Na NJUMAI NGOTA,
Kahama
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimesema Ilani ya Uchaguzi ya Chama ya mwaka 2025-2030, imeweka umuhimu katika kuendeleza misingi ya amani na usalama, kwa kuwa, bila utulivu hakuna maendeleo yatakayofanyika.
Pia, kimesema Mgombea Urais wa CCM, Dk. Samia Suluhu Hassan, ametekeleza kwa mafanikio makubwa, dhamira ya kulinda uhuru, usalama na mipaka ya nchi, tangu alipoingia madarakani, jambo lililoifanya Tanzania kuwa mfano wa kuigwa Afrika.
Hayo yamebainishwa wilayani Kahama, mkoani Shinyanga na Mgombea Mwenza wa Urais wa CCM, Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi, aliposimamia kuwasalimia wananchi wa Isaka, huku akiwaomba Oktoba 29, mwaka huu, wampigie kura Dk. Samia, wabunge na madiwani wa CCM.
Amesema kwamba, Dk. Samia, amefanya kazi kubwa kuhakikisha nchi inakuwa na amani na usalama.
“Bila utulivu, hakuna mtu anaweza kupanga mipango ya maendeleo. Ukiwa na amani, kila kitu kinawezekana,” amesema.
Dk. Nchimbi, ameeleza kuwa, amani ni urithi wa taifa, ambao haulinganishwi na rasilimali yoyote na kwa msingi huo, CCM itaendelea kuilinda kwa nguvu zote kwa kuimarisha usalama wa mipaka, mshikamano wa kitaifa na maelewano ya kijamii.
“Tunataka Watanzania wajue kwamba, CCM inathamini amani kuliko kitu chochote, kwa sababu bila amani hakuna elimu, hakuna afya, hakuna maendeleo ya viwanda wala barabara. Haya yote yanawezekana tukidumisha utulivu,” amesema.
Baada ya maneno hayo, baadhi ya wananchi waliuliza maswali kadhaa, aliwapa, wakaeleza changamoto zinazowakabili, hasa barabara na miundombinu, akaahidi zitapatiwa ufumbuzi.
Akiwa Kagongwa, wilayani humo, Dk. Nchimbi, amesema kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Dk. Samia, serikali imetekeleza miradi ya maendeleo iliyogusa sekta muhimu kwa wananchi wa Kata ya Kagongwa na maeneo jirani.
Dk. Nchimbi, amesema kuna mafanikio yaliyopatikana kipindi hicho, akaahidi wataendelea kutatua changamoto zinazowakabili.
ILANI YA 2020-2025
Amesema miongoni mwa mafanikio makubwa katika sekta ya afya ni kuboreshwa Kituo cha Afya cha Kagongwa, hivi sasa kinatoa huduma bora kwa wananchi.
SEKTA YA ELIMU
Amesema ujenzi na ukarabati wa madarasa katika shule za msingi na sekondari, umetekelezwa.
Amesema katika miaka mitano iliyopita, hatua ya ujenzi wa madarasa, umepunguza msongamano wa wanafunzi darasani na kuongeza kiwango cha ufaulu.
Amebainisha idadi ya wananchi wanaopata maji hivi sasa imeongezeka kutoka watu 81 kati ya 100, hadi 86.
UJENZI WA RELI YA SGR
Kuhusu Ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR), Dk. Nchimbi amesema umekamilika kwa asilimia 63, sehemu iliyobaki itakamilika mwakani.
Balozi Dk. Nchimbi, amesema katika kuwainua wananchi kiuchumi, serikali imetoa mikopo kwa zaidi ya vikundi 607 vya vijana na kinamama, huku zaidi ya sh. bilioni 5.4, zikitolewa kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), kuwawezesha vijana.
Pia, amesema wanatambua kuna changamoto, vijana wengi wanahitaji mikopo, serikali itaendelea kulifanyia kazi suala hilo.