Na MUSSA YUSUPH,
Mbeya
MGOMBEA urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Samia Suluhu Hassan, ametangaza neema kwa wakulima nchini.
Amewataka kujisajili kwa wingi katika mfumo wa ruzuku za mbegu na pembejeo za kilimo, kwani serikali bado ina uwezo wa kutoa ruzuku hiyo kwa wakulima wengi nchini.
Amesema lengo na dhamira yake ni kila Mtanzania aguswe na maendeleo yanayopatikana sekta zote.
Pia, amesisitiza wakulima kutoshirikiana na wahalifu wanaouza pembejeo hizo, kwani mpango wa serikali ni kuongeza wigo wa uzalishaji mazao nchini, hatimaye kuimarisha vipato vyao.
Akihutubia maelfu ya wananchi waliohudhuria mkutano wa kampeni katika Uwanja wa Mlima wa Reli uliopo Mji mdogo wa Mbalizi mkoani Mbeya, Dk. Samia, amesema ruzuku hiyo inatolewa kwa wakulima wote nchini.
“Hadi sasa, mbolea na mbegu za ruzuku, zinagawiwa kwa wakulima nchi nzima. Kuna kila aina ya mbolea za kupandia na kukuzia,” alieleza.
Ameyataja baadhi ya mazao ambayo mbolea na mbegu za ruzuku zinatolewa ni mahindi, mpunga, tumbaku na parachichi.
“Lengo tuzalishe, tujilishe kisha kuuza nje ya nchi. Wakulima endeleeni kujisajili, kwani serikali bado ina uwezo wa kutoa ruzuku.
“Tunzeni namba zenu za siri na msishirikiane na waovu kuuza pembejeo za ruzuku,” amesisitiza Dk. Samia.
Kuhusu wafugaji, alisema serikali itakamilisha ujenzi wa machinjio ya mifugo ya kisasa, Utengule.
Amesema serikali inaendelea na kampeni ya chanjo na utambuzi wa mifugo, yenye lengo la kuongeza hadhi ya mifugo kutoka Tanzania katika masoko ya kimataifa.
Awali, kabla ya kampeni hiyo, mifugo ya Tanzania, ilikuwa haina soko la uhakika kwa sababu ya kukosa rekodi za chanjo.
Akiwa njiani kwenda Mbalizi, Dk. Samia aliwasalimia wananchi wa eneo la Mlowo na kuwaomba kukipigia kura Chama Cha Mapinduzi.
KAULI YA CHONGOLO
Katibu Mkuu Mstaafu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo, amesema ushindi wa Dk. Samia katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29, mwaka huu, upo wazi kutokana na utekelezaji mzuri wa miradi ya maendeleo.
Chongolo ambaye pia ni Mratibu wa Kampeni za CCM Nyanda za Juu Kusini, amesema maendeleo makubwa yanayopatikana katika mkoa huo, ni ushahidi wa uongozi mzuri wa Rais Dk. Samia.
Amesema wananchi wa mkoa huo, kwa muda mrefu, walilalamikia kuhusu upanuzi wa barabara kuu kuanzia Igawa – Tunduma kwa njia nne kupunguza msongamano.
Amebainisha kuwa, tayari mkandarasi anaendelea na ujenzi wa barabara hiyo, itakayorahisisha shughuli za kiuchumi.
KIHONGOSI ASHAURI VIJANA
Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Kenani Kihongosi, amewasihi vijana kuwa mstari wa mbele kulinda amani ya nchi.
Amesema kundi hilo muhimu, kamwe lisikubali kuingia katika mtego wa kikundi cha watu wenye dhamira ya kuleta vurugu nchini.
“Vijana wa Tanzania wakiwemo wa Mbalizi, wana wajibu wa kulinda taifa, kwani linawategemea,” amesisitiza.
MGOMBEA UBUNGE MBALIZI
Naye, mgombea Ubunge wa Jimbo la Mbalizi, Patari Shida Patari, alisema mafanikio yaliyopatikana ni matokeo ya uongozi thabiti wa serikali, mshikamano baina ya viongozi na wananchi.
Alieleza kuwa, sekta ya afya, imepata mafanikio makubwa baada ya kupatiwa sh. bilioni sita kutekeleza miradi mbalimbali ya afya.
“Tangu kuanzishwa kwa jimbo mwaka 1980, hakuna hospitali iliyojengwa, sasa jimbo lina hospitali inayofanya kazi kikamilifu,” ameeleza.
Katika sekta ya maji, alisema sh. bilioni 4.8 zimewekezwa katika mradi wa Ilulu utakaoleta maji safi na salama katika eneo la Mbalizi.
ELIMU
Kuhusu elimu, amesema sh. bilioni 9.3, zimetumika kujenga shule na nyumba za walimu huku sh. bilioni 13.9, zikitumika kujenga madarasa 29 na maabara 14.