Na CHRISTOPHER LISSA
RAIS mstaafu Dk. Jakaya Kikwete, amewataka Watanzania Oktoba 29, mwaka huu kumpigia kura za kishindo Mgombea Urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Samia Suluhu Hassan, kwa sababu ana uwezo mkubwa wa kuliongoza taifa.
Dk. Kikwete aliyasema hayo alipozidua kampeni za Mgombea Ubunge wa Jimbo la Kivule kwa tiketi ya CCM, Ojambi Masaburi, wilayani Ilala, mkoani Dar es Salaam.
“Mimi nilikuwa rais wa nchi yetu, sikufanya mambo mengi kama anayoyafanya Rais Dk. Samia. Amejenga uwezo mkubwa wa kupata fedha kwa kuimarisha mamlaka ya mapato na kujenga uhusiano mzuri na mataifa ya nje,”alisema Dk. Kikwete.
Pia, alisema Dk. Samia, ameimarisha uhusiano na mashirika ya maendeleo duniani ndiyo maana amepata misaada mikubwa inayosaidia kufanya mambo makubwa ya maendeleo.
“Hii ni sifa nyingine ya rais, amemekuwa hodari wa kujenga uhusiano wa kimataifa. Uhusiano huu umekuwa na manufaa tunayoyaona,”alinainisha.
Pia, alieleza Dk. Samia, anapenda nchi yake na anahuruma na raia wake.
“Katika mambo ambayo ameyatilia mkazo ni yanayo gusa maisha ya watu. Afya, elimu, maji, barabara bima ya afya na umeme,”alieleza Dk. Kikwete.
Alisema hivi karibuni mgombea huyo wa urais, alitangaza kupiga marufuku kuzuia maiti hospitalini kitu ambacho kilikuwa kilio cha watanzania cha muda mrefu.
“Ni mapenzi kiasi gani aliyo nayo. Hana deni. Hatuna deni naye. Yeye ndiyo anatudai sisi na tumlipe kwa kura nyingi Oktoba 29,”alieleza.
Pia, Dk. Kikwete alisema, Dk.Samia, anapenda amani, umoja, utulivu na mshikamano katika taifa lake.
“Alitambua kuna mfarakano katika uwanja wa siasa. Aliamua kukutana na viongozi wa vyama vya upinzani, wakazungumza wakakubaliana namna ya kwenda pamoja. Ana upendo wa dhati,”alisema.
Aidha, alisema Dk. Samia, ameongeza uhuru wa kutoa maoni ikiwa ni pamoja na kufungulia baadhi ya vyombo vya habari vilivyokuwa vimefungwa.
“Rais Dk. Samia, alipokea miradi mikubwa ya gharama kubwa. Angeweza kusema miradi siyo yangu naanza yangu lakini aliikamilisha,”alisema Dk. Kikwete.
Alisema Dk. Samia ni hodari na ana maarifa ya kutafuta fedha zinazosaidia taifa kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo.
“Kubwa zaidi Dk. Samia, ameandaa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2050 inayotoa mwongozo wa kulitoa taifa kutoka uchumi wa kati daraja la chini hadi uchumi wa kati daraja la juu,”alisema.
Aliwataka wananchi kumchagua Dk. Samia na Mgombea Ubunge wa Jimbo la Kivule, Ojambi Masaburi na wagombea udiuwani wote wa CCM.
“Mafanikio yaliyopo Kivule yamewezeshwa kwa kiwango kikubwa kwa zaidi ya asilimia 77 na serikali inayoongozwa na Rais Dk. Samia,”alisema.
Alisema Wilaya ya Ilala ilipewa fedha za maendeleo kiasi cha sh. bilioni 253 zilizotolewa na serikali.
“Mchague Samia, tumchague Ojambi na madiwani wale sita wa Kata za Kitunda, Kivule, Mzinga, Majohe, Msongola na Kipunguni,” alieleza.
Alisema Ojambi anafaa kuwa mbunge kwani amekuwa diwani kwa miaka 10, Naibu Meya wa Jiji la Dar es Salaam, kwa miaka nane, hivyo anajua mambo mengi kuhusu Jimbo la Kivule.
“Akichaguliwa tu kuwa mbunge siku hiyo hiyo anaanza kazi kwa sababu anajua kila kitu ndani ya jimbo hili,”alisema.