Na NASRA KITANA
BAADA ya kupata sare ya bao 1-1 dhidi ya Al Ahly, kocha mkuu wa Yanga, Pedro Gonçalves amesema mechi na AS FAR Rabat ni fainali kwao.
Kikosi cha Yanga kiliondoka nchini kuelekea Morocco kwa ajili ya mchezo wake wa tano wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya FAR Rabat ya Morocco utakaopigwa Februari 7, mwaka huu katika Uwanja wa Stade Olympique, Rabat.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Pedro alisema wanakwenda nchini humo mapema ili kuzoea hali ya hewa ya huko na kupata muda mzuri wa kukijenga kikosi chake
“Mechi hiyo ni muhimu kwetu kuhakikisha tunapata ushindi ili kujihakikishia nafasi ya kutinga hatua ya robo fainali ya mashindano hayo muhimu.
“Tumejipanga vizuri kuelekea katika mchezo huo, kwani tunaendea kucheza kama fainali ya kufa au kupona, lengo letu ni kusonga mbele,” alisema Pedro.
Kocha huyo alisema hana hofu kwani anajivunia kuwa na wachezaji bora ambao wana hali ya kujiamini na kupata matokeo.
MZIZE
Hata hivyo, Pedro alisema kuwa nyota wake Clement Mzize tayari amerejea katika mazoezi na ndio wiki yake ya kwanza hivyo anaimani kubwa atakuwa vizuri katika mechi zinazofuata.
HERSI SAID
Rais wa klabu hiyo, Mhadisi Hersi Said alisema kikosi cha Yanga kinakwenda nchini humo kuhakikisha kinapambana kupata ushindi na kusonga mbele.
“Tunajua utakuwa mchezo mgumu kwetu, lakini tutapambana mwanzo mwisho ili kupata matokeo mazuri,” alisema Hersi.
Naye Ofisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe alisema kuwa wachezaji wanafahamu umuhimu wa mchezo huo, ana imani kuwa watapambana kupata ushindi.
Alifafanua kuwa wachezaji wanajua kuna raha ya kufuzu robo fainali hasa wakiwa ugenini.
“Wachezaji wamekewa zawadi nono endapo watapata matokeo mazuri ugenini na kufanikiwa kutinga robo fainali ya mashindano hayo, tuna wachezaji wakubwa na wenye uwezo wa kutupa matokeo, sisi raha yetu ni kuona tunafuzu tukiwa ugenini,” alisema.
Kamwe alisema kuwa wana imani kubwa na kikosi chao kuwa kinaenda kuwapa raha mashabiki na wapenzi wa timu hiyo na Watanzania wote kwa jumla.
Kikosi kilichoondoka ni makipa, Djigue Diarra, Hussein Masagala, Abdultwalib Mshery, Israel Mwenda, Yao Kouassi, Ibrahim Bacca, Frank Assinki, Dikson Job, Chadrack Boka, Mohamed Hussein, Aziz Andambwile na Damaro Camara.
Wengine ni Duke Abuya, Lassine Kouma, Maxi Nzengeli, Mudathir Yahya, Allan Okello, Edmund John, Pacome Zouzoua, Emmanuel Mwanengo, Laurindo Aurelio ‘Depu’, Prince Dube na Clement Mzize.
Kwa sasa, msimamo wa Kundi B wa Ligi ya Mabingwa Afrika unaongozwa na Al Ahly yenye pointi nane, ikifuatiwa na Yanga yenye pointi tano sawa na FAR Rabat huku JS Kabylie ikiwa na pointi 2.




