NA MUSSA YUSUPH,
Songwe
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimetaja sababu kuu mbili zilizofanya kiombe kura za ndiyo kwa wananchi mkoani Songwe kuelekea Uchaguzi Mkuu mwaka huu.
Sababu hizo, CCM imepeleka maendeleo katika maeneo mengi nchini na pili ina uwezo wa kuendelea kuifanya kazi hiyo.
Hayo yalielezwa mkoani humo na mgombea urais kupitia CCM, Dk. Samia Suluhu Hassan katika mkutano wa kampeni uliofanyika mjini Vwawa.
“Tuna nguvu zote za kifedha, ari ya kufanya kazi na dhamira ya dhati ya kuwatumikia wananchi. Ndiyo maana kwa kujiamini tunakuja kwenu kuomba kura. Tupeni kura tuendeshe nchi hii kwa miaka mitano ijayo na ikifika wakati mwingine tutakuja tena kuwaomba. Tuwapeni kura tuendelee kuwaonesha uwezo wetu wa kuwatumikia, kama tulivyofanya huko nyuma,” amesema.
Dk. Samia alisema maboresho yaliyofanyika katika Bandari ya Dar es Salaam yamechochea ongezeko la mizigo inayosafirishwa kwenda nchini Zambia.
“Natambua maboresho makubwa yaliyofanyika Bandari ya Dar es Salaam yameongeza mizigo inayotoka nchini kwenda nje ya nchi. Kabla ya maboresho tani za mizigo iliyokuwa ikiingia bandarini ilikuwa milioni 15.8, baada ya maboresho bandari inapokea tani milioni 28 za mizigo,” amesema.
Ameongeza: “Mzigo unaovuka mpaka wa Tunduma umepanda kutoka tani milioni 3.7 hadi tani milioni tisa. Hali hiyo inaleta msongamano wa malori ya mizigo yanayoelekea kuvuka mpaka wa Tunduma, kwa maana hiyo tumeanza ukarabati kwa kupanua barabara kuu inayounganisha Tanzania na Zambia. Kazi inaendelea na tutaendelea nayo hadi itakapokamilika.”
Ameeleza ukarabati huo umeanza kwa njia nne kutoka Igawa hadi Tunduma kwa urefu wa kilometa 75 huku mazungumzo ya kukarabati na kuimarisha Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA) yakiendelea.
Amesema reli hiyo ya miaka mingi imechoka na kusababisha kubeba kiwango kidogo cha mizigo wakati huu ambao mizigo imeongezeka Bandari ya Dar es Salaam.
“Tutakamilisha ujenzi wa Bandari kavu eneo la ekari 1,800 eneo la Katenjele, Kata ya Mpemba malori yasipaki barabarani, tutaongeza barabara ya mbadala itakayoanzia Mwakabanga, tutajenga maegesho ya kisasa, kuongeza mizani, kuharakisha uchakataji nyaraka kabla ya magari kufika mpakani. Pia, serikali tumeanza kuzungumza na mamlaka za ukusanyaji mapato Zambia zifanye kazi saa 24 kama ilivyo Tanzania,” amebainisha.
Dk. Samia alisema serikali imejipanga kutekeleza mradi wa umeme kutoka Iringa-Njombe hadi Tunduma wenye msongo wa kilovoti 730 ambazo kati ya hizo, kilovoti 400 zitatumika Tunduma na Rukwa huku 330 zitauzwa nchini Zambia.
“Tumeshakamilisha mazungumzo, tumeanza mchakato kujenga njia hii umeme ufike kwa uhakika. Hii inakwenda pamoja na uhamasishaji matumizi ya nishati safi kwa sababu umeme na gesi ni nishati safi,” amesema.
“Nataka kuwathibitishia na kuwaahidi, nitaendelea kufanya makubwa katika sekta ya elimu, afya, maji na umeme. Tunakwenda kutoa huduma kwa wananchi, tutaendelea kuongeza shule, elimu bila ada, mikopo kwa wanafunzi wa vyuo vikuu na VETA, kujenga vyuo vya VETA kuwawezesha vijana wapate ujuzi na kujiajiri.
Mgombea huyo urais kwa tiketi ya CCM aliahidi akishinda, ataendelea kujenga vituo vya afya na zahanati na kukamilisha miradi ya maji lengo kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma hiyo kwa asilimia 85 vijijini na asilimia 95 mijini.
Kuhusu umeme, alieleza vijiji vyote vimefikiwa na nishati hiyo huku nusu ya vitongoji vikifikiwa na umeme lengo kuhakikisha kila mwananchi anafaidika.