Na MUSSA YUSUPH,
Zanzibar
MGOMBEA Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Samia Suluhu Hassan amesema Mgombea Urais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi, ndiye mgombea sahihi atakayeshirikiana naye, kuleta maendeleo kwa manufaa ya pande mbili za Muungano.
Pia, Dk. Samia, amesema matokeo ya ukuaji uchumi na utekelezaji ahadi za CCM kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita, umeonekana dhahiri uwezo wa kiongozi huyo katika kuwaongoza Wazanzibari.
Akizungumza na maelfu ya wananchi waliofurika katika mkutano wa kampeni uliofanyika Uwanja wa Hamburu, Jimbo la Nungwi, Mkoa wa Kaskazini Unguja, Dk. Samia, alisema maendeleo makubwa yameshuhudiwa Zanzibar.
“Pamoja na majanga yote tuliyopitia ikiwemo Covid, tumeweza kufanya kazi kubwa pamoja katika sera za kifedha na uchumi, ndiyo maana hatukukwamisha miradi yetu.
“Katika sera za kifedha na sera za kiuchumi, Dk. Hussein ameweza kusimamia na kuimarisha uchumi ambao kwa sasa unakuwa kwa kasi kubwa,” alisisitiza.
Dk. Samia, alibainisha ukuaji uchumi kwa Tanzania bara, umeongezeka kwa asilimia sita, huku Zanzibar ukiwa juu zaidi kwa asilimia 7.1 kwa mwaka.
“Zaidi uchumi umekua hata mifukoni kwa kila mwananchi. Wakati nilipokuwa nikiwasili Nungwi, nilikuwa nikitazama kila pande na kujionea namna ambavyo kumejengeka nyumba nzuri za makazi, biashara zinafanyika na mambo yanakwenda vyema kwa amani na utulivu,” alisisitiza.
ONGEZEKO LA WATALII
Kuhusu ukuaji utalii, Dk. Samia, alisema idadi ya watalii, imeongezeka, watalii zaidi ya milioni tano wamefika Tanzania bara, huku zaidi ya watalii 700,000 wamefika visiwani Zanzibar, ikiwa ni zaidi ya lengo.
CCM HAINA SHAKA NA USHINDI
Katika hatua nyingine, Dk. Samia, alisema CCM haina shaka katika kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, mwaka huu, kwa sababu mambo mengi yamefanyika.
“CCM tuna ujasiri kuja kwenu kuomba kura na ujasiri huu, unatokana na kwamba, tumefanya mambo makubwa na tunajiamini tutaweza kufanya mambo makubwa.
“Ndiyo maana tunakuja kwenu kwa kujiamini kuomba kura, mtuchague tena twende tufanye mambo makubwa zaidi kama alivyosema Dk. Mwinyi,” alisisitiza.
VIPAUMBELE
Dk. Samia, alibainisha mambo muhimu yatakayopewa kipaumbele katika kuyatekeleza kwa Watanzania baada ya CCM kupewa ushindi wa kishindo.
Aliyataja mambo hayo ni kuendelea kukuza uchumi na kipato cha wananchi, kuinua maisha ya Watanzania na kuimarisha ustawi wa jamii.
Mambo mengine ni kulinda amani na utulivu nchini, kudumisha demokrasia na utawala bora na kujenga Taifa linalojitegemea.
Kuhusu suala la kujenga Taifa linalojitegemea, Dk. Samia alibainisha kufikia hatua hiyo, lazima kila mwananchi hususan vijana awe na shughuli itakayompa kipato.
“Na hii ndiyo kazi inayoendelea kufanywa na CCM ya kuandaa mazingira rafiki kwa vijana kuwa na shughuli za kujishughulisha kila mmoja awe na kipato yeye mweyewe asimame ajitegemee na ndiyo kazi tunayoendelea kuifanya.
“Kuweka mazingira kwa vijana wetu kuwa na shughuli za kujishughulisha kuingiza kipato kila mmoja ainue ustawi wa maisha yake na ndiyo tunasema, Kazi na Utu, Tunasonga Mbele,” alisisitiza Dk. Samia.
Akizungumzia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), Dk. Samia, alisema kwa kushirikiana na Dk. Mwinyi, wameinua maendeleo ya watu kutoka kaya maskini kupitia TASAF.
Alisema hivi sasa, watu hao wameweza kujitegemea kimaisha, serikali itakuja na awamu nyingine ya mradi huo unaogusa pande zote za muungano.
ROYAL TOUR ILIVYOFUNGUA NCHI
Katibu Mkuu wa CCM, Dk. Asha-Rose Migiro, alisema mafanikio yaliyopatikana kupitia filamu ya Tanzania The Royal Tour chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia na Dk. Mwinyi ni miongoni mwa sababu wagombea hao kupewa kura za kishindo.
Dk. Migiro alisema mafanikio ya Royal Tour yameongeza thamani ya utalii, kuimarisha uchumi na kuonesha wazi dira ya maendeleo ya viongozi hao.
