Na AMINA KASHEBA
WAKATI wadau wa masumbwi wakitoa maoni tofauti kuhusu ushindi wa Mtanzania Hassan Mwakinyo na ubora wa mpinzani wake, Stanley Eribo, takwimu zinaonyesha Mnigeria huyo ni moto wa kuotea mbali na siyo ‘dhaifu’ kama inavyodaiwa.
Mwakinyo mwenye nyota tatu na nusu katika mtandao wa boxrec alimchapa Eribo mwenye nyota moja na nusu kwa TKO raundi ya pili katika pambano lisilo la ubingwa la raundi 10, uzito wa kati lililofanyika Ijumaa iliyopita katika Ukumbi wa Warehouse, Dar es Salaam.
Katika mtanange huo uliohudhuriwa na mamia ya mashabiki, Mwakinyo alimchakaza Eribo katika raundi ya pili baada ya kumpiga ngumi ya kidevu na Mnigeria huyo kusalimu amri.
Baada ya pambano hilo, wadau wa masumbwi walitoa maoni tofauti kuhusu pambano hilo huku wengine wakidai Mwakinyo alipigana na bondia dhaifu ambaye hakuwa na ushindani.
Akizungumza baada ya pambano hilo, bondia wa ngumi za kulipwa, Mtanzania Ibrahim Mgender maarufu Ibrah Class, alidai Mwakinyo alipigana na mpinzani asiye na uwezo mkubwa katika kurusha makonde.
“Mwakinyo anawaaminisha watu ni bora kwa kuleta mabondia wasiyo na uwezo wowote, yule bondia aliyecheza naye angecheza na mimi hata raundi ya kwanza asingemaliza, hata Mfaume Mfaume (bondia) angecheza naye nina imani angempiga mapema sana,” alisema Ibrahim Class.
Hata hivyo, baadhi ya wadau wametofautiana na maoni hayo ambapo wamesisitiza kuwa Eribo ni bondia mzuri ambaye alizidiwa na maarifa ya Mwakinyo.
Bondia wa zamani na aliyekuwa bingwa wa kick boxing, Japhet Kaseba alisema Mwakinyo alipata ushindi kutokana na ubora wake wa kuwapiga wapinzani maeneo ikiwemo kidevuni.
“Mapambano mengi ya Mwakinyo amekuwa akipata ushindi wa namna ile kwa kumpiga mpinzani eneo la kidevu, hakuna ngumi inayouma kama sehemu hiyo duniani kote, ndiyo maana Eribo alishindwa kuendelea kupigana.
“Mwakinyo ameona silaha yake kubwa ni kupiga eneo la kidevuni ndiyo maana amekuwa akifanyia mazoezi ya mara kwa mara, hivyo Watanzania wanapaswa kuelewa suala hili na kuachana na kumpa lawama ambazo hazina afya katika mchezo,” alisema.
Bondia wa ngumi za kulipwa, George Mbonabucha, alisema Mwakinyo alimzidi kiwango Eribo hatua ambayo ilimpa nafasi kubwa ya kushinda na siyo mpinzani kutokuwa na uwezo wa kupigana.
“Kuwa na nyota nyingi siyo tatizo, unaweza kuwa hauna nyota hata moja katika mtandao wa boxrec unawapiga mabondia mbalimbali, watanzania wanatakiwa kuelewa Mwakinyo amejiandaa vizuri ndiyo maana amepata ushindi wa mapema,” alisema.
Mbonabucha alisema Watanzania wanapaswa kujivunia kuwa na mabondia wazuri akiwemo Mwakinyo ambao wanapata ushindi unaoleta heshima katika taifa na siyo kuwakatisha tamaa.
TAKWIMU HIZI HAPA
Wakati baadhi ya wadau wakitilia shaka uwezo wa Eribo, takwimu za mtandao wa boxrec zinaonyesha kuwa, Mnigeria huyo kabla ya kukutana na Mwakinyo, hakuwahi kupoteza katika mapambano 10 yaliyopita.
Katika mapambano hayo, Eribo alishinda mara tisa na kutoka sare mara moja hatua ambayo inamfanya bondia huyo kuwa na rekodi nzuri.
Eribo mwenye umri wa miaka 36, alitoka sare na Prince Bakattah kutoka Ghana huku akiwapiga Saheed Lawal (Nigeria), Djamiou Ekpesso (Benin), Ramadhani Shauri (Tanzania), Isaac Sowah (Ghana), Dele Adeleke (Nigeria), Sunday Olalekan (Nigeria), Isiaka Malik (Nigeria), Saheed Olayiwola (Nigeria)na Yaw Sakiya (Ghana).




