Na NJUMAI NGOTA,
Katavi
MGOMBEA Mwenza wa Urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi, amesema katika kipindi cha miaka mitano ijayo, iwapo watapewa ridhaa ya kuongoza nchi, wataanzisha kongani za viwanda vya ndani katika kila wilaya.
Aliyasema hayo, Kata ya Katumba, iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo, mkoani Katavi, aliposimama kuwasalimia wananchi wa eneo hilo, akiwa njiani kwenda Halmashauri ya Wilaya Mlele, Jimbo la Kavuu.
Katika mkutano huo wa hadhara, Dk. Nchimbi, aliwaomba wananchi kumchagua Mgombea Urais wa CCM, Dk. Samia Suluhu Hassan, katika Uchaguzi Mkuu, utakaofanyika Oktoba 29, mwaka huu.
Pia, alieleza utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2020-2025 na kuinadi mpya ya mwaka 2025-2030 kwa wananchi.
Alisema mpango huo ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya CCM na kila wilaya, itatambuliwa kwa uzalishaji mahsusi, kuanzisha viwanda vinavyolingana na rasilimali zilizopo katika maeneo husika.
“Kwa kutambua umuhimu wa viwanda katika Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), tumekubaliana kwamba, miaka mitano inayokuja, tutakuwa na kongani ya viwanda vya ndani kwa maana ya kwamba, kila wilaya katika nchi yetu, tutaitazama inazalisha nini kwa wingi, kitu gani kinapotea bure na kitu gani kinakosa soko.
“Tukishajua, kila maeneo katika nchi yetu, tutapanga viwanda kutegemea na maeneo yaliyopo,” alisema.
Balozi Dk. Nchimbi, alitolea mfano mazao kutoka Mpanda na Katavi, yatasindikwa na bidhaa hizo kufikishwa maeneo mengine, ikiwemo Wilaya ya Nsimbo.
Alisema hiyo itasaidia kuhakikisha bidhaa za Watanzania hazikosi soko.
Mbali na viwanda, Balozi Dk. Nchimbi, alisema dhamira ya Serikali ya CCM ni kuendeleza sekta za afya, elimu, kilimo, maji na miundombinu.
AFYA
Balozi Dk. Nchimbi, alisema katika Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo, wanakusudia kujenga vituo vipya vya afya vitatu na zahanati tatu, kuimarisha utoaji wa huduma hizo karibu zaidi na wananchi.
ELIMU
Kuhusu elimu, alisema katika miaka mitano ijayo, wamedhamiria kujenga shule za sekondari 11, kuimarisha miundombinu ya madarasa kwa kuhakikisha watoto wanasoma katika mazingira bora zaidi.
Alisema katika bajeti ya elimu, itaendelea kuongezwa kuhakikisha kila Mtanzania mwenye nia ya kusoma, anapata fursa hiyo bila vikwazo.
KILIMO
Kwa mujibu wa Balozi Dk. Nchimbi, serikali ijayo, inatarajia kuongeza maradufu bajeti ya ruzuku ya mbolea na mbegu, kwa kutambua Watanzania wengi hutegemea kilimo.
UFUGAJI
Akizungumzia ufugaji, alisema sekta hiyo, itaendelea kuimarishwa kwa kuongeza chanjo za mifugo, majosho, mabwawa na minada ya kuuza mifugo.
UVUVI
Alisema katika kipindi cha miaka mitano ijayo, serikali ya CCM itawekeza katika uvuvi wa kisasa kwa kutumia vizimba, mabwawa, kuimarisha upatikanaji wa vifaa na masoko kwa wavuvi wadogo.
MADINI
Kuhusu sekta ya madini, Dk. Nchimbi, alisema serikali imeongeza zaidi ya asilimia 50 ya bajeti ya utafiti wa madini huku ikielekeza nguvu katika kuwapa leseni wachimbaji wadogo hususan vijana kuwawezesha kiuchumi.
MAJI
Akielezea upatikanaji wa maji, alisema wamejipanga kuanzisha miradi ya maji 16 ikijumuisha visima virefu na mabwawa, lengo likiwa ni kuondoa na upungufu wa maji katika maeneo yenye changamoto.
BARABARA
Dk. Nchimbi, alisema katika miaka hiyo ijayo, wanatarajia kuimarisha miundombinu ya barabara kwa kuhakikisha inafanya kazi na zinapitika masika na kiangazi.
Alitumia fursa ya mkutano huo, kuwaomba wananchi kumchagua Mgombea Urais wa CCM, Dk. Samia, wabunge na madiwani kwa kura za kishindo.
Akiwa katika mkutano wa hadhara wa kampeni za Chama uliofanyika Kijiji cha Inyonga, Halmashauri ya Wilaya Mlele, mkoani Katavi, Dk. Nchimbi, alisema wanatarajia kujenga kongani ya viwanda wilayani na mikoani