Na MUSSA YUSUPH,
Tabora
MGOMBEA Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Samia Suluhu Hassan, amesema CCM imedhamiria kujenga uchumi jumuishi, unaozingatia ustawi wa wananchi katika maeneo ya mijini na vijijini, endapo kikipata ridhaa kwa kuchaguliwa na Watanzania.
Amesisitiza huo ndiyo msingi mkuu wa kauli mbiu ya ‘Kazi na Utu’ yenye dhamira ya kuifanya Tanzania kuwa, taifa lenye kujitegemea na kuneemesha watu wake.
Pia, Dk. Samia ameahidi neema ya ujenzi wa madaraja 133 na taa za barabarani 2,500 katika barabara za kimkakati ndani ya mkoa huo kinara kwa kilimo cha tumbaku.
Vilevile, amesisitiza serikali yake, itaendelea kuimarisha huduma za afya, elimu, nishati, maji na miundombinu.
Akizungumza na maelfu ya wananchi katika mkutano wa kampeni uliofanyika Uwanja wa Nanenane Ipuli mkoani hapa, Dk. Samia amesema Tabora ina nafasi ya kipekee katika historia ya kisiasa nchini.
Amesema mmoja wa waasisi na Mwenyekiti wa kwanza wa CCM, Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere alisoma katika mkoa huo.
“Na hata alipohitimu masomo kule Makerere (Uganda) alirudi kufundisha katika shule ya sekondari St. Marrys hapa Tabora (Tabora Boys). Vilevile kuna maamuzi muhimu ya kihistoria yaliyofanyika Tabora.
“Mwaka 1958 maamuzi yaliyofanywa na mkutano mkuu wa TANU kushiriki uchaguzi, maamuzi ambayo yalisogeza nchi yetu karibu na uhuru wake,”alisema.
Dk. Samia alisema hayo yanathibitisha namna ambavyo CCM ina historia kubwa mkoani Tabora.
Alisema mnara wa kumbukumbu kuhusu maamuzi hayo ya busara ya TANU, upo mkoani hapo hadi sasa.
Alieleza kuwa, mnara huo unaonyesha ukumbusho wa safari kuelekea uhuru wa kisiasa.
“Leo nchi yetu inaendeleza mapambano ya uhuru wa kujitegemea kiuchumi. Tayari uhuru wa siasa tulishaupata mwaka 1961, leo tunakwenda katika mapambano ya kujitegemea uhuru wa kiuchumi.
“Uhuru wa kujenga taifa lenye uchumi jumuishi linalotegemea na linalozingatia ustawi wa watu wote. Na ndiyo maana tunasema Kazi na Utu, Tunasonga mbele,” alisisitiza.
Alibainisha kuwa, CCM inataka kujenga taifa linalojitegemea na linalozingatia ustawi wa watu.
Katika mapambano hayo, alibainisha kuwa, CCM inaendeleza yale ambayo Baba wa Taifa aliyasisitiza kwa kusema wananchi ni sisi sote kwa pamoja.
“Maendeleo ni yetu na juu yetu wenyewe. Maendeleo tunayoyataka ni maendeleo ya watu, yaletwe na watu wenyewe, yaendelezwe na watu wenyewe na yawafuate watu kule walipo,” alisisitiza.
Alisema hiyo ndiyo maana halisi ya uchumi jumuishi ambao CCM imedhamiria kuujenga kuleta maendeleo mijini na vijijini.
Dk. Samia alisema maendeleo hayo yaletwe na watu wenyewe ambao ni wananchi.
Alibainisha kuwa maeneo yote ya mkoa huo, amejionea maendeleo makubwa yaliyofikiwa.
“Jana (juzi) nilikuwa Kaliua mwaka 2023, nimeingia Kaliua jana (juzi) siyo ile niliyoiona. Kuna mabadiliko na maendeleo makubwa sana. Pia maeneo yote nikipita maendeleo yanaonekana kwa macho, tena katika sekta zote,”alisema.
MAPINDUZI SEKTA YA AFYA
Alieleza kuwa, katika sekta ya afya, elimu, maji, nishati na kilimo mambo makubwa yamefanyika.
Hata hivyo, alisema serikali inafahamu bado maendeleo hayo hayajatosheleza kwa sababu wananchi wanaendelea kuongezeka.
