Na NJUMAI NGOTA,
Kahama
MBUNGE mteule kupitia Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), Jesca Magufuli, ametaka wananchi wa Wilaya ya Kahama, mkoani Shinyanga, kuendelea kukiamini na kukipa ushindi wa kishindo Chama katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29, mwaka huu.
Jesca, mtoto wa Rais wa Awamu ya Tano, Hayati Dk. John Magufuli, amesema hayo, katika Kata ya Kagongwa, wilayani Kahama, aliposimamishwa kutoa salamu kwa wakazi wa eneo hilo na mgombea mwenza wa urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi.
“Wananchi wa Shinyanga, tunaposema tuendelee kukiamini Chama chetu, tunamaanisha. Chama Cha Mapinduzi, ni Chama ambacho kimetekeleza Ilani ya mwaka 2020-2025 kwa vitendo.
“Wanashinyanga ni mashahidi mmeona miradi mikubwa ya miundombinu, barabara, reli ya kisasa ya kiwango cha kimataifa (SGR), maji na nishati, kubwa zaidi katika sekta ya madini imeendelea kuwanufaisha vijana wa Shinyanga,”amesema.
Jesca amesema mafanikio hayo ni matokeo ya uongozi thabiti wa CCM chini ya Mgombea Urais wa CCM, Dk. Samia Suluhu Hassan katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wake.
“Tuendelee kukiamini Chama, katika Ilani ya mwaka 2025-2030 kimeahidi mambo mengi kwa vijana ikiwemo kuongeza ajira, suala la mikopo ambayo itaendelea kutolewa,”amesema.
Pia, Jesca amesema serikali imeendelea kutoa elimu kwa wajasiriamali, kutafuta masoko ya nje na ndani kwa kuwapatia mitaji
“Itakapofi ka Oktoba 29, mwaka huu tuendelee kukiamini Chama chetu, kura nyingi kwa madiwani , wabunge na kura nyingi zaidi kwa mgombea wetu, Rais Dk. Samia Suluhu Hassan,”amesema.
Naye, Mgombea Ubunge wa Jimbo la Msalala, Mabula Magangila, amesema CCM imefanya kazi kubwa katika utekelezaji wa Ilani ya Chama.
Mabula amesema madarasa, vituo vya afya, barabara ya lami kutoka Kahama kwenda Kakola, hivyo wanatarajia makubwa zaidi katika sekta ya uzalishaji.