Na AMINA KASHEBA
WAKATI timu ya Simba Queens ikifurahia ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Yanga Princess, wapinzani wake hao wamelia na makosa madogo yaliyofanywa na wachezaji wake.
Simba Queens ilipata ushindi huo katika mchezo wa Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania Bara uliopigwa katika Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.
Akizungumza Dar es Salaam, Kocha wa Simba Queens, Mussa Hassan ‘Mgosi’, alisema ubora na utulivu wa wachezaji wake ndiyo sababu ya kuvuna pointi tatu muhimu.
“Niwapongeze wachezaji wangu, walifuata kile tulichofanya katika uwanja wa mazoezi. Ili uwe bingwa unapaswa kuzifunga timu bora na kupata ushindi katika kila mchezo, ikishindikana sana basi hata sare,” alisema.
Kocha huyo alisema kikosi chake kilikuwa bora kimbinu zaidi wa wapinzani wake hatua ambayo pia iliwaongoza kupata ushindi huo.
Naye Kocha wa Yanga Princess, Edna Lema alisema kilichosababisha hadi kufungwa ni wachezaji wake kufanya makosa ambayo wapinzani wao waliyatumia na kupata ushindi.
“Makosa madogo madogo yamesababisha hadi kupoteza mchezo kwani wachezaji wangu hawakuwa makini, lakini niwapongeze kwa kuonyesha ushindani mbele ya mtani kwa sababu mechi ilikuwa ngumu,” alisema..
Kutokana na matokeo hayo, Simba Queens ipo kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania Bara ikiwa na pointi 15 wakati Yanga Princess ikiwa nafasi ya tatu kwa alama 12, zote zikicheza mechi tano.




