Na MUSSA YUSUPH,
UNGUJA
MGOMBEA Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Samia Suluhu Hassan, amesema amedhamiria kujenga taifa imara, litakalofungua fursa zaidi kwa vijana kufanya kazi zitakazowaingizia kipato, kujiegemea kiuchumi.
Dk. Samia alisema hayo alipozungumza na maelfu ya wananchi katika mkutano wa kampeni za Uchaguzi Mkuu za CCM, uliofanyika Uwanja wa Hamburu, Jimbo la Nungwi Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Alieleza kufikia hatua hiyo, lazima kila mwananchi hususan vijana wawe na shughuli zitakazowapa kipato.
“Na hii ndiyo kazi inayoendelea kufanywa na CCM, kuandaa mazingira rafiki kwa vijana kuwa na shughuli za kufanya, kila mmoja awe na kipato mweyewe, asimame, ajitegemee.
“Kuweka mazingira kwa vijana wetu kuwa na shughuli za kujishughulisha kuingiza kipato, kila mmoja ainue ustawi wa maisha yake, ndiyo tunasema, Kazi na Utu, Tunasonga Mbele,” alisisitiza Dk. Samia.
WAGOMBEA UBUNGE WAZUNGUMZA
Wakizungumzia maendeleo aliyopatikana pande zote za Muungano, baadhi ya wagombea ubunge kutoka majimbo mbalimbali visiwani hapa, walisema kazi kubwa imefanyika kuimarisha amani, utulivu, hivyo kuchochea maendeleo kila sekta.
Mgombea Ubunge wa Jimbo la Chaani, Ayoub Mohammed Mahmoud, alisema wananchi wanawapongeza Rais Dk. Samia na mgombea urais wa Zanzibar kupitia CCM, Dk. Hussein Ali Mwinyi kwa kuongoza mapambano ya maendeleo katika miaka mitano.
Alisema katika mapambano hayo, wamefaulu kuwaletea maendeleo wananchi wa pande zote za Muungano.
“Upande wa elimu ya juu, mimi ni mlezi wa TAHLISO (Shirikisho la Wanafunzi wa Elimu ya Juu) nimeshuhudia uamuzi wetu wa kuhakikisha mnatoa fedha za mikopo kwa wanafunzi wa diploma umesaidia wazazi.
“Uamuzi huu umesaidia watoto wa familia za kinyonge kupata elimu. Nyie ni majemedari, wapo waliojaribu kututikisa nyie hamkutikisika. Mmekuwa mstari wa mbele kutuongoza,” alieleza.
Kwa upande wake, mgombea ubunge wa Jimbo la Donge, Sadifa Juma Khamis, alisema katika jimbo hilo tayari CCM ina uhakika wa kura za kutosha.
“Wananchi wamesema kura zote wanakwenda kumpigia Dk. Samia kwa upande wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Dk. Mwinyi kwa Zanzibar. Hii ni kwa sababu mara ya kwanza miradi mikubwa ya maendeleo inatekelezwa kwa pamoja.
“Katika sekta ya afya kuna hospitali za kisasa kama hoteli za nyota tano. Kwa wajasiriamali tulizindua Soko la Chuini, juzi kuna Mzungu alipotea akidhani anaingia hotelini kumbe ni soko,” alisema.
Alisema hizo ndizo salamu za wananchi wa Zanzibar kwa sababu Ilani ya Uchaguzi ya CCM imetekelezwa kwa zaidi ya asilimia 100.
Mbunge wa Viti Maalumu, Riziki Pembe Juma, alisema Dk. Samia na Mwinyi wanapaswa kuungwa mkono kwa kasi ya maendeleo yaliyopatikana.
“Ninawaomba viongozi wangu mtembee kifua mbele, sisi wanawake tutapita kichochoro kwa kichochoro, mitaa kwa mitaa kuzisaka kura, viongozi hawa tulionao wanatosha na chenji inabaki,” alisisitiza.