Dodoma
NA FRED ALFRED
WAZIRI Mkuu Dk. Mwigulu Nchemba, amezitaka taasisi za elimu nchini kutowazuia wanafunzi kufanya mitihani ya masomo yao kwa kushindwa kulipa ada.
Pia, amesisitiza kuwa serikali itaendelea kuongeza fedha za mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu na vyuo vya kati ili wanafunzi wengi zaidi wanufaike.
Dk. Mwigulu ametoa maelekezo hayo bungeni jijini Dodoma, katika kipindi cha maswali kwa Waziri Mkuu, alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Latifa Juwakali, aliyetaka kujua mkakati wa serikali kuhusu wanafunzi wanaozuiwa kufanya mitihani kwa kutolipa ada.
Akijibu swali hilo, Waziri Mkuu Nchemba amezihimiza taasisi za elimu kuzingatia utaratibu wa kutowazuia wanafunzi kufanya mitihani.
“Mitihani ni jambo la maandalizi, mwanafunzi anakuwa ameshajiandaa, yupo tayari kwa mitihani na jambo la ada siyo la kwake. Kwa hiyo anapata adhabu kutokana na hali halisi ya kimaisha ya familia yake, hili ni jambo ambalo siyo jema,” alisisitiza.
Alisisitiza: “Turejee kwenye ule utaratibu mitihani ikifika wanafunzi wafanye mitihani, wapimwe, kwa sababu hawapimwi kwa ada, wanapimwa kwa maandalizi ya mafunzo waliyoyapata na utaratibu ule wa kwamba atakapohitaji cheti chake lazima awe amemaliza mahitaji yote ya kimalipo ambayo alitakiwa kuyafanya.”
Pia, alizitaka taasisi hizo kuendelea kuwashirikisha na kuwakumbusha wazazi mara kwa mara kwamba kuna mahitaji ya kifedha ambayo wanafunzi hawajayamalizia ili walipe bila kuathiri masomo ya wanafunzi.
“Anayelipa ada ni mzazi, siyo mwanafunzi, jukumu la mwanafunzi ni kusoma pamoja na ukweli kwamba vyuo vinatakiwa kupata fedha ili viweze kujiendesha, lakini ufanyike utaratibu mzuri kama ilivyokuwa ikifanyika,” alisema.
Akizungumza kuhusu mikopo ya elimu ya juu, Waziri Mkuu alisema serikali itaendelea kuongeza fedha kwa kuwa tangu Serikali ya Awamu ya Sita iingie madarakani fedha zimeongezeka mara mbili kutoka sh. bilioni 400 hadi sh. bilioni 900.
Katika hatua nyingine, Dk. Mwigulu aliwahimiza waliowahi kunufaika na mikopo hiyo kurejesha kwa wakati ili wanafunzi wengi zaidi wanufaike.




