Na AMINA KASHEBA
UONGOZI wa klabu ya Yanga umeridhishwa na matokeo ya uzaji wa jezi zao kuelekea msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara, utakaoanza hivi karibuni.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Ofisa Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo, Ali Kamwe alipotembelea duka la Goba Sports Wear amesema mapokezi yamekuwa makubwa kwa wanachama kununua jezi tangu zilipozinduliwa.
Amesema kwa mwaka huu jezi hizo zimenunuliwa kwa kiwango kikubwa tofauti na miaka ya nyuma.
“Tunaweza kusema tumefanikiwa kwa kiwango kikubwa katika uzaji wa jezi msimu huu, mwitikio umekuwa wa kipekee wala hatukutegemea.
“Katika siku za nyuma hali haijawahi kuwa hivi kabisa, lakini tumevunja rekodi ambayo inatupa nguvu ya kuongeza ubora katika jezi zetu,” alisema Kamwe.
Kamwe alisema hivi sasa kuna maduka mengi ya uuzaji jezi hivyo ameamua kufanya ziara ili kutambua changamoto wanazopata wauzaji hao.
“Nimekuja Goba Sports Wear kuangalia namna uuzaji wa jezi unavyokwenda na kutambua changamoto zinazowakuta wenye maduka,” amesema.
Kamwe amewataka wanachama wa Yanga kununua tiketi mapema kwa ajili ya kwenda kupata burudani katika Wiki ya Wananchi.