“Katika kazi nyingi walizofanya, hatuwezi kusahau mchango mkubwa wa Rais Dk. Samia katika kuandaa filamu ya Royal Tour. Ilikuwa kielelezo cha kuipeleka Tanzania kiuchumi na leo tumeona matokeo yake,” alisema Dk. Migiro.
Aliongeza kuwa Zanzibar imenufaika zaidi kupitia filamu hiyo kwani ni kisiwa chenye utajiri wa viungo, manukato na vivutio vya kipekee vinavyoongeza mvuto wa kitalii duniani.
“Ulipokuwa Waziri wakati wa Rais Karume, ulitangaza vyema Zanzibar na sasa uzoefu huo umetumika kwenye Royal Tour. Mwinyi ameendeleza misingi hiyo na utalii leo ni injini ya uchumi wa kisasa,” alisema.
Alisisitiza wagombea wa CCM, Dk. Samia na Dk. Mwinyi wanatekeleza kwa vitendo kauli mbiu ya ‘Kazi na Utu’ ambapo wameweka msisitizo kupitia uwekezaji wa rasilimali watu, elimu, afya na maji.
“Dk. Samia ameonesha kwa dhati anataka kuitimiza kaulimbiu ya kazi na utu. Tumeona jitihada katika kupunguza vifo vya mama na mtoto, elimu, maji na afya. Haya ni mafanikio yasiyopingika,” alisema.0
Dk. Migiro alimpongeza Dk. Mwinyi kwa kuimarisha miundombinu, akitolea mfano ujenzi wa barabara na miradi ya mbalimbali.
Alibainisha wananchi wameanza kumuita ‘Hussein Mabati’ kutokana na mabati mengi yanayozungushiwa katika maeneo ambayo miradi ya maendeleo inatekelezwa.
“Ujenzi wa kisasa unaendelea. Zanzibar inaelekea kuwa na uchumi wa kisasa. Tuna kila sababu ya kuwaunga mkono wagombea hawa,” alisisitiza.
WABUNGE WAELEZA
Kwa upande wake, Dk. Khalid Salum Mohammed, alisema kazi kubwa imefanyika kuimarisha amani na utulivu.
Alimpongeza Dk. Samia kwa kuimarisha siasa za kikanda na kimataifa, hali iliyosaidia kuongeza kasi ya utekelezaji miradi ya maendeleo pande zote za Muungano.
“Kwanini tunasema miaka mitano tena ni kwa sababu kwa haya yaliyofanyika, tutarajie makubwa zaidi yatafanyika katika miaka mitano ijayo,” alieleza.
Mgombea Ubunge, Jimbo la Chaani, Ayoub Mohammed Mahmoud, alisema wananchi wanawapongeza wagombea hao kupitia CCM kwa kuongoza mapambano ya maendeleo katika miaka mitano.
Alisema katika mapambano hayo wamefaulu kuwaletea maendeleo wananchi wa pande zote za Muungano.
“Upande wa elimu ya juu, mimi ni mlezi wa TAHLISO (Shirikisho la Wanafunzi wa Elimu ya Juu) nimeshuhudia uamuzi wenu wa kuhakikisha mnatoa fedha za mikopo kwa wanafunzi wa diploma umesaidia wazazi.
“Uamuzi huu umewasaidia watoto kutoka familia za kinyonge kupata elimu. Nyie ni majemedari, wapo waliojaribu kututikisa nyie hamkutikisika. Mmekuwa mstari wa mbele kutuongoza,” alieleza.
Kwa upande wake, mgombea Ubunge Jimbo la Donge, Sadifa Juma Khamis, alisema katika jimbo hilo tayari CCM ina uhakika wa kura za kutosha.
“Wananchi wamesema kura zote wanakwenda kumpigia Dk. Samia kwa upande wa Tanzania na Dk. Mwinyi kwa Zanzibar. Hii ni kwa sababu mara ya kwanza miradi mikubwa ya maendeleo inatekelezwa kwa pamoja.
“Katika sekta ya afya kuna hospitali za kisasa kama hoteli za nyota tano. Kwa wajasiriamali tulizindua Soko la Chuini, juzi kuna Mzungu alipotea akidhani anaingia hotelini kumbe ni soko,” alisema.
Alisema hizo ndizo salamu za wananchi wa Zanzibar kwa sababu Ilani ya Uchaguzi ya CCM imetekelezwa kwa zaidi ya asilimia 100.
Mbunge mteule wa Viti Maalumu, Riziki Pembe Juma, alisema Dk. Samia na Dk. Hussein, wanapaswa kuungwa mkono kwa kasi ya maendeleo yaliyopatikana.
“Ninawaomba viongozi wangu mtembee kifua mbele, sisi wanawake tutapita kichochoro kwa kichochoro, mitaa kwa mitaa kuzisaka kura, viongozi hawa tulionao wanatosha na chenji inabaki,” alisisitiza.