Na MWANDISHI WETU
MKUTANO wa 32 wa Baraza la Uongozi la Shirika la Forodha Duniani Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika (WCO ESA) umefunguliwa rasmi Mei 14, 2026 katika visiwa vya Zanzibar na Mgeni Rasmi Waziri wa Fedha wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (JMT), Balozi Khamis Mussa Omar, kwa kushirikisha wajumbe kutoka nchi mbalimbali wanachama wa kanda hiyo.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano huo, Balozi Omar, amesema Tanzania ina historia kubwa katika maendeleo ya mifumo ya forodha Afrika Mashariki, akieleza kuwa eneo hilo lilikuwa kitovu muhimu cha biashara na miongoni mwa maeneo ya mwanzo kuanzisha idara ya forodha katika ukanda huo tangu mwaka 1896.
Aidha, amesema dunia inaendelea kukabiliwa na mabadiliko makubwa katika biashara ya kimataifa yanayochochewa na maendeleo ya teknolojia, matumizi ya akili mnemba (AI), biashara mtandao pamoja na changamoto za kiusalama, hali inayozifanya mamlaka za forodha kuwa na jukumu kubwa zaidi katika kulinda uchumi wa nchi na kurahisisha biashara halali.
Balozi Omari amesisitiza umuhimu wa nchi wanachama kuendelea kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kimataifa kupitia mifumo ya kisasa ya kidijitali, usimamizi wa vihatarishi pamoja na matumizi ya teknolojia za ukaguzi zisizoingilia bidhaa ili kuongeza ufanisi katika udhibiti wa mipaka na ukusanyaji wa mapato.
Kwa upande wake, Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Yusuph Juma Mwenda, emeeleza kuwa TRA imeendelea kufanya maboresho makubwa ya mifumo ya forodha kupitia uwekezaji katika mifumo ya kidijitali, uimarishaji wa mifumo ya usimamizi wa mizigo pamoja na kuunganisha huduma za forodha katika dirisha moja la utoaji huduma kwa lengo la kuongeza uwazi, ufanisi na kurahisisha biashara.
Mkutano huo wa WCO ESA unawakutanisha Wanachama kutoka Mataifa 24 na kujadili masuala mbalimbali ya ushirikiano wa forodha, mageuzi ya kidijitali, usalama wa mipaka, uboreshaji wa biashara na namna bora ya kukabiliana na changamoto zinazoikabili sekta ya forodha duniani huku ukilenga kuimarisha ustawi wa uchumi wa nchi wanachama wa ukanda huo.




