Na HANIFA RAMADHANI,
Zanzibar
MGOMBEA Urais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Hussein Ali Mwinyi, ameahidi kuboresha maisha ya wazee kwa kuongeza pensheni jamii, pensheni za wastaafu na kuandaa mazingira bora ya makaazi, yatakayowapa heshima na utu katika uzee wao.
Dk. Mwinyi, ametoa kauli hiyo Mjini Unguja, wakati alipokutana na viongozi wa dini, wastaafu wa serikali na Chama, ukiwa ni mwendelezo wa kampeni zake kuelekea Uchaguzi Mkuu..
Alisema Serikali ya Awamu ya Nane, tayari imeongeza pensheni jamii kutoka shilingi 20,000 hadi 50,000, ambayo imeongezeka kwa asilimia 100 na kuongeza pensheni kwa wastaafu wa serikali, kutoka shilingi 90,000 hadi 180,000.
Aidha, alisema akipata ridhaa ya kuongoza kwa miaka mitano ijayo, serikali itaongeza kiwango hicho zaidi, kuwasaidia wazee kumudu gharama za maisha yao kila siku.
“Wazee wetu, wameitumikia nchi, sasa jukumu letu kuwapa hadhi na maisha bora. Uchumi ukiimarika, hatuna sababu ya kutoongeza pensheni zaidi.” alisema.
Aidha, mgombea huyo, alisisitiza kuwa, serikali itaendelea kuweka mazingira mazuri zaidi kwa wazee wa Sebleni na Limbani, Wete Pemba.
Aliwaomba viongozi wa dini na wazee, kuendelea kuiombea dua nchi, iendelee kuwa na amani, umoja na mshikamano, kumaliza uchaguzi kwa salama na kuiunga mkono CCM.
Alisema CCM kazi yake ni kuunganisha wananchi wa Zanzibar, bila ya kujali rangi, dini, kabila wala itikadi za kisiasa na itaendelea kufanya hivyo, kuwafanya wananchi kuwa wamoja wakati wote.
Alibainisha kuwa, Zanzibar imeendelea kuwa na hali ya amani na mshikamano mkubwa kwa wananchi wake, tofauti na ilivyokuwa miaka iliyopita, ambapo kulikuwa na mifarakano na misuguano zikiwemo nyumba za ibada na hata kifamilia.
“Tunaomba mwendele kuichagua CCM, kiendeleze mambo haya muhimu, ambayo ni tunu zetu za amani, umoja na mshikamano,” alisema.
Alibainisha kuwa, msingi wa maendeleo ya Zanzibar ni amani, umoja na mshikakamano wa wananchi wake.
Mgombea huyo, akizungumzia mafanikio yaliyopatikana katika miaka mitano iliyopita, alisema uchumi wa Zanzibar, umekua kutoka asilimia 4 hadi 7.4 katika miaka mitano iliyopita, na CCM imelenga kuongeza kasi ya ukuaji huo zaidi.
Aidha, kwa huduma za jamii, alisema serikali imejenga madarasa zaidi ya 4,800 na kuvuka lengo la 1,500, lililotajwa katika Ilani, huku skuli za ghorofa zikifika hadi vijijini na ufaulu wa wanafunzi kuongezeka.
Pia, kujenga hospitali kila wilaya na vituo vya afya katika shehia na kuendeleza ujenzi wa hospitali kwa Unguja na Pemba, lengo ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma za afya bora ndani ya nchi bila kulazimika kusafiri nje ya nchi.
Dk. Mwinyi alisema katika kuwawezesha wananchi kiuchumi, zaidi ya shilingi bilioni 39, zimetolewa kwa wajasiriamali kama mkopo usiokuwa na riba, ujenzi wa masoko mapya na itaendelea kufanya hivyo ili kuweka mazingira mazuri kwa wajasiriamali hao.
Aliahidi kuendelea kujenga barabara zote za Zanzibar na kuendeleza miradi mikubwa na huduma za kijamii ili Zanzibar iendelee kukua kimaendeleo.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Mohammed Said Mohammed (Dimwa), alisema mkutano huo, umelenga kuweka imani kwa wananchi hasa katika suala la kutunza amani, umoja na mshikamano hasa katika kipindi hichi cha kuelekea uchaguzi mkuu.
Alisema miaka mitano iliyopita chama kiliunganisha wazanzibar na wamemaliza miaka hiyo na kuanza safari nyengine kukutana na makundi hayo ili kuiombea nchi dua na kuendelea kusiisitiza amani ndani ya nchi kwani CCM kipaumbele kikubwa ni muwa na amani umoja na mshikamano kwani bila ya kuwa na amani hawatoweza kufanya ibada zao vizuri.
“CCM haina mbadala na amani yetu kwani matumaini yangu sote kwa pamoja tutaendelea kulinda amani ya nchi yetu ili tuweze kuabudu vizuri na sisi kutupa nafasi ya kufanya maendeleo, twende kwenye mahubiri yetu ambayo yataendelea kusisitiza amani” alisema.
Alisema viongozi wa ndini ndio wenye dhima kubwa ya kuelimisha waumini wao suala la kutunza amani, umoja na mshikamano.
Nao baadhi ya viongozi wa dini waliunga mkono suala la amani, umoja na mshikakamano ili Zanzibar inendelee kupiga hatua za kimaendeleo na kumhakikishia imani zao kwake kwa kumuunga mkono kwa maendeleo aliyoyaonesha.