“Watu wanazaliwa wanakuwa wakubwa hivyo tunajua madarasa yatahitajika, vituo vya afya na matibabu yatatakiwa kila siku, maji yatahitajika, nishati itatakiwa kila siku kwa sababu maendeleo ya viwanda na mengine yanayohitaji umeme yanaendelea kukuwa ndani ya nchi yetu.
“Hivyo, Serikali ya CCM itakapopata ridhaa itasogeza karibu maji, umeme, kilimo na ufugaji. Hata shughuli za uvuvi nazo zitajumuishwa,”alisema.
Dk. Samia alisema serikali itaendelea kwenda kufanya shughuli za maendeleo kwa nguvu kubwa zaidi, kama ilivyofanya miaka mitano iliyopita.
MAENDELEO UPATIKANAJI UMEME
Pia, alisema katika Wilaya za Urambo na Kaliua, umeme ulikuwa hautoshelezi mahitaji.
Kwa sababu hiyo, alisema serikali iliahidi kujenga kituo cha kupoza umeme na sasa tatizo hilo limemalizika.
Vilevile, alisema serikali itajenga kituo cha kudhibiti mifumo ya usambazaji umeme eneo la Ziba wilayani Igunga ili kazi ya kusambaza umeme katika vitongoji itakapokamilika, vituo hivyo vitadhibiti, kupoza na kusambaza nishati hiyo.
Alibainisha kuwa, serikali imeahidi kufanya upanuzi na ukarabati kiwanja cha ndege Tabora kazi ambayo imefikia asilimia 95 huku kiwanja kikiendelea kutumika.
“Tabora tunakwenda kuwa na kiwanja kikubwa na kizuri cha kutua ndege kubwa zaidi,” alisisitiza.
MAGEUZI MAKUBWA KILIMO
Kuhusu sekta ya kilimo, alisema serikali inakwenda kuweka mkazo kutoa ruzuku kwa wakulima kuanzia mbolea, pembejeo na chanjo.
Kadhalika, alisema serikali itakwenda kufanya maboresho ya minada, ujenzi wa majosho na kutoa zaidi chanjo ya mifugo.
“Kwa upande wa kilimo cha mazao, tunakwenda kuendeleza ujenzi na ukarabati wa skimu za kumwagilia ili wakulima waweze kuzalisha mara mbili kwa mwaka.
“Kuna miradi inayoendelea kutekelezwa, itakapokamilika tunatarajia Mkoa wa Tabora uwe na maji ya kutosha. Na kila mwananchi apate maji ya kutosha,” alisisitiza.
MIKAKATI UPATIKANAJI MAJI
Alibainisha kuwa, kupitia mradi unaotoa maji Ziwa Victoria na ule wa miji 28, utakwenda kuondoa changamoto ya maji ndani ya mkoa huo.
Pia, alisema ipo miradi ya kitaifa ambayo inapita mkoani Tabora.
Aliitaja baadhi ya miradi hiyo ni ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi kutoka Uganda hadi Tanga ambao unapita katika Wilaya za Nzega na Igunga, unakwenda kuzalisha ajira kwa vijana watakaokuwa na sifa za kufanyakazi katika mradi huo.
UJENZI WA MIUNDOMBINU
Vilevile, alisema ujenzi wa reli ya mwendokasi (SGR) ambao inatoka Makutupora kuja Tabora na Tabora kwenda Isaka, utafungua fursa zaidi.
Alisema mradi huo, unapita katika Wilaya za Uyui, Urambo na Kaliua ambapo vitajengwa vituo vya kushusha na kupakia abiria.
“Katika maeneo ya vituo maendeleo mbalimbali yatakuja, biashara zitakazowekwa kupitia sekta binafsi pia maghala ya kuhifadhi bidhaa zitakazosafirishwa na reli hiyo.
“Hiyo ni ajira na fursa za biashara ambazo tungeomba wananchi wa Tabora wazitumie ili kukuza uchumi, kupata ajira na kuendeleza biashara,” alisisitiza.
Kuhusu miundombinu, Dk. Samia alisema barabara za mijini na vijijini mkoani humo zitaimarishwa.
Alisema kitaifa miundombinu hiyo iliimarishwa kwa kuongeza bajeti ya Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) kwa mwaka huu wa fedha kutoka sh. bilioni 700 hadi sh. trilioni 1.9 kufungua barabara vijijini na kujenga za mijini.
Pia, aliongeza kuwa barabara za changarawe zimejengwa maeneo mbalimbali ambazo zinapitika kwa mwaka mzima.
“Kwa hapa Tabora Manispaa nina furaha kuwajulisha tunakuja na ujenzi wa barabara mpya ya mzunguko ya Tabora Mji, tumeshaifanyia tathmini itakayokuwa na urefu wa kilometa 82.
“Ili kuhakikisha magari yote yasiyokuwa na ulazima kupita ndani ya mji wa Tabora, yapite katika barabara hiyo ya nje kwenda yanayoelekea,” alieleza.
Aliongeza: “Tunataka Tabora yenye historia kubwa iwe na hadhi kubwa pia. Katika hatua nyingine ndani ya Mkoa wa Tabora tunakwenda kujenga madaraja 133.”
Alisema madaraja hayo, yatajengwa katika barabara zilizojumuishwa katika Ilani ya uchaguzi ambazo zitajengwa.
Pia, alisema serikali itakwenda kujenga taa za barabarani 2,500 hivyo mkoa huo na wilaya zake zitapata fursa ya kufanyabiashara saa 24.
“Kwa sababu umeme ni usalama, umeme ni mwanga. Umeme unasaidia katika uzalishaji, hivyo tunakwenda kuweka mataa vijana wapate fursa kufanyabiashara saa 24.
“Barabara nilizozisema zitakuwa ni za mkakati maeneo mbalimbali ambako zimejumuishwa,” alisisitiza.
MONGELA AFUNGUKA
Awali, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara, John Mongela, alisema anachokifanya Dk Samia siyo tu kufanya kampeni bali ni kuwaunganisha Watanzania kupitia mikutano yake ya kampeni.
“Hiki unachokifanya siyo kampeni tu katika kutimiza wajibu wa mchakato wa kidemokrasia ambao nchi yetu imeamua kuusimamia kwa kumpa haki kila mtu.
Alisisitiza: “Umeamua kutumia fursa hii kuendelea kuliunganisha taifa letu, kulifanya liwe moja. Tunashuhudia, tumeona viongozi wengi wa dini, viongozi wa kimila mpaka wapinzani tumewaona.
“Hii ni ishara kwamba kwa nia yako ya dhati ya kuwaunganisha Watanzania katika mchakato wa maendeleo ya nchi yetu ni jambo ambalo umelidhamiria,” alisisitiza.
Alisema hatua hiyo inajenga heshima ya Chama, ya nchi hususan Tabora eneo ambalo ni la kihistoria.
HISTORIA YA TABORA NA SIASA NCHINI
Naye, Katibu Mkuu Mstaafu wa CCM, Dk. Bashiru Ally, alisisitiza umuhimu kwa vijana kuzingatia busara kutoka kwa wazee ambao wanamchango mkubwa katika historia ya nchi.
Dk. Bashiru alisema historia ya taifa imebebwa na busara ya wazee, hivyo vijana hawapaswi kujitenga nayo.
Mratibu huyo wa kampeni za CCM Kanda ya Kati, alisema wazee ni nguzo muhimu ya mshikamano ndani ya Chama.
Alisema maelekezo kutoka kwa Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Dk. Asharose Migiro ni kuhakikisha mabaraza ya wazee yanaendelea kushirikishwa katika kulinda misingi ya chama.
KAULI ZA WABUNGE
Mgombea ubunge wa Jimbo la Tabora Mjini, Hawa Mwaifunga, alimshukuru Dk. Samia kwa kutoa sh. bilioni 228 za utekelezaji miradi mbalimbali ya maendeleo.
Pia, alimwomba Dk. Samia kuanzisha dampo la kisasa la kuhifadhi taka ikiwa ni pamoja na kurekebisha uwanja wa michezo wa Ally Hassan Mwinyi kuwahamasisha vijana kushiriki shughuli za michezo na burudani.
Naye, mgombea Ubunge Viti Maalum Mkoa wa Tabora, Christina Mndeme, alimshukuru Dk. Samia kutekeleza miradi ya maendeleo.
Dk. Samia amehitimisha kampeni zake mkoani Tabora ambapo leo anatarajia kuanza kampeni mkoani Kigoma.