Na HANIFA RAMADHANI,
Zanzibar
MGOMBEA Urais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema msingi wa maendeleo ya nchi yoyote duniani, unatokana na amani, umoja, mshikamano na maridhiano.
Amesema kutokana na hilo, alipoingia madarakani mwaka 2020, jambo la kwanza aliloimarisha, lilikuwa mshikamano, maridhiano na kuendeleza Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Dk. Mwinyi, alisema hayo, katika mkutano wa kampeni za Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, uliofanyika Viwanja vya Mnarani, Nungwi, Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Alisema bila ya amani, umoja, mshikamano na maridhiano, hakuna jambo lolote la maendeleo litakalofanyika nchini.
Mgombea huyo, alisema hiyo ndiyo sera mama kwa Serikali na Chama Cha Mapinduzi, hivyo aliwahimiza wagombea ubunge, uwakilishi na udiwani wanaposimama majukwaani, waendelee kuhimiza suala hilo, kila dakika nchi iendelee kuwa na amani na kukua kimaendeleo.
Akizungumzia Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2020/2025, Dk. Mwinyi, alisema Chama kiliinadi kwa wananchi miaka mitano iliyopita, wameitekeleza kwa asilimia kubwa, hivyo kuwaonesha kwa vitendo kwamba, CCM ikiahidi, inatekeleza.
“CCM ni Chama imara, kwani tuliahidi tumetekeleza na kuvuka Ilani yetu, ninawaahidi miaka mitano ijayo, yajayo ni neema zaidi,” aliahidi.
Aliwasisitiza wanachama wa CCM na wananchi, kujitokeza kwa wingi kupiga kura Oktoba 29, mwaka huu na kukichagua Chama, kipate ushindi wa kishindo.
“Hamasa za kujitokeza kwa wingi katika mikutano ni jambo moja, lakini uchaguzi ni kupiga kura, tuhakikishe tunajitokeza kwa wingi, Chama kishinde kwa kishindo,” alisisitiza.
Dk. Mwinyi, alimwombea kura Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia, yeye na wagombea wa ubunge, uwakilishi na udiwani wa CCM.
Naye, Mgombea Uwakilishi kupitia nafasi za wanawake, Mkoa wa Kaskazini Unguja, Riziki Pembe Juma, aliwasisitiza wananchi, kuendelea kutunza amani, kwani ndiyo inayowaletea mafanikio na kutambua ikipotea, kinamama na watoto ndiyo wanaohangaika.
Alisema kinamama, wamejipanga kuhakikisha wanasaka kura kwa kuwatoa watu majumbani, kwenda kuipiga kura CCM iendelee kushinda kwa kishindo.
Kwa upande wake, Mgombea Uwakilishi wa Jimbo la Kijini, Badria Attai Masoud, alimpongeza Dk. Samia kwa kudumisha Muungano na kuondoa hoja zaidi ya 15, huku akitekeleza miradi ya maendeleo.
Pia, alimpongeza Dk. Mwinyi kwa kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM kwa asilimia kubwa, ukiwemo ujenzi wa barabara zinazokwenda Kijiji cha Kijini.




