutano ya kampeni ndani ya mkoa huo iliyoanzia Kibaigwa wilayani Kongwa, Chamwino, Chemba, Kondoa kisha kishindo kikuu kuhitimishwa ndani ya Jiji la Dodoma ambako jana, mafuriko ya watu yalitawala katika viwanja vya Tambukareli huku viongozi mbalimbali, waliungana na Dk. Samia kuwaomba wananchi kura zote kwa wagombea wa CCM.
Viongozi hao ni Waziri Mkuu Mstaafu na Makamu Mwenyekiti Mstaafu wa CCM, John Samweli Malecela, Makamu Mwenyekiti Mstaafu wa CCM, Philip Mangula na Katibu Mkuu mstaafu wa Chama, Balozi Dk. Bashiru Ali.
Kabla ya kuanza mkutano, wananchi walianza kumiminika uwanjani kuanzia saa tatu asubuhi, wakionesha mahaba ya dhati kwa Chama tawala huku wakiwa na kiu ya kumsikiliza Dk. Samia.
Viwanja hivyo, vilipambwa na bendera za CCM, kuzunguka eneo hilo na kuanzia saa nane
mchana, helkopta ilizunguka maeneo mbalimbali ya jiji hilo na eneo la uwanja likipeperusha ujumbe maalumu uliosomeka ‘Chagua Samia, Oktoba Tunatiki.’
WENYE MASWALI WAMEANZA KUYAFUTA
Akihutubia wananchi katika mkutano huo, Dk. Samia, alisema wananchi wa Dodoma, wamethibitisha mkoa huo ndiyo makao makuu ya Chama Cha Mapinduzi. “Dodoma tangu nilipoingia jana (juzi) pale Kibaigwa, leo (jana) nimetoka Chemba, Kondoa na hapa Dodoma Manispaa, Dodoma mmefunika.
“Dodoma CCM ina wenyewe na wenyewe ndiyo nyinyi. Hapa wale wenye maswali nadhani kidogokidogo wanaanza kufuta, wale wenye kujiuliza nadhani wanaanza kufuta.
“Kwa umma huu, CCM oyeee….niwashukuru sana ndugu zangu wa Dodoma kwa mapokezi haya, kwa kweli mmethibitisha kwamba, hapa ndiyo makao makuu ya Chama Cha Mapinduzi, mmethibitisha na mmembeba mgombea wenu, mkazi wa Chamwino hapa Dodoma, nawashukuru sana ndugu zangu,” alieleza Dk. Samia.
Alitoa wito kwa wananchi kuendelea kuchapakazi huku akieleza mafanikio mbalimbali yaliyopatikana katika kipindi cha uongozi wake.
“Awamu ya tano, tulifanya maamuzi ya kuhamia Dodoma, awamu ya sita, tumekwenda kuendeleza kuhamia Dodoma, taasisi zote za serikali zipo Dodoma, maamuzi yote makubwa sasa yanafanyika hapa.
Aliongeza: “Tumemimina shilingi trilioni 9.5 kwa miradi 3,093 ndani ya Mkoa wa Dodoma, mbali na kuongeza majengo na kuipa hadhi Hospitali ya Benjamin Mkapa, wilaya za Dodoma, zina hospitali za kisasa ambazo vipimo vyote vinapatikana huko,”.
Pia, Dk. Samia, alisema serikali yake, imejitahidi kufungua fursa za ajira kupitia uwekezaji kwa kujenga viwanda, kutengeneza fursa kwa wafanyabiashara wadogo huku mradi wa reli ya kisasa (SGR) ukiongeza kasi ya ukuaji uchumi.
KUHUSU UMEME
Alisema serikali inaendelea na kazi ya kumalizia vitongoji, kila mtu apate nishati hiyo kufanyakazi na kulinda usalama wao.
Aidha, alisema Chama kimejipanga kutatua uhaba wa maji kwa kutekeleza mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria na kumalizia ujenzi Bwawa la Farkwa kusaidia kuleta maji Dodoma.
“Umeme wakati mwingine ni mdogo, tumejipanga kujenga njia kusafi risha umeme kutoka Chalinze hadi Dodoma ili tupate umeme mkubwa wa kilovoti 400.,” alieleza.
Alitoa ahadi ya kuongeza kasi ya upimaji na usajili ardhi kutatua migogoro, kukamilisha ujenzi wa kiwanja kikubwa cha mpira wa miguu, tayari mkandarasi ameshapatikana.
WAKONGWE WAFUNGUKA
Akizungumza na wananchi, Malecela alisema Mkoa wa Dodoma, umekuwa na historia tangu kuanzishwa mfumo wa vyama vingi, kuongoza kwa idadi ya kura nyingi kwa wagombea urais kupitia CCM.
“Napenda kuchukua nafasi kumshukuru Dk. Samia Suluhu Hassan, ambaye amechaguliwa kugombea urais kupitia CCM. “Niwaeleze huko nyuma, ukienda kuangalia katika rekodi tangu Tanzania tuanze kuwa huru, kuchagua viongozi wetu wa nchi ambaye ni Rais, kuna mikoa miwili ambayo imekuwa na rekodi nzuri tangu tuanze uchaguzi.
“Mikoa hiyo ni Iringa na Dodoma, sasa mimi nina jambo moja la kuwaomba Wana Dodoma wenzangu, rekodi za huko nyuma, zinaonesha kwamba, kila mara tumekuwa tukiwapa marais wetu wagombea kura nyingi kuliko mikoa mingine, sasa niwaombe safari hii ndugu zangu wote Mkoa wa Dodoma, nina uhakika wananchi wote tutampa kura zetu Dk. Samia,” alisisitiza.
Kwa upande wake, Makamu wa Rais Dk. Philip Mpango, alifunguka namna ambavyo baadhi ya wananchi katika mataifa mbalimbali duniani wanavyotamani kuwa na kiongozi aina ya Dk. Samia.
“Kule unaponituma wenzetu wanatamani huyu awe Rais wao, nawasihi sana, Oktoba 29 mwaka huu, mkampigie kura Mama Samia mitano tena,” alieleza huku wananchi wakiitikia mitano tena.
MZEE MANGULA
Makamu Mwenyekiti Mstaafu wa CCM Bara, Mangula alisema Watanzania anapaswa kumpigia kura Dk. Samia, akamalize mazuri ambayo ameendelea kuyafanya kwa maslahi ya Watanzania.
“Ukiwa unaingia kwenye gari, unatakiwa kuangalia anayekuendesha, kwani wengine wanaweza kuwa ‘malena’ lakini ni tofauti kwa Dk. Samia, kwani ana leseni ya kimataifa ambayo inamfanya awe na uzoefu katika kuendesha.
DK. BASHIRU ALI
Katibu Mkuu Mstaafu wa CCM, Dk. Bashiru Ali, alisema nguvu ya CCM, inatokana na umoja ndani ya Chama huku akimpongeza Dk. Samia kuliunganisha taifa.
“Nakushukuru mwenyekiti kwa kuchukua kazi hii na umeisimamia kuunganisha vizuri nchi yetu, inaendelea kufanya vizuri katika maeneo mengi, tupo kuwanadi wagombea kutokana wa ilani na utendaji wetu bora.
“Tunaomba sana, mwendelee kukiamini Chama Cha Mapinduzi na Dk. Samia,” alisema.
MWENYEKITI CCM, DODOMA
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dodoma, Adam Kimbisa, alisema wamekuja na bidhaa adimu ambayo ni Dk. Samia Suluhu Hassan, hivyo amewaomba wananchi kumpigia kura ifi kapo Oktoba mwaka huu.