Na REHEMA MAIGALA
CHAMA cha National League for Democracy (NLD), kimesema iwapo kitapata ridhaa ya kuongoza nchi, kitahakikisha kinaunda serikali ya umoja wa kitaifa, kwa lengo la kujenga mshikamano.
Mgombea urais kupitia chama hicho, Hassan Doyo, alisema hayo, alipokuwa akihojiwa katika kipindi cha Kiongozi 2025 kinachorushwa na Kituo cha Utangazaji cha TBC.
“Chama chetu kikipata ridhaa ya kuongoza nchi, kitahakikisha kinaunda serikali ya umoja wa kimataifa, kwa lengo la kujenga mshikamano wa kweli,” aliahidi.
Aidha, Doyo alisema kwa kuwa Tanzania haina uhasama na nchi yoyote duniani, chama chao kitaendeleza mazuri yaliyofanywa na serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Pia, alisema serikali ya chama chao kitaimarisha uhusiano mzuri wa ndani ya nchi, ndiyo maana kila wakati kinawahimiza Watanzania kudumisha amani, mshikamano na umoja.
Mbali na hayo, Doyo alisema takwimu zinaonesha zaidi ya asilimia 70 ya Watanzania ni wakulima, lakini bajeti ya kilimo ni asilimia 10, hivyo wakipata ridhaa watahakikisha wakulima wanapewa mbegu bora bure, kutafutiwa masoko na kuboreshwa miundombinu ya barabara kuwawezesha kusafirisha mazao yao moja kwa moja sokoni.
Akizungumzia sekta ya elimu, Doyo aliahidi chama chao kitajenga vituo vya elimu ya teknolojia kila halmashauri.
“Vituo hivyo vitakuwa vya kipekee barani Afrika na vitakusanya vijana kutoka maeneo yote ya halmashauri husika, kuwawezesha kujifunza, kufanya utafiti na kutoa ushauri wa kitaalamu kwa serikali,” alisema.
Aliongeza kupitia vituo hivyo vijana hawatakuwa wasikilizaji tu, bali watashiriki mabadiliko ya teknolojia.
Doyo alisema NLD imejipanga kuboresha huduma bora za kijamii, zikiwemo afya, ajira, elimu na miundombinu ya barabara.
Kuhusu dhamira yake ya kugombea urais, Doyo alisema anataka kulitumikia taifa kwa misingi ya uzalendo, haki na maendeleo.
“Nikipata nafasi ya kuwa rais, serikali yangu itaongozwa na misingi mitatu ambayo ni Uzalendo, Haki na Maendeleo.
“Nitahakikisha nchi hii inakuwa na maendeleo, huku nikiwahimiza Watanzania kupendana na kuwa na umoja wa kizalendo ulioasisiwa na waasisi wa nchi hii,” aliahidi.