NA MUSSA YUSUPH,
UNGUJA
MGOMBEA Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Samia Suluhu Hassan, amesema vyombo vya ulinzi na usalama vya pande zote za muungano, vipo tayari kulinda nchi wakati huu wa Uchaguzi Mkuu.
Amesisitiza kuwa amani na utulivu ni suala la kipaumbele katika kipindi hiki, hivyo yeyote asiyetaka kishindo ifikapo Oktoba 29 mwaka huu, akapige kura kisha kurejea nyumbani.
Akizungumza na maelfu ya wananchi waliokusanyika katika Uwanja wa Kajengwa, Jimbo la Makunduchi, Wilaya ya Kusini mkoani Kusini Unguja, Dk. Samia alisema utulivu wa kisiasa ni muhimu.
“Tunaingia kipindi cha uchaguzi, mwanzo nilipokuja kujitambulisha ahadi kubwa niliyoitoa ni kuifanya Tanzania iwe yenye amani na utulivu.
“Nilipotembelea kisiwa cha Pemba kubwa waliloniomba wazee wa Pemba ni kufanya uchaguzi kwa amani na utulivu, hili ndilo ninalotaka nilitilie mkazo,” alieleza.
Dk. Samia alisema wakati huu wa kuelekea uchaguzi mkuu aliwaomba wananchi kudumisha amani na utulivu.
Alisema uchaguzi siyo vita kwani uchaguzi ni tendo la kidemokrasia, watu kwenda kwa utaratibu uliowekwa kupiga kura kisha kurejea nyumbani ili nchi ibaki salama.
“Sasa siyo muda wote kushika silaha kunaleta suluhisho. Muda wowote kushika silaha iwe ya moto au ya kimila hakuwezi kuleta suluhisho. Ni waombe sana, amani na utulivu wa nchi ni jambo la muhimu zaidi kuliko mengine.

Alisisitiza: “Nataka niwatoe hofu ndugu zangu wa Zanzibar na Watanzania kwa ujumla kwamba vyombo vya ulinzi na usalama vya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na vile vya Zanzibar vimejipanga vyema kulinda nchi yetu.”
“Hutaki kishindo, kapige kura, rudi nyumbani tulia. Ni sisitize suala la amani na utulivu,” alibainisha.
KUHUSU MUUNGANO
Dk. Samia alisema kwa sasa muungano umeimarika na kuwa muungano wa undugu zaidi, kulinda uhuru na mapinduzi matukufu ya Zanzibar.
“Tumedumisha umoja, amani na utulivu nchini. Hizi ndizo tunu za msingi katika maendeleo ya Taifa letu. Kwa bidii zetu kubwa ni wahakikishie tunaendelea kulinda tunu za muungano, umoja, utulivu na amani ya nchi yetu,” alisisitiza.
Alisema tunu hizo ndizo zimejenga Taifa na utambulisho wa kipekee kimataifa kwani Tanzania imekuza uhusiano kidiplomasia, hivyo kuwa mbia muhimu mwenye kutegemewa duniani.
Mgombea huyo wa Urais alieleza kuwa, hatua hiyo imefungua milango ya ushirikiano na fursa zaidi kwa Watanzania.
“Watanzania huko duniani wakitembea kifua mbele ukiitaja Tanzania wanakuuliza Mama Samia, hivyo nasi katika kijitahada za kuhifadhi urithi na kujenga uelewa kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
“Tunakoendelea mbele tunakwenda kuanzisha kituo cha kumbukumbu na nyaraka za muungano wa Tanganyika na Zanzibar ili kiwe kituo ambacho vijana wetu na watu wanaotoka nje waingie, wasome na wajue kwamba muungano wetu una maana gani, ulianzaje na tunauendelezaje,” alisisitiza.
MAMBO YAKUJIVUNIA KWA CCM
Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC) Oganaizesheni, Issa Haji Gavu ambaye pia ni Mgombea Uwakilishi Jimbo la Chwaka alisema CCM kina mambo makubwa mawili yakujivunia.
Alisema mambo hayo yanawafanya wagombea wake kutembea kifua mbele katika kuomba kura kwa Watanzania.
Gavu aliyataja mambo hayo ni umoja na mshikamano ndani ya CCM huku jambo la pili ni utelekelezaji Ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020/2025.

“Hakuna mtu mwenye akili timamu anayeweza kudharau ama kupinga utekelezaji Ilani ya CCM.
Alibainisha: “Maendeleo yaliyofanywa na CCM kupitia Rais Dk. Samia na Dk. Mwinyi yamegonga hodi kila sehemu ya Taifa hili na yanaonekana kwa macho.”
Kadhalika, alisema akiwa na mgombea mwenza wa Urais, Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi, wamefanya mikutano ya kampeni katika mikoa 11.
Alisema katika mikoa hiyo wananchi wamedhihirisha imani yao kwa chama hicho kikongwe barani Afrika.
Gavu alisema wale wote wanaobeza kazi kubwa ya CCM ni watani tu wa CCM lakini chama hicho hakina utani katika kutafuta dola kwani itahakikisha inawashinda kwa kishindo.
Alisema CCM haichukulii uchaguzi huu kama sehemu ya kujifunza bali ni sehemu ya kuchagua amani na maendeleo ya Watanzania.
“Uchaguzi huu siyo wa kujifundisha, kwetu ni uchaguzi wa kuendelea kuchagua amani, umoja, mshikamano na maendeleo. Hayo mambo manne hayawezi kupatikana sehemu nyingine yeyote zaidi ya kuichagua CCM,” alisisitiza.
Alitoa wito kwa Watanzania kutopoteza muda kuwasikiliza wale wote wanaokebei, kupandikiza chuki, fujo na vurugu kwakuwa huko ni kuonyesha vyama hivyo vimeishiwa hoja.
Alisema CCM ndiyo Chama chenye kubeba matakwa na matarajio ya wananchi katika kuzidi kupata maendeleo ya pamoja, utulivu na amani.
KAWAIDA APONGEZA MAENDELEO
Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), Ali Mohammed Kawaida, alisema wakati wa janga la Uviko Tanzania ilipatiwa zaidi ya sh. trilioni moja kwa ununuzi wa barakoa na vifaa kinga vingine.
Alisema Dk. Samia alisema badala ya fedha hizo kutumika kununua barakoa zitatumika katika mahitaji muhimu ya wananchi kama shule, vifaa tiba, ujenzi wa hospitali, vituo vya afya na zahanati
Pia, alisema Dk. Samia alitoa zaidi ya sh. bilioni 200 kwa Zanzibar ambazo zimetumika kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa shule na hospitali.
KAULI ZA WABUNGE
Kwa upande wake, Mgombea Ubunge Jimbo la Makunduchi, Wanu Hafidh Ameir, alisema wananchi wa jimbo hilo wapo tayari kumpigia kura za kishindo Dk. Samia na mgombea Urais wa Zanzibar, Dk. Mwinyi.
Alisema wananchi wa jimbo hilo wanajivunia amani, umoja na mshikamano ambao umeimarisha uchumi wa wananchi.
“Tumeshuhudia mapinduzi makubwa katika uchumi hususan wa buluu, ongezeko la ajira kupitia uchumi wa buluu, tumeshuhudia maisha ya watu na ustawi wa jamii.
“Tumejenga shule mbalimbali kupitia mfumo wa Uviko – 19, kila mahali zimejengwa vituo vya afya. Tumeweza kuwezesha shule za kusini kuingia katika 10 bora katika mitihani ya kitaifa,” alisisitiza.

Alisema kwa baadhi ya mafanikio hayo wananchi wa kusini hawana sababu ya kutowapatia kura za kishindo wagombea hao.
Mgombea Ubunge Jimbo la Chwaka, Ramadhan Muhidin Ramadhan, alisema CCM kiendelee kutimiza yale ambayo imeyaahidi kwa wananchi ni muhimu watu kujitokeza kwa wingi kukipigia kura.
Mgombea uwakilishi Jimbo la Makunduchi, Haroun Ali Suleiman, alisema kazi kubwa imefanyika ya kuimarisha muungano na upatikanaji maendeleo ikiwemo ujenzi wa barabara.
Alisema majengo ya shule za ghorofa yamejengwa ambapo kisiwa cha Uzi kunajengwa barabara ya kwanza kuunganisha kisiwa hicho na Unguja Ukuu.
“Wananchi wa Mkoa wa Kusini tupo imara na tarehe 29 tunakwenda kukipa ushindi wa kutosha CCM,” alieleleza.
Mgombea Ubunge Viti Maalum Mkoa wa Kusini Unguja, Mwantatu Mubaraka, alisema Rais Dk. Samia na Dk. Mwinyi, wametekeleza Ilani ya CCM kwa zaidi ya asilimia 100.
Alibainisha kuwa usalama umeirishwa hali ambayo imewawezesha wananchi kufanya shughuli zao kwa amani na utulivu.