Na MWANDISHI WETU
KOCHA wa timu ya taifa ‘Taifa Stars’, Hemed Suleiman ‘Morocco’, amesema anaamini kikosi chake kitapata ushindi dhidi ya Niger keshokutwa.
Taifa Stars itachuana na Niger saa 10:00 jioni katika mchezo wa kundi E kuwania kufuzu Kombe la Dunia, utakaopigwa katika Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.
Katika mtanange huo, Taifa Stars itaingia ikiwa nafasi ya pili kwa alama 10 baada ya kushuka dimbani mara sita sawa na kinara Morocco ambayo tayari imeshakata tiketi baada ya kuvuna pointi 18.
Akizungumza kutoka Brazaville nchini Congo ambapo kikosi chake kilitoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Congo Brazavile, Kocha Morocco alisema wapinzani wake walikuwa bora.
“Congo walitupa presha kubwa na pia hatukuwa katika kiwango kizuri. Tutajitahidi kurekebisha makosa,” alisema.
Tunahitajika kuongeza nguvu, tutakuwa na siku kadhaa za kujiandaa naamini mechi ya nyumbani tutakuwa vizuri zaidi,” alisema.
Ili Taifa Stars iendelee kusalia nafasi ya pili, inapaswa kupata matokeo mazuri katika mechi zilizobaki ikiwemo dhidi ya Niger keshokutwa.