NA MUSSA YUSUPH
KIGOMA Mnashindwaje….? huo ndiyo msisitizo alioutoa Mgombea Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Rais Dk. Samia Suluhu Hassan alipokuwa akiwahutubia umati wa wananchi waliofurika katika viwanja vya Katosho katika mkutano wake wa kampeni ambao umevunja rekodi kwa kuhudhuriwa na idadi kubwa ya wananchi ikiwa ni ishara ya mapenzi yao kwa Dk. Samia.
Mapenzi ya wananchi hao kwa mgombea huyo wa Urais kupitia CCM, yalidhihirika wazi kwani maelfu ya wananchi kutoka viunga mbalimbali ya mji wa Kigoma walianza kuingia uwanjani hapo kuanzia saa moja asubuhi huku Mgombea Ubunge Jimbo la Kigoma Mjini Clyaton Chiponda maarufu kama Baba Levo akiwasili saa tatu asubuhi akiwa amepanda pikipiki ‘bodaboda’ akisindikizwa na msafara wa pikipiki na bajaji zaidi ya 500.
Saa 11:21 asubuhi, msafara wa Dk. Samia, uliwasiri uwanjani ukisindikizwa na msafara wa pikipiki, baiskeli, tarumbeta, wabeba miamvuli ambapo shangwe ilitawala kutoka kwa wananchi huku helkopta mbili iliyokuwa ikipeperusha bendera, ilinogesha zaidi mapokezi hayo ya kihistoria ambayo yamesambaratisha ngome za wapinzani.
Akihutubia maelfu ya wananchi hao, Dk. Samia alisema kwa umati uliojitokeza, hakuna sababu yeyote kwa CCM kushindwa katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29 mwaka huu.
“Kwa umati huu, CCM inashindwaje.?. Kwa wingi huu tuliojitokeza hapa na kwa kuungwa mkono na wale walioona mambo yaliyotendeka, nauliza CCM tunashindwaje?,” Dk. Samia alihoji huku umati wa wananchi wakiitikia hakishindwi.
KIGOMA SIYO MWISHO WA RELI
Dk. Samia, alisema miaka iliyopita, watu walikuwa wamezoea kusema Kigoma ni mwisho wa reli, lakini kwa kasi ya maendeleo yanayoonekana katika mkoa huo, sasa ni kitovu cha uchumi na biashara.
Alibainisha kuwa, hata ujenzi wa Reli ya Kisasa ya (SGR), haitoshia Kigoma, itakwenda hadi Burundi, kisha kufika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), hivyo mkoa huo siyo mwisho wa reli tena.
Alisema Agosti mwaka 2022, alifika wilayani Kakonko kuzindua miradi mitatu muhimu ambayo ni barabara ya Kabingo – Nyakanazi, mradi wa maji Nyamfisi na hospitali ya wilaya.
Alieleza kuwa hayo ni sehemu ya maendeleo ambayo yalianzia kipindi cha Awamu ya Tano, kisha akaikamilisha na kuzindua huku akitumia fursa hiyo kuahidi hakuna miradi itakayosimama.

“Wakati nilipokuwa Kibondo Oktoba 16 mwaka 2022, nilisisitiza kwamba kila tulichokiahidi katika awamu ya tano tunakwenda kukifanyiakazi na hakuna kitakachosimama. Kwa haya niliyoyasikia tangu nilipoingia Kigoma kwa hakika hakuna kilichosimama. Ni dhahiri kwamba serikali imetimiza ahadi zake.”
Alitaja miongoni mwa ahadi ambazo CCM na serikali yake iliweka kwa wananchi mkoani Kigoma ni kuutoa mkoa huo kutoka wa pembezoni hadi kuufanya kuwa wa kimkakati, jambo ambalo limedhihirika.
Mgombea huyo wa Urais kupitia CCM, alisema Kigoma sasa siyo mkoa wa pembezoni bali ni mkoa wa kimkakati.
“Siyo mwisho wa reli bali ni kitovu cha biashara na maendeleo. Kwa uwezo wa Mungu, tutayakamilisha hayo. Ili kulifikia lengo hilo katika miundombinu ya usafiri na usafirishaji, ambayo ndiyo muhimili mkubwa wa kukuza uchumi, tumejizatiti kuunganisha mkoa huu kwa njia zote yaani barabara, anga, reli na njia ya maji.
“Tayari maboresho ya uwanja wa ndege yanaendelea, njia tayari imeanza kutumika na jengo linaendelea kujengwa. “Mradi huu ni sehemu ya mpango mpana wa kitaifa wa kulifungua anga la Tanzania na kuimarisha shirika letu la ndege la Air Tanzania,” alisisitiza.
Alisema tayari shirika hilo, ndege zake zinatua katika mkoa huo, huku likiendelea kupanua wigo wa usafirishaji ambapo hivi karibuni linatarajiwa kuanzisha safari kwenda Lagos, Nigeria.
Alieleza kuwa, kwa sasa serikali inafanya maboresho ya viwanja vya ndege 14 ambavyo sita vimekamilika na vinane ujenzi unaendelea.
Kuhusu reli, alisema Kigoma ni sehemu muhimu ya reli ya SGR, kwani kuna vipande viwili ambavyo ni Tabora – Kigoma na kipande cha Uvinza – Msongati.
Alisema baada ya reli hiyo kufika Kigoma, itaelekea Burundi kisha kwenda mashariki mwa DRC.
“Tumekamilisha sehemu ya kwanza na ya pili (Dar es Salaam hadi Dododoma) na sehemu zote zilizobakia ya tatu, nne na tano ambayo ni Mwanza – Isaka itakamilika mwaka huu, ya sita ambayo ni Tabora – Kigoma na ya saba ni Uvinza – Msongati, kazi inaendelea.
“Sambamba na SGR, tunaiboresha reli ya zamani (MGR) kwa kununua vichwa vipya vya treni vitatu, mabehewa mapya 22 ya abiria na mabehewa ya mizigo 44.
“Vilevile jumla ya mabehewa 350 ya mizigo na 33 ya abiria, tunayafanyia ukarabati na mengi tayari yameshakamilika,” alisisitiza.
Dk. Samia, alisema kazi hiyo, imefanyika kwa kushirikiana na wabia ambao walikarabati mabehewa 68 yanayotunza ubaridi kwa ajili ya kusafirisha mazao ya matunda na mbogamboga.
Vilevile, alisema serikali imefanya maboresho ya kanuni kuhusu uendeshaji wa huduma kupitia reli ambapo sasa sheria na kanuni zinaruhusu waendeshaji binafsi kufanyabiashara katika miundombinu ya reli iliyowekwa na serikali.
Pia, alisema lengo la hatua hiyo ni kuongeza ufanisi wa usafirishaji mizigo na abiria kuwezesha mzunguko wa kasi kiuchumi.
USAFIRI NJIA YA MAJI
Kwa upande wa usafiri wa majini, alisema serikali imetekeleza miradi mikubwa katika maziwa makuu, ukiwemo ujenzi na ukarabati wa bandari, meli za abiria na mizigo.
Alibainisha kuwa, kwa upande wa Ziwa Tanganyika hususan Mkoa wa Kigoma, serikali inaendeleza ujenzi na ukarabati wa bandari za Ujiji, Kibirizi, Kabwe, Kigoma na Bandari ya Kalema iliyopo Katavi na Kasanga iliyopo mkoani Rukwa.
Aidha, alisema serikali inajenga meli nne katika Bandari ya Kalema, moja imekamilika huku zingine tatu zikiwa katika hatua mbalimbali za ujenzi.
“Matarajiao ni kwamba, meli hizi zitakapokamilika zitahudumia Tanzania na nchi jirani za DRC, Zambia na Burundi.
“Mwaka jana, tulianza ukarabati na uboreshaji meli kongwe za Mv Liemba ambayo tunatarajia kuikamilisha mwaka ujao wa fedha.
Alisisitiza: “Tunapokwenda mbele na mkitupa ridhaa yenu, tutakuwa na mradi mwingine mkubwa wa kuunganisha reli na usafiri wa meli ambapo tayari tumesaini mikataba mitatu ya ujenzi wa kiwanda cha ujenzi wa meli ambao umeshaanza kutekelezwa eneo la Katabe hapa Kigoma.
“Ujenzi wa meli mbili za mizigo, moja kwa ajili ya Ziwa Tanganyika na nyingine kwa ajili ya Ziwa Victoria.
“Ya hapa Ziwa Tanganyika itakuwa na uwezo wa kubeba tani 3,500 itakayokuwa na ghorofa moja, meli hizo maalum zitapokea shehena ya mizigo inayosafirishwa na reli ya SGR kutoka bandari za Bahari ya Hindi.
“ Hata kama ipo Bandari ya Mtwara kwa sababu, tumeiweka maalumu kwa ajili ya pembejeo za kilimo, tutashusha kule zije Dar es Salaam kisha kusafirishwa kwa SGR kwenda mikoa mingine.”
Alisema huo ndiyo mpango wa serikali katika usafirishaji kwa njia ya maji huku akibainisha miradi hiyo inaendelezwa maeneo mbalimbali nchini ikiwemo bandari za Bahari ya Hindi, Ziwa Victoria, Ziwa Tanganyika na Ziwa Nyasa.
UJENZI WA BARABARA NA UPATIKANAJI UMEME
Akizungumzia miundombinu ya barabara, alisema serikali itahakikisha inakamilika, vikiwemo vipande vilivyosalia vya barabara kuu kutoka Manyovu hadi mpakani na barabara zote zilizoahidiwa mkoani humo katika mikutano yake ya kampeni.
Alieleza kuwa, ahadi nyingine ni kuhakikisha barabara za vijijini ambazo hazipo katika mpango wa kuwekewa lami, zinajengwa kwa changarawe kuzifanya zipitike misimu yote.
Kuhusu umeme, alisema serikali inatekeleza mradi wa Mto Malagalasi ambao utazalisha megawati za umeme 49.5 kisha kujengwa msongo wa kilovoti 132 kutoka Malagalasi hadi Kidahwe wenye urefu wa kilometa 54.
Alisema umeme huo utafikishwa katika kituo cha kupoza nishati hiyo kilichopo Kidahwe na kusambazwa katika maeneo mengine ya mkoa huo.
Kadhalika, alieleza kuwa miundombinu ya umeme katika mkoa huo imefikishwa katika vijiji vyote ambapo sasa serikali inamaliza kusambaza nishati hiyo vitongojini.
Akizungumzia fidia kwa wananchi kwa waliopisha upanuzi wa uwanja wa ndege, alisema kama kuna maeneo ambayo yamechukuliwa kutoka kwa wananchi serikali italipa fidia.
“Tunafanya uchambuzi na uhakiki. Kwa zile ambazo tunahakika ndizo thamani yake, tutakuja kuzilipa. Serikali ya Chama Cha Mapinduzi haidhurumu mtu, tutakuja kuzilipa fidia zote,” alisisitiza.
KUVUTIA UWEKEZAJI
Pia, alisema uwepo umeme wa kutosha ndani ya mkoa huo utajenga mazingira rafiki kuvutia uwekezaji akitolea mfano uwekezaji mkubwa uliofanyika wilayani Kasulu wa kiwanda cha sukari ambacho kimeajiri watu 500.
Alisema kitakapoanza kufanyakazi kwa ukamilifu, kitaongeza upatikanaji sukari nchini hivyo kuleta utulivu wa bei kwa ajili ya walaji.
Dk. Samia, alisema katika mkoa huo, kuna kiwanda kikubwa cha saruji ambacho kinazalisha bidhaa hiyo kwenye soko la Kigoma na nchi jirani.
“Kwa hiyo tuna mpango wa kuvutia viwanda vingi kuja ndani ya Kigoma na hatutasahau suala la kongani za viwanda kwa vijana kuongeza thamani mazao yanayozalishwa hapa. Taifa letu tumejipanga kuhakikisha tunajitosheleza uzalishaji mafuta ya kupikia.
“Michikichi ni sehemu muhimu ya mpango huo, ninafahamu bado kuna eneo la kulima chikichi ambalo ni kubwa lakini bado halijafanyiwa kazi, vilevile uhitaji wa miche milioni moja bado hatujalifanyiakazi. Niwatake ndugu zangu wakulima wa chikichi, serikali mkitupa ridhaa tunakwenda kujielekeza kwenye kilimo cha michikichi kwa nguvu kubwa ili tupate malighafi nyingi tuweze kuvutia kiwanda cha kuchakata chikichi na kutengeneza mafuta nchini.
“Tunapokuwa na mpango huo, tutatoa ruzuku ya miche na mambo mengine yanayohitajika ili chikichi zilimwe kwa wingi tuweze kuvutia viwanda. Serikali ya CCM ina mkakati wa kuona wawekezaji wengi wanaendelea kuja Kigoma, miongoni mwa ahadi zetu ni kongani za viwanda. Uzuri hapa Kigoma soko lipo jirani na ni soko kubwa.
Alisisitiza: “Kila kinachozalishwa Kigoma kikivuka kwenda Burundi na DRC hayo ni masoko yetu makubwa sana na wala hatuwezi kukamilisha mahitaji yao, niwaombe tujielekeze huko.”

Dk. Samia alisema katika sekta ya afya, elimu, umeme na maji uwekezaji mkubwa umefanyika, hivyo ahadi ya Chama ni kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma safi za afya, elimu na kupeleka umeme katika vitongoji vyote.
Katika hatua nyingine, alisema kwa wafugaji kazi kubwa imefanyika ambapo ahadi ya serikali kwa jamii hiyo ni kuendeleza ujenzi wa majosho, mabwawa kwa ajili ya mifugo, chanjo na kuboresha machinjio.
Kwa upande wa uvuvi, alisema serikali imeanza kuleta vizimba na boti ambavyo kwa sasa katika mkoa huo vizimba 26 tayari vipo na boti mbili za uvuvi.
“Mtakapotupa ridhaa, tutaongeza mikopo kwa ajili ya boti na vizimba ili tuzidi kuvua samaki wengi kupeleka sokoni. Tutaendelea kuwawezesha wafanyabiashara na wajasiriamali wadogo.
“Pamoja na mikopo itakayotolewa na halmashauri, wakati nikizindua kampeni nilisema tutatenga sh. bilioni 200 kuwezesha upatikanaji mitaji kwa wafanyabiashara ndogondogo.
“Tumejipanga kutimiza ahadi yetu ya muda mrefu ya kuboresha vibanda vya machinga Kibirizi, kazi hiyo tumewapa Wizara ya Uchukuzi wanapoendeleza na kuboresha Bandari ya Kigoma wafanye na hilo. Mamlaka ya bandari ndiyo yenye jukumu la kuboresha vibanda hivyo na sisi tutakwenda kuwakumbusha ili waanze na hilo wakati wanaendelea na mambo mengine,” alieleza.
Akizungumzia changamoto ya mafuliko, alisema mkoa huo nyakati za masika umekuwa ukikumbwa na mafuliko hususani Kaya ya Katibuka ambapo chanzo cha tatizo hilo ni kuongezeka maji katika bwawa la Katibuka linalopokea maji kutoka maeneo mbalimbali ya mji wa Kigoma.
Aliwaambia wananchi hao kwamba tayari serikali imeanza kushughulikia kero hiyo ambapo inakwenda kuondoa kabisa changamoto hiyo.
Vilevile, alisema amepata taarifa kuhusu changamoto ya vivuko vya wananchi wa kata tatu zilizopo wilayani Kigoma ambazo zinafikika kwa njia ya maji pekee kupitia Ziwa Tanganyika, suala ambalo ameahidi kulitafutia ufumbuzi kwa kuleta kivuko bora kinachokidhi mahitaji ya wananchi.
AMSHUKURU DK. MPANGO
Awali, Rais Dk. Samia alieleza mchango wa wananchi wa mkoa huo katika maendeleo ya nchi kupitia viongozi wa kitaifa.
“Lakini kubwa ni kiongozi wa kitaifa aliyetoka mkoani humu ambaye ni ndugu yetu Dk. Philip Mpango, amekuwa kiongozi makini, mwadilifu, mchapakazi na mzalendo katika nafasi zote alizowatumikiwa Watanzania.
Aliogeza: “Kwa kweli amenisaidia sana katika kipindi cha miaka minne iliyopita na kuwa sehemu ya mafanikio yaliyopatikana ambayo mengi yametajwa. Nataka niwaambie Dk. Mpango bado ataendelea kutusaidia kama sehemu ya kutekeleza yanayokuja mbele yetu pindi mkitupa ridhaa yenu